Kwaheri wanasiasa, vyama uchwara


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

UFARANSA walikuwa na Maximillien Robespierre, Zanzibar walikuwa na John Okello na Cuba walikuwa na Fidel Castro. Misri hawakuwa na yeyote na bado Muhammad Hosni Mubarak akaachia ngazi.

Hii ndiyo sura ya mapinduzi ya kizazi cha sasa. Watu hawahitaji tena kiongozi wa kuwaongoza kufanya mapinduzi bali agenda ndiyo inayoleta mapinduzi.

Ni vigumu kuelewa kwa vipi wananchi wa Misri, na Tunisia kabla ya hapo, waliweza kuungana na kung’oa madarakani watawala wa kimabavu waliokuwapo bila ya kuwa na watu wa kuwaongoza.

Mubarak na Zine Abedine Ben Ali wa Tunisia hawakuwa viongozi wa kawaida. Wote waliwahi kuwa wanajeshi enzi ya ujana wao na walikuwa na nguvu kubwa katika jeshi na vyombo vingine vya usalama.

Kufanya mapinduzi yoyote dhidi ya viongozi wa aina hii, kulihitaji si uongozi wa kipekee tu, bali pia mbinu kali za kimkakati kukwepa neti za vyombo vya dola.

Hata hivyo, hakukuwapo na kiongozi wa mapinduzi na wala hakukuwapo na mbinu zozote kali za kimkakati. Kila kitu kilikuwa wazi kwenye mtandao wa kompyuta hususani facebook.

Kwamba labda leo kuanzia saa fulani wananchi wakusanyike pale Tahrir kwa ajili ya kufanya hili na likafanyika mipango ilifanywa kwa njia ya facebook na ujumbe mfupi wa simu za mkononi. Jeshi lilijua na usalama wa taifa ulijua. Hiki ndicho kizazi cha sasa.

Ndiyo maana mimi ni miongoni mwa watu ambao wanaamini kuwa nguvu za viongozi na vyama vya siasa zimepungua mno katika siku za karibuni. Na  huko tunakoelekea itapungua zaidi.

Hiki ni kizazi ambacho kinaathiriwa na nguvu ya makampuni makubwa na watu matajiri kuliko nguvu ya viongozi na vyama vya siasa.

Leo hii, Bill Gates, tajiri mmoja tu wa Marekani, anatumia fedha nyingi katika kupambana na malaria na ukimwi kuliko serikali nyingi za afrika ukizichanganya kwa pamoja.

Jaffer Sabodo wa Tanzania anataka kuchimba visima vya maji nchi nzima, huku serikali ikionekana kushindwa kufanya kazi hiyo. Makampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, Airtel, TIGO na mengine yanafanya shughuli mbalimbali za kijamii ambazo zamani ni serikali pekee iliyokuwa ikionekana kufanya.

Wale wanaoitwa Lions Club of Tanzania wanasaidia Watanzania wengi masikini wenye matatizo ya moyo kuliko serikali yetu inavyofanya.

Na hili haliishii kwa Tanzania pekee. Katika nchi nyingi za Afrika na nchi zinazoendelea, hali iko hivyo kwa ujumla. Kwamba sekta binafsi, watu binafsi na asasi zisizo za kiserikali zinaonekana kufanya makubwa kuliko serikali zenyewe.

Na ndiyo maana, watu hawana hofu tena na serikali wala taasisi zake. Watu hawana tena woga waliokuwa nao kwa viongozi wao katika siku za nyuma kwa sababu wanachokifanya hakionekani.

Hapa sina maana kwamba watu hawahitaji tena viongozi, la hasha. Watu wanahitaji viongozi na wanajua wanapomwona kiongozi wa kweli. Ukweli ni kuwa, wanajua pia wanapokuwa na kiongozi asiye wa ukweli.

Kilichotokea kwa Mubarak kitufundishe Watanzania na wanasiasa kwa ujumla kwamba wananchi wala hawana haja na wanasiasa uchwara wala vyama vyao visivyo na mwelekeo.

Chama pekee kikubwa na chenye nguvu kwa sasa ni shida za wananchi. Si Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF) wala Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Vyama vya siasa vitadumu iwapo tu vitafuata matakwa ya wananchi walio wengi. Si viongozi wake wala itikadi zake zilizowekwa miaka mingi iliyopita.

Katika kufuatilia historia ya vyama vya siasa duniani nimebaini kwamba vilianza takribani miaka 300 iliyopita. Kabla ya hapo hakukuwapo na vyama vya siasa na maisha yalikwenda kama kawaida.

Binadamu ni kiumbe aliyejaaliwa sana maarifa. Wakati wowote, mahali popote, hutafuta namna ya kumwezesha kuishi kuendana na hali halisi iliyopo.

Aliishi katika zama ambazo vyama vya siasa havikuwapo, anaishi sasa katika dunia ambayo vyama vya siasa vipo na ataendelea kuwapo katika mfumo wowote utakaokuwapo baadaye.

Dunia imebadilika sana kutokana na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia yaliyotokea katika kipindi cha miaka kumi tu iliyopita.

Na huko tuendako, dunia itakuwa ndogo sana kuliko ilivyo sasa kwa sababu ya maendeleo hayo ya kiteknolojia.

Maana ya hii ni kuwa watu wenyewe wataungana na kutengeneza ajenda zao na ilani za uchaguzi za vyama hazitakuwa na maana kubwa kwao. Ajenda hiyo ya watu ndiyo itakayokuwa na maana kuliko yale yanayoamuliwa na wachache kwenye Halmashauri na Kamati Kuu za vyama.

Na kama hayo ya wananchi walio wengi hayatafuatwa, watu wataungana tu na kutaka mabadiliko maana katika dunia hii, kitu pekee ambacho hakitabadilika ni mabadiliko yenyewe.

Ni muhimu kwa wanasiasa kuacha sasa kufikiria kuwa na magari ya kifahari kuliko wananchi wa kawaida kwa vile hawatadumu muda mrefu.

Ni muhimu kwa viongozi sasa kuacha kujiona wao ni kundi bora kuliko makundi mengine yoyote kwa sababu hilo halitafaa katika dunia ya sasa.

Kile kipindi cha viongozi kujiona wao wanafaa, kutembea kwenye ndege za kifahari wakati wananchi wakila majani, na kukosa dawa na pamba hospitalini, sasa kinaelekea ukingoni. Kiongozi sasa atakuwa mtu mmoja tu; ajenda.

Ni jambo la fahari kwangu kuandika waraka huu wiki hii. Naona kila dalili kwa heshima kurejea miongoni mwa wana jamii.

Nina neno moja kubwa kwa wanasiasa na vyama vya siasa visivyo na dira wala mwelekeo… Mwisho umewadia. Mwisho wa mchezo umefika !

0718 81 48 75
0
No votes yet