Kwa sifa hizi hakuna waziri atakayesalimika


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
Mtazamo

“WAZIRI, naibu waziri, katibu mkuu na naibu katibu mkuu wasinyooshewe kidole kwa uvivu, uzembe, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, vitendo vya utovu wa uadilifu kama vile wizi, ulevi wa kupindukia, uzinzi, majigambo, ubabe na uonevu na dhuluma. Kuwa hivyo ni kupungukiwa sifa za msingi za uongozi.”

Pia,  “Mawaziri … kuhudhuria vikao vya Bunge ni jambo la lazima kama ilivyo kwa vikao vya baraza la mawaziri. Si jambo la hiari.  Ni lazima waziri ahudhuria vikao vya bunge bila ya kukosa labda awe na sababu kubwa inayoelezeka na kukubalika. Kutembelea jimbo lako la uchaguzi ni jambo la lazima lakini siyo sababu ya kukufanya ukose vikao vya Bunge au Baraza la Mawaziri.”

“Haifurahishi kuona waziri na katibu mkuu, au waziri na naibu waziri, naibu waziri na katibu mkuu au katibu mkuu na naibu katibu mkuu hawaelewani.  Wanasemana na hata wakipingana hadharani, yaani mbele za wafanyakazi.  Na baya zaidi pale wanapingana katika vyombo vya habari kuhusu maamuzi au utendaji wa wizara au serikali kwa ujumla.  Hayo si maadili mema katika taasisi yoyote.

“Uzoefu unaonesha kuwa jambo hili hutokea pale ambapo kunakuwa na kuingiliana katika majukumu au kwa kutozingatiwa kwa taratibu na maadili ya uongozi.  Lazima ieleweke kuwa tukishaamua jambo kwa pamoja Wizarani au katika Baraza la Mawaziri ni uamuzi wetu sote hata kama wewe ulikuwa na mawazo tofauti.  “Wote tunao wajibu wa kuunga mkono na kuutetea.”

Nimeamua kumnukuu Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya ufunguzi wa semina elekezi kwa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu inayoendelea mjini Dodoma kwa sasa.

Hii ni semina ya pili kwa mfululizo wa semina kama hizo ambazo Rais Kikwete alianza nazo mara tu alipoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Semina hiyo ilifanyika mwaka 2006.

Msingi wa rais Kikwete kuwaeleza mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu maneno hayo ni kuwataka wapime juu ya mwenendo wao wa utumishi wa umma, kama hawafai na wajiengue kwenye nafasi zao.

Hata hivyo, Rais hakuishia kuzungumzia mambo hayo tu, aligusia pia mambo ya uvivu, uzembe, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, vitendo vya utovu wa uadilifu kama vile wizi, ulevi wa kupindukia, uzinzi, majigambo, ubabe, uonevu na dhuluma. Kwa kigezo cha Rais Kikwete yeyote mwenye sifa hizo amekosa sifa za kuwa kiongozi, kwa maneno mengine “bora kutoka.”

Ukitazama kwa kina sifa hizi za Rais Kikwete, nachelea kusema kuwa yupo waziri au katibu mkuu atakaye salia madarakani kama kweli sifa hizo zitatazamwa kwa umakini na msisitizo unaostahili.

Ukitazama kwa makini zaidi tangu Kikwete aingie madarakani kufuatia uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, sasa ni miezi sita kamili, yaani nusu mwaka; kwa maelezo mengine muda huo ni sawa na asilimia 10 ya kipindi cha miezi 60 yaani miaka mitano, lakini kuna mawaziri ambao hadi sasa hawajui wanatakiwa wafanye nini ingawa kwa kiwango kikubwa wanajua fika kwamba wakati wa uchaguzi Rais Kikwete alimwaga ahadi rundo.

Tangu kuteuliwa kwa mawaziri wa sasa, ukiacha waziri kama Dk. John Magufuli anayeongoza wizara ya ujenzi na Profesa Anna TIbaijuka, anayeongoza wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, huwezi kusema kwa hakika kuna waziri mwingine amekwisha kuanza kazi.

Wengi wanaelekea kuwa katika fungate tu; wanasafiri huko na huko, wanaamini kuwa bado wana muda wa kufanya kazi, wanaamini kwamba wana nafasi ya kuendelea kupumzika lakini wakisahau kwamba hali ya uchumi kwa sasa ni ngumu mno, maisha yanazidi kuwa magumu kila uchao.

Mawaziri na wengi wa makatibu wakuu hawaonyeshi uchapa kazi wowote, hawaonekani wakijitutumua kwa lolote kukabili shida za kweli za wananchi, wameishiwa nguvu hata kabla ya kuanza kufanya kazi.

Tangu mawaziri wa sasa wateuliwe wamekumbwa na changamoto kuu zifuatazo, matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne ambayo kwa wastani asilimia 88 ya wanafunzi wote walifeli kwa maana ya kupata madaraja ya IV na sifuri; taifa limeshindwa kukabiliana na tatizo la mgawo wa umeme.

Tatizo hili limekuwa kama sehemu ya maisha ya Watanzania kila uchao mgawo wa umeme unatangazwa kwa visingizo vipya, kupungua kwa kina cha maji, kuharibika kwa mitambo ya gesi; lakini pia kuna mfumuko wa bei kuzidi kupaa huku bei ya mafuta ya petroli na dizeli ikipanda kila siku.

Si serikali kwa ujumla wake, au waziri mwenye dhamana na nishati, au waziri wa fedha amebuni mkakati wowote wa maana kupunguza makali ya maisha kwa wananchi; serikali imeendelea kung’ang’ana na kodi zile zile kana kwamba uchumi umeshamiri, lakini wakati huo huo mawaziri wa Rais Kikwete wakiwa hawana lolote jipya la maana wanalobuni katika kukabiliana na hali hii.

Tunakumbuka, mwaka 2006, mawaziri 27 kati ya hawa walipo leo walikuwa madarakani, walifanyiwa semina elekezi. Kwa takwimu ni sawa na kusema kati ya mawaziri kamili 30 na manaibu wao 21 waliopo leo, asilimia 53 walifanyiwa semina elekezi kwa maana hiyo uwajibikaji wao na uchapaka kazi haukustahili kusubiri maelekezo yoyote ili waanze kuchapa kazi.

Ndiyo maana kila mtu akitafakari kwa kina kauli ya Rais Kikwete juu ya utendaji wa mawaziri wake, inakuwa vigumu kujua ni nani hasa atasalimika katika msimamo wake mpya juu ya sifa za kumfanya waziri au katibu mkuu kupoteza sifa za kuwa kiongozi kwa sasa isipokuwa Magufuli na Tibaijuka.

Kwa hali ya mambo inavyokwenda nchini kwa sasa, hali ngumu ya maisha, wananchi kuzidi kukata tamaa kwa sababu ya kuendelea kutaabika na shida za kawaida mno ambazo mikakati ya ziada ingeliweza kabisa kuwapa nafuu ya maisha, hakuna ubishi kuwa mawaziri wengi wamekwisha kukosa sifa ya kuendelea kukalia viti vyao.

Nchini Kenya, kutokana na ukali wa maisha na hasa ukichangiwa na kupaa kwa bei ya petroli na dizeli, waliamua kupungua kwa asilimia 20 kodi za mafuta ili kuwapa wananchi uanfuu, haya kwa vyovyote ni maamuzia ya kijasiri na kimapinduzi.

Lakini kwetu, hakuna kiongozi anayewaza hatua za kuchukua juu ya adha zinazowakabili wananchi. Hali ni mbaya na hakuna uwezekano kwamba mambo yatapata ufumbuzi katika siku za hivi karibuni.

Ni katika kutafakari hali ya mambo, inakuwa si uchimvi kuhitimisha kwamba miongoni mwa mawaziri wa Kikwete kwa hakika ni vigumu kumpata anayeweza kutajwa kuwa ni mchapa kazi wa hakika labda wawili au watatu tu. Hii ndiyo changamoto ya kweli ya wakubwa hawa ambao wanaendelea na fungate miezi sita baada ya kuteuliwa.

0
No votes yet