Kwa Prof. Maghembe ‘kwachafuka’


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 07 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Ndani ya Jamii
Profesa Jumanne Maghembe

JIMBONI Mwanga, katika mkoa wa Kilimanjaro, kwa Profesa Jumanne Maghembe, hakukaliki. Ni malumbano na tuhuma. Kambi za wagombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinakabana koo.

Kuna madai ya kugawa rushwa usiku na mchana. Kuna tuhuma za kutumia udini. Nani anatoa rushwa ni jambo ambalo viongozi wa CCM wamekataa kuweka wazi.

Mpaka sasa aliyetangaza kumvaa Profesa Maghembe jimboni Mwanga ni wakili wa kujitegemea Joseph Thadayo.

Katibu wa CCM wilaya ya Mwanga, Sidael Goroi anakataa kuzungumzia uvumi na tuhuma za rushwa na udini. Anasema yeye hapaswi kuzungumzia hilo magazetini, isipokuwa kwenye vikao halali vya chama chake.

Bali MwanaHALISI iliongea na Prof. Maghembe.

Mwandishi: Mheshimiwa Profesa, kuna madai kuwa wewe na mtangaza nia kugombea ubunge jimboni kwako, mnatoa rushwa…

Pfof. Maghembe: Wanaoelewa vema suala hili ni wananchi. Nenda ukawalize.

Mwandishi: Sisi tunataka kauli yako mwenyewe. Wananchi tutawauliza tu na baadhi tumekutana nao tayari.

Pfof. Maghembe: Mdogo wangu, kila kitu kinafahamika na wanaoendesha kampeni chafu wanajulikana. Lakini nataka uelewe kuwa siyo mimi wala wale wanaopenda niendelee na ubunge baada ya uchaguzi mwaka huu.

Mwandishi: Uendelee? Utagombea tena? Mbona kuna wanaodai kuwa hukuleta maendeleo jimboni?

Pfof. Maghembe: Narudia. Wewe waulize wananchi wenyewe; watakueleza kama kuna jambo lolote la maendeleo nimefanya au hakuna.

Mwandishi: Wanaodai hivyo ni wananchi pia kutoka jimboni kwako.

Pfof. Maghembe: Wewe unajua. Watu wote hawawezi kufikiri kumoja hata kama wamezaliwa na wazazi walewale; na katika siasa, hasa penye misukumo ya hayo unayoniuliza, hakika chochote kinaweza kusemwa. Nakuhakikishia kuwa nimefanya mengi…nenda jimboni ukajionee.

Thadayo hakuweza kupatikana kujadili suala la rushwa na udini katika kampeni. Mwandishi alipiga simu Na. 0754 255299 aliyoambiwa ni ya Thadayo aliyetangaza nia ya kugombea Mwanga na kuongea na aliyejitambulisha kuwa mgombea mtarajiwa.

Mwandishi: Mheshimiwa Thadayo…

Thadayo: Naam!

Mwandishi: Mimi ni mwandishi wa habari. Naomba nikutana nawe.

Thadayo: Ninaendesha gari. Nitakupigia baada ya dakika tano.

Hakupiga. Mwandishi alipiga simu ileile baada ya saa mbili.

Thadayo: Unasema wewe ni mwandishi wa gazeti gani?

Mwandishi: MwanaHALISI.

Thadayo: Nitakutafuta; nitakupigia (Akakata simu. Hajapiga hadi sasa).

Mhariri wa gazeti hili alipopiga simu hiyo hiyo Jumapili, aliyepokea aliitikia lakini alikata simu na juzi Jumatatu alipiga tena lakini alijibiwa na mtu aliyesema yeye siyo Thadayo bali Zakayo.

Haijafahamika iwapo aliyekuwa anaongea na waandishi alikuwa kweli Zakayo; lakini katika mfumo wa usajili wa simu, siyo vigumu kuthibitisha nani hasa mmiliki wa simu hiyo.

Mwandishi alipata namba ya simu ya Thadayo kutoka kwa diwani mmoja mjini Mwanga (jina tunalo).

Taarifa zinasema vikao vya kampeni hufanyika usiku na mchana na kugawa vitu mbalimbali vikiwamo vyakula na nguo.

Mkazi mmoja wa Mwanga ameliambia gazeti hili kuwa alihudhuria kikao ambacho kilifanyika nyumbani kwa mfanyabiashara mmoja (jina tunalo) katika kijiji cha Ngulu, kata ya Kwakoa na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 40.

Veneranda Jackson (49), mwenyekiti wa kikundi cha wanawake wa sokoni kata ya Lembeni, kilometa 19 kutoka mjini Mwanga, anakiri kikundi chao kupelekewa mifuko ya unga wa ngano na mpambe wa mgombea mmojawapo.

“Tuliletewa mifuko mitatu ya unga wa ngano yenye ujazo wa kilo 25 kila mfuko. Lakini hatukuutumia hata mfuko mmoja kwa sababu tuliona hiyo ni rushwa,” anasimulia Veneranda. Anasema alipeleka mifuko hiyo kwa diwani.

Alipoulizwa iwapo yuko upande wa Prof. Maghembe au Thadayo, Veneranda alisema, “Wewe umekuja kuchukua ushahidi hapa? Ulichouliza ndicho umejibiwa. Kama unataka mengine waulize wengine labda watakwambia.”

Saidi Daudi Mbelesero, naye wa Lembeni, anakiri kukabidhiwa mifuko 148 ya ngano, vitenge zaidi ya doti 200 na kadi feki 100 za CCM.

Anasema hata kadi 100 zilizolipiwa kwa mwaka mzima alizopewa ili azigawe bure, hakuzigawa, bali alizipeleka kwa diwani wa kata.

Kwa upande wake, diwani Mamboleo Teli ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mwanga, amethibitisha tukio la ugawaji ngano.

Kuhusu wanaolalamika kwamba jimbo hilo halina maendeleo, Teli anasema, “Katika halmashauri yangu kuna kata 22 na hakuna hata kata moja iliyosahauliwa na mbunge huyu. Wanaosema hakuna maendeleo aliyoyaleta wana lengo lao, lakini wananchi wanajua anachokifanya.”

“Prof Maghembe aliingia madarakani mwaka 2000 kukiwa na shule 93 za msingi, yeye akasimamia zikajengwa shule 16 na sasa zipo 109.

Shule za sekondari za serikali zilikuwa 8 sasa zipo 26. Kulikuwa na zahanati 33 sasa zipo 48, vituo vya afya vilikuwa 35 na sasa vipo 52. Sasa watasemaje hajafanya kitu?” anahoji diwani Teli.

Katika suala la rushwa, Mzee Peter Kisumo, mmoja wa wadhamini wa CCM, anakiri kuwepo kile alichoita “kampeni chafu” hata kabla ya kipenga cha kuanza kampeni kupulizwa. “Sijawahi kuona siasa chafu katika jimbo hili kama hizi za mwaka huu,” anasema Kisumo.

Alisema anayepaswa kulaumiwa katika hili ni uongozi wa CCM wilayani Mwanga kwa kushindwa kuwachukulia hatua wahusika na kuongeza,  “Sijui wana maslahi gani na mambo haya? Hivi nchi hii viongozi waadilifu ndio wameisha?”

Shutuma zote hizi zinaelekezwa kwa katibu wa CCM  wilaya, Sidael Goroi; ama kwa kuegemea upande mmoja au kufumbia macho vitendo vya rushwa.

Baadhi ya wana-CCM waliokutwa makao makuu ya wilaya wiki iliyopita, waliliambia MwanaHALISI kuwa katibu wa wilaya amekalia malalamiko yaliyopelekwa kwake juu ya “kampeni chafu.”

Kwa mfano, CCM kata ya Butu imemsimamisha mwenyekiti wa kijiji cha Kigongoni kwa kitendo cha kuendesha vikao vya kampeni kabla ya muda wake.

“Baada ya kukiri mbele ya kamati ya siasa kuendesha vikao kinyume na taratibu, kamati hiyo imemsimamisha mwenyekiti, Ndugu Idd Shaban,” inasema sehemu ya muhtasari wa kamati ya siasa ya kata ya Butu uliotiwa saini na mwenyekiti Mussa Maleke na katibu Halima Mkwizu, tarehe 30 Mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa muhtasari, mwenyekiti huyo anadaiwa kuendesha vikao vitatu kwenye kata hiyo akishirikiana na mmoja wa wagombea ubunge kinyume cha taratibu.

Muhtasari unaonyesha kikao cha kwanza alikifanya Kigonigoni “A” Ijumaa ya 7 Mei 2010, saa 8:30 alasiri.

Kikao cha pili kilifanyika, Jumatatu, 10 Mei 2010 saa 2:30 usiku; na kikao cha tatu kilifanyika Ijumaa 28 Mei 2010, saa 2:30 usiku.

Alipong’ang’aniwa Goroi kutoa maelezo juu ya shutuma hizo  alisisitiza, “Hatuwezi kujibizana na magazeti.”

Bali katika hali ambayo haikutegemewa, Goroi alisema, “Katika wilaya yangu, ambayo ndio jimbo la uchaguzi la Mwanga, Ilani ya CCM imetekelezwa kwa asilimia 90, na waliosimamia utekelezaji huo ni mbunge na madiwani; sasa wanaosema hakuna kilichofanyika mimi sijui habari hizo wanazipata wapi,” ameeleza.

Kuna madai kwamba baadhi ya wanachama wa CCM wanaunda kambi ili kumuunga mkono mgombea ambaye atasaidia kuundwa kwa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Iwapo madai haya ni kweli, basi kuna uwezekano wa kuibua mgogoro katika KKKT, Dayosisi ya Pare ulioibuka miaka 11 iliyopita na kumalizika mwaka jana kwa wahusika kukubaliana kuvunja makundi na kurudi Dayosisi ya Pare.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa asasi zisizo za kiserikali mkoa Kilimanjaro, Peter Sauri anasema, “Kwangu naliona jambo hili la kuingiza udini katika siasa, ni gumu. Hawawezi kufanikiwa kwa kutumia gia ya kuunda Dayosisi."

0
No votes yet