Kwa tamasha hili, Simba waa waa...


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 04 August 2009

Printer-friendly versionSend to friend

KWA mwanamichezo yeyote mwenye upeo, wazo la Klabu ya Simba ya kuanzisha siku maalumu ya klabu hiyo ambayo wameibatiza jina la 'Simba Day', linastahili pongezi.

Ni ubunifu wa aina yake wenye dhamira ya kweli ya kuwakutanisha pamoja Wanasimba, bila kujali umri, jinsia wala rangi.

Tamasha la kwanza la Simba limepangwa kufanyika kwa siku moja kwenyeb Uwanja wa Uhuru, huku kukiwa na shughuli mbalimbali zitakazohitimishwa na pambano la kukata na shoka dhidi ya SC Villa ya Uganda .

Baadhi ya shughuli za siku hiyo zimetajwa kuwa ni kutembelea Hospitali ya taifa ya Muhimbili (MNH) ambako wachezaji na viongozi wanatarajiwa kutoa msaada wa chandarua.

Siku hiyo itakuwa pia maalumu kwa kutambulisha kikosi cha msimu ujao na kile cha vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.

Aidha, jezi zitakazotumiwa na klabu hiyo zitaonyeshwa rasmi kwa mashabiki wao.

Wachezaji wa zamani, viongozi na wadau wengine waliowahi kupitia Simba, nao watakumbukwa siku hiyo.

Kwa ujumla, ni shughuli pevu ambayo kama ikitumiwa vizuri, yaweza kuwa na manufaa ya miaka mingi, ingawa tukio litakuwa la siku moja tu kwa mwaka.

Ninaamini yaweza kuwa tamasha la neema kama viongozi wakienda mbali zaidi, kwa kuwaelimisha wapenzi na wanachama umuhimu wa kulipia kadi za uanachama, hatua ninayoamini yaweza kuwa ukombozi kwa klabu kutokana na kuwa na mamilioni ya mashabiki ndani na nje ya nchi.

Tuchukulie kwa mfano, ukifanyika uhamasishaji mzuri na wanachama wakaitikia, Simba yaweza kuingia mamilioni ya shilingi bila kulazimika kutoka jasho au kuuza uhuru kwa wafadhili uchwara.

Hata kama itakuwa na wanachama zaidi ya milioni moja, kama laki moja tu kati yao wakilipia ada zao, sh 1,000 kwa mwezi sawa na sh 12,000 kwa mwaka, Simba itakuwa na uhakika wa kutia kibindoni sh bilioni 1.2.

Kwa hakika hiki ni kiasi kikubwa mno kwa uwezo wa sasa wa klabu zetu zinazoukalia uchumi bila kujua au kwa makusudi ili kuhalalisha ulaji wa kikundi cha watu ndani ya Simba.

Tujiulize, kwa sh bilioni 1.2, Simba itahaha kusaka fedha za usajili kiasi Sh 200 milioni hadi 300 milioni? Itashindwa kulipa mishahara kwa wakati? Uongozi utalazimika kukopa hata 'chapati'? Hapana, bila shaka haya yatabaki kuwa historia.

Hapo tumezungumzia mapato kutokana na kadi za uanachama pekee, hatujagusa michezo kama bahati nasibu, uuzaji wa jezi na bidhaa nyingine zenye nembo ya klabu kama vishika funguo, miamvuli, fulana, kofia, mabegi, viatu, leso, khanga, na vitu vingine vingi.

Hivi, ingawa vinaonekana kuwa vidogo, vinasaidia mno kukuza uchumi wa klabu. Ni stahili hizi ndizo zinazowapaisha wenzetu kiuchumi katika nchi zilizopiga hatua kimaendeleo.

Ndiyo maana bila kutafuna maneno, nimelazimika kuumwagia sifa uongozi wa Simba kwa ubunifu wao, kwani ni mlango rahisi zaidi wa kuusaka utajiri.

Hata hivyo, nalazimika kutoa onyo kwamba, litakuwa kosa la mwaka kama viongozi hawa wa Simba watakuwa wametumiwa na kikundi cha watu, na matunda yote ya siku hiyo yakaishia mifukoni mwa wajanja wachache.

Hili linawezekana, kwani kumekuwa na historia ya watu kusutana ndani ya klabu hii kuwa wanatumika, hasa linapokuja suala lenye manufaa kama hili la fedha.

Ninaamini mtaungwa mkono na wadau, kwani kufana kwa siku hii ni kustawisha maendeleo ya klabu.

Nihitimishe kwa kurejea kuwapongeza viongozi wa Simba kwamba, ubunifu wao ni wa kuigwa. Hata Yanga, pamoja na kuywa na nguvu ya 'kuazima' kutoka kwa Manji, wana nafasi ya kuiga staili hii, lengo likiwa lile lile, kuwaunganisha wanachama wao na kufungua milango ya kiuchumi kuelekea katika kujitegemea.

Kila la kheri tamasha la Simba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: