Kwanini sikuteuliwa ukuu wa wilaya


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

DUH, nimeumbuka mwenzenu. Katika orodha ya waandishi wa habari walioteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa wakuu wa wilaya, jina langu la Nyaronyo Mwita Kicheere halimo! Ajabu sana hii.

Hata mimi sikutarajia kwani katika waandishi sita bora nchini wanaofaa kuteuliwa wakuu wa wilaya mimi simo! Yaani siku ile baada ya kupata orodha ya wakuu wapya wa wilaya, niliisoma orodha ile hadi mwisho, nikarudia mara saba lakini sikuamini kama kweli Mheshimiwa sana kaniacha.

Yaani kuandika kote kule Kikwete kanitupa, kaniona si lolote si chochote – hakuniona nafaa! Au kwa sababu niliwahi kuandika mambo mengi kuhusu wakuu wa wilaya waliopo wanavyoboronga kazi yao ya ukuu wa wilaya?

Natamani ningekutana mahali fulani na Mheshimiwa Kikwete nimuulize nilimkosea nini hata kusababisha asinifikirie kuwa mkuu wa wilaya ya Tarime au Temeke, Kinondoni au Ilala ili nikapambane na wanaovamia maeneo ya wazi jijini.

Siku nikikutana na rais, wallahi wa billahi, nitamhoji maswali ambayo nafahamu hatakuwa na majibu yake.

Kwa mfano, hivi mwandishi mwenzangu Muhingo Rweyemamu kaandika nini ambacho mimi sijaandika lakini mwenzangu kateuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Handeni?

Bila utani nitamtaka rais aniambie, mbona makala au habari alizoandika Selemani Mzee Selemani huko Dodoma ni sawa kabisa na mimi lakini mwenzangu kateuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kwimba?

Nasema siwezi kuelewa, wanaomshauri rais walitumia vigezo gani ambavyo yaelekea sote hatuvielewi kwa maana kila ninayemuuliza anasema hajui. Sasa nani anajua kwa nini ameniacha mimi mkongwe akawateua Lucy Mayenga na Novatus Makunga? Loo Mayenga kawa mkuu wa wilaya Hai na Makunga kapelekwa Uyui.

Ahmed Kipozi tulianza kumsahau lakini leo kateuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Bagamoyo nyumbani kwao na Ridhwani Jakaya Mrisho Kikwete! Je, ni kwa vile ana sauti nzuri inayovutia masikio ya watawala au kuna vigezo vingine?

Naweza kuelewa sababu za Jacqueline Liana kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Magu. Huyu dada ni kada wa siku nyingi wa CCM, na ameanzia kazi za uandishi kwenye magazeti ya propaganda za CCM yaitwayo Uhuru, Mzalendo, na Burudani.

Na hata wakati fulani Liana alipohamia gazeti la Majira hakuweza kuvumilia kusikia chama chake cha CCM kikipondwa bila huruma kwenye kurasa za gazeti analolifanyia kazi ndiyo maana akahama haraka kurejea Uhuru ambako CCM hawasemwi wala kuhojiwa hata wakifisidi nchi.

Huyu Liana kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya inaeleweka ila bado najiuliza kwa nini akina Makunga, Mayenga, Muhingo, Mzee na Kipozi wamenipiku. Nitafanya kila njia nionane na waungwana hawa waniambie nini siri ya mafanikio yao. Nahisi kuwa watawala hawaamini kuwa mimi naweza kutekeleza sera za chama tawala.

Bwana kutawala ni kutawala na kuandika ni kuandika mimi ningetawala vizuri tu tofauti na ninavyoandika.  Hivi kweli nitashindwa kuitisha mkutano wa wananchi na kuwakoromea wapinzani watakaohudhuria na wale watakaobaki majumbani mwao na kuelezea umuhimu wa kuheshimu chama tawala, sera zake na mipango yake mwaka huu?

Hivi kweli nitashindwa kumwamuru kamanda wa polisi wa wilaya (OCD) kuvunja mkutano wa CHADEMA, TLP, CUF au NCCR! Yaani mimi kweli niwe mkuu wa wilaya halafu nishindwe kupiga marufuku mikutano ya wapinzani kwenye wilaya yangu ninayomwakilisha rais wangu?

Hivi kweli ninaweza kuwa mkuu wa wilaya ya Tarime au Magu halafu mtu kama Godbless Lema aje kuhubiri eti “people’s power” kwenye wilaya yangu? Au aje mtu kuzungumzia namna CCM walivyoshindwa kuvuana magamba? Mbona ningewamudu vizuri!

Basi tu waliopo jirani kabisa na kambi zenye mamlaka nchini hawajanielewa vizuri. Mimi ni shabiki mkubwa wa yule anayeteua siyo mawazo yangu na dhamira yangu. Ningemtumikia vema rais na siyo nchi yangu. Mimi ningekuwa “yesman” kwa kila ninaloamriwa na rais na chama tawala.

Lakini ili kuteuliwa waandishi wenzagu wamefanya nini? Wameandika nini au wametangaza nini cha mno? Hilo ndilo swali la kujibiwa ili nikipata majibu nifanye hivyo; kujiweka sawa wakati mwingine nafasi kama hizo zikipatikana, niteuliwe kuwa mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa kama Fatma Mwasa au Abihud Saidea.

Lakini kwa sababu ni rahisi kwa waandishi kupanda chati na kuwa wakuu wa wilaya napendekeza basi kuanzia leo waandishi, watangazaji na waandaaji vipindi waandike mambo yanayoifurahisha CCM na makada wake pamoja na viongozi wa serikali.

Nawaomba wandishi ili kuhakikisha nasi tunapata vyeo serikalini lazima tuhakikishe maandishi na matangazo yetu hayaikwazi serikali na pia hayaikwazi CCM na kufanya serikali na chama tawala vionekane vibaya mbele ya wananchi.

Pia nawashauri waandishi wenzangu mwaka 2015 wagombee kupitia CCM kwa sababu wote waliogombea kwa tiketi ya chama hicho wameteuliwa wakuu wa wilaya. Wewe gombea tu hata ukishindwa si neno kwa maana utateuliwa mkuu wa wilaya mpya ya Kigamboni.

Kabla ya uchaguzi wa 2015 zitaundwa wilaya mpya ikiwemo ya Kigamboni ili kupata nafasi ya kuteua wakuu wa wilaya kwa wale wana CCM watakaoshindwa kuteuliwa kugombea au watakaoshindwa uchaguzi wa ubunge.

Mwaka jana au mwaka juzi sikumbuki vizuri ziliundwa wilaya nyingi mpya bila watu kujua ni za nini. Kumbe hizi ziliundwa ili kuwapatia nafasi za ubosi wale wote hata waandishi wa habari waliogombea kwa tiketi ya CCM kama vile Makunga, Mayenga na  waliompigia kampeni Kikwete 2010 kama Rweyemamu.

Ili kupata ukuu wa wilaya waandishi wenzangu tuimbe wote CCM, wote tuandike CCM ilivyo nzuri, tusiandike Richmond, tusiandike twin towers, nyumba za serikali, wizi migodini, Kagoda na kadhalia. Mie nadhani ujanja huu ndio uliowapatia wenzetu ukuu wa wilaya.

0
No votes yet