Lembeli: Nitaacha ubunge niwe mwenyekiti


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

JAMES Lembeli, Mbunge wa Jimbo la Kahama mkoani Shinyanga (CCM) ametangaza nia ya kuwania kiti cha uenyekiti wa chama chake katika mkoa huo na ikiwa akishinda atafanya kazi ya kusafisha chama.

Lembeli, mmoja wa wanachama machachari wa Chama Cha Mapinduzi na mpambanaji dhidi ya ufisadi ndani na nje ya chama, anasema dhamira yake sasa ni kuwa mwenyekiti wa chama mkoa wa Shinyanga na ikibidi ataacha ubunge.

Akishinda kiti hicho, anasema hatapata kigugumizi cha kuendeleza mapambano dhidi ya virusi vinavyoharibu chama.

Kwa tangazo hilo, Lembeli atapambana moja kwa moja na Mwenyekiti wa muda mrefu mkoa huo, Hamis Mgeja.

Katika mahojiano yake na mwandishi wa gazeti hili hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Lembeli alisema kwa kadri anavyokitaka kiti hicho “…hata kama kutakuwa na mabadiliko ndani ya chama eti wabunge wasiwanie uongozi wa chama, nitaacha ubunge niwanie kiti hicho.”

Lengo lake kuwania nafasi hiyo ni kutafuta namna ya kukitumikia chama kivitendo akilenga hasa kukirejesha kwenye msingi wa kuanzishwa kwake, kuwa chama cha kutetea wakulima na wafanyakazi.

Mbunge huyo anaona chama kimechoka mkoani kiasi kwamba kinafagiliwa kando taratibu na vyama vya upinzani.

“Hebu tazama katika uchaguzi mwaka 2005 kulikuwa na mbunge mmoja tu wa upinzani. Kule Bariadi Mashariki kwa John Cheyo, lakini kufikia uchaguzi wa 2010 wapinzani wana viti tano kati ya 13,” anafafanua.

Majimbo yaliyochukuliwa na upinzani ni Bukombe (Profesa Kulikoyela Kahigi), Meatu (Meshack Opulukwa), Maswa Mashariki (Sylvester Kasulumbayi) na Maswa Magharibi (John Shibuda) wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati lile la Bariadi Mashariki yuko John Cheyo wa UDP.

Lembeli hasikitishwi tu na kuchoka kwa uongozi wa chama mkoa, bali pia uhuni aliofanyiwa na uongozi wa chama wilaya na mkoa alipojitosa kutetea kiti chake cha ubunge mwaka 2010.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, iliandaliwa mikakati kiufundi na mbunifu ni aliyekuwa Katibu Mkuu, Yussuf Makamba.

“Kilichonisaidia ni kelele za wanaharakati na ujasiri wangu wa kuhakikisha napata haki yangu,” anaeleza.

Siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu za kuwania ubunge katika ofisi za CCM Wilaya ya Kahama 30 Julai 2010, ilitolewa taarifa kwamba limeanzishwa jimbo jipya la Ushetu na kwamba aliyetoa taarifa hiyo ni Makamba.

Katibu wa CCM wilayani Kahama, Sospeter Nyigoti alitangaza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekubali kugawa jimbo la Kahama na hivyo kuanzisha jimbo jipya la Ushetu.

Nyigoti alinukuliwa akitangaza jimbo jipya kutokana na alichodai ni “maelekezo ya Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.”

Kutokana na tangazo hilo, Lembeli na wenzake wawili, Raphael Mlolwa na Elichard Mulyasi waliamua kugombea ubunge jimbo la Ushetu ambako ndiko wanakotoka.

Pamoja na furaha hiyo, Lembeli alipata hofu na aliyetangaza jimbo jipya. Uzoefu wake katika masuala ya utawala anajua anayetangaza jimbo jipya ni Tume ya Uchaguzi na si mtu mwingine yeyote.

Akahoji uongozi wa wilaya, “Nani aliyetoa tangazo la kuwepo jimbo jipya?” ambako alijibiwa kuwa ni katibu mkuu wa CCM (taifa).

“Ile kuhoji tu nikaonekana mkorofi. Tukaambiwa baadhi ya wagombea twende Ushetu. Nilitafakari sana, lakini mwishoni nikaitikia wito kwa sababu huko ndiko nilikozaliwa, wazee wangu wako huko,” anasema.

“Wananchi wengi wa Kahama walinikatalia kwenda, walisikitika na wakapanga kutopiga kura. Pamoja na kuwasilisha fomu zetu, ikaja kubainika kwamba Ushetu ni jimbo feki. Ulikuwa mkakati wa kuniondoa katika mbio kuwania za ubunge,” anasisitiza.

Anasema wakati tangazo hilo linatolewa alikuwako pia mke wa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja.

Mke huyo alikuwa katika ofisi za wilaya kwa ajili ya kumchukulia fomu mume wake kinyume cha utaratibu. Sheria inataka unapochukua fomu mbali ya kusaini pia unatakiwa kutia alama ya dole gumba.

“Tulipohoji tukaambiwa kwamba Mgeja ameombewa kibali maalumu cha kuchukuliwa fomu na mke wake,” anasema.

Kwa utaratibu huo, wapinzani wa Lembeli walikwisha kufanikiwa kumng’oa Kahama kwani kura za maoni zilianza kupigwa siku iliyofuata na kwa vile hakukuwa na Jimbo la Ushetu, ina maana huo ulikuwa mwisho wake.

Bahati ikawa kwa Lembeli. Tarehe 1 Agosti 2010, Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu, alitangaza kuwa hakuna jimbo lililotengwa na kwamba bado wanatambua jimbo la Kahama.

Baada ya taarifa hiyo, Lembeli na wenzake waliorudisha fomu kuwania ubunge Jimbo la Ushetu, Mlolwa na Mlyansi wakapambana kuhakikisha majina yao yanarudi Kahama.

“Na kweli yalirudi. Kelele zetu zilisaidia kurejeshwa Kahama. Na wakati huohuo nilitishia kumshitaki Makamba kwa jina kwa sababu ya taarifa za kutangaza jimbo feki huku tume ya uchaguzi ikikanusha.”

Vita ikaanza. Walipoingia kwenye mchakato wa kura za maoni, Mgeja akajitoa. Katika hilo Lembeli anasema, “alijua hawezi kunishinda hata siku moja...”

Lembeli anasema njama za kutaka kuondolewa kwake ni mikakati iliyoandaliwa na kuratibiwa kwa ustadi na mafisadi ambao, licha ya kuwa na fedha nyingi vilevile wana mbinu nyingi.

“Hawa mafisadi wana fedha nyingi sana maana utaona kabisa wapiganaji wawili Aloyce Kimaro (Vunjo) na Lucas Selelii wa (Nzega) walitupwa nje kiajabu. Mimi nilimshinda mpinzani wangu kwa tofauti ya kura saba tu za maoni,” anasema.

“Matokeo yalicheleweshwa siku nne. Kabla nilikuwa nimemzidi mpinzani wangu Mlolwa kwa zaidi ya kura 3,000 lakini baadaye ikaja kuonekana nimemzidi kura saba tu,” anaeleza.

Huo ndio uchafu anaouona Lembeli na atakaousafisha ikiwa atashinda kiti cha uenyekiti katika uchaguzi ujao mkoa wa Shinyanga.

Hivi sasa Lembeli anasema kuwa kwa namna wananchi wa Kahama walivyompigania hana budi kuchapa kazi kukidhi matarajio yao na kwamba yuko tayari kufa kwa kutetea haki zao.

Changamoto nyingine inayomkabili Lembeli ni uzushi kwamba yuko karibu na CHADEMA. Kwake yote anaona ni chuki binafsi na anasisitiza, “Nitaendelea kusema ukweli, kupinga wezi, ufisadi na matapeli wa kisiasa. Ni kwa njia hiyo tu taifa hili litaokolewa.”

Anafurahi kwamba hali jimboni kwake si mbaya sana akisema, “Sijisifu, ila hali ya jimbo inaridhisha tofauti na nilivyoingia ubunge mwaka 2005. Shule za sekondari hazikuwa zaidi ya sita, lakini sasa ziko 25.”

Anasema barabara zimeboreshwa kwani mwaka 2005 kulikuwa na barabara moja tu inayohudumiwa na Wakala wa Barabara (Tanroads), lakini sasa ziko barabara kuu nne zinazokwenda kwenye maeneo ya uzalishaji.

Barabara hizo ni Kahama – Butibu yenye urefu wa karibu kilomita 40; Kahama – Chambo yenye urefu wa kilometa 50; Kahama – Uyoga – Nsunga yenye urefu wa kilometa 100 na mtandao wa barabara vijijini wenye kilometa 300. Vituo vya afya vipo vitatu ambavyo ni Ukue, Ushetu na Buhungwa.

Anakiri jimbo hilo kuwa na shida kubwa ya maji safi na salama kwani mradi wa visima vilivyofadhiliwa na Benki ya Dunia vimekauka na “…jitihada zinafanyika kuhakikisha maji yanapatikana kwa kipindi hiki cha uongozi wangu.”

Kahama ina migodi miwili ya dhahadu Bulyanhulu na Buzwagi, lakini kwa mujibu wa mbunge hiyo migodi hiyo haisaidii Kahama kiuchumi wala kijamii kwa kuwa hawapati ajira.

“Leo ilitakiwa sura ya mji wa Kahama iwe dhahabu. Lakini, wananchi wa Kahama wanavuna vumbi tu. Migodi inazalisha dola 400,000 (sawa na bilioni sita) kwa mwaka inazidiwa hata na tumbaku inayoingiza Sh 15 bilioni,” anasema.

0
No votes yet