Lini hizi semina elekezi zitalipa?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

RAIS Jakaya Kikwete juzi Jumatatu alizindua semina elekezi iliyoshirikisha mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kupata maelekezo juu ya utendaji kazi serikalini.

Maudhui ya semina hiyo iliyofanyika mjini Dodoma, mbali na kukumbusha majukumu yao kama viongozi wakuu wa serikali, pia kujifunza utendaji wa vyombo vingine vya serikali.

Mada za semina hiyo ni umuhimu wa kuisemea serikali, kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya na uhalifu mwingine.

Aidha, amewataka wateule wake katika ngazi zote za uongozi kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa; wawe watu wa kupigiwa mfano, wasinyooshewe kidole kwa ulevi, uchelewaji kazini na kuwahi kuondoka, kwa uzembe, wizi, kutumia ofisi kujinufaisha, kwa uzinzi na ubabe.

Rais amefanya jambo muhimu sana kukumbusha watendaji kuzingatia uwajibikaji kwa wananchi kwani baadhi ya mawaziri walikuwa mzigo kipindi chake cha kwanza.

Mwaka 2006, Rais aliandaa semina elekezi kama hii mjini Arusha ili kuchochea ufanisi na kukuza uwajibikaji kazini. Lakini haikuchukua muda, baadhi yao walianza kulaumiwa kutowajibika ipasavyo.

Mathalani, baadhi ya mawaziri waliingia kwenye kashfa ya ufisadi kwa kuidhinisha zabuni ya kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond, Juni 23, 2006.

Hiyo ikamgharimu waziri mkuu na mawaziri wawili waliolazimika kujiuzulu na hatimaye kusababisha serikali kuvunjika.

Waziri mwingine alijiuzulu kwa shinikizo baada ya kuhusishwa na ufisadi katika ununuzi wa rada ya taifa. Alituhumiwa kupokea mlungula hadi kuchunguzwa na shirika la ukachero la Uingereza, ingawa aliita fedha alizokutwa nazo kama “vijisenti.”

Mkuu mmoja wa wilaya akajisikia raha kuwacharaza viboko walimu eti kwa vile shule zao zimepata matokeo mabaya katika mtihani wa darasa la saba.

Ripoti ya kila mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huonyesha wizi, ubadhirifu wa fedha za serikali katika idara za serikali na halmashauri. Ukiacha wakurugenzi waliosimamishwa katika wilaya ya Bagamoyo, wengine wanaendelea na kazi licha ya kuitia hasara serikali.

Ni dhahiri semina hizi hazijaleta matunda kwa mawaziri na watendaji wengi serikalini kwani matendo maovu ikiwemo uzembe na ufisadi yanaongezeka. Lini zitalipa?

Tunaamini sasa kilichobaki ni kwa rais mwenyewe pamoja na waziri mkuu kuonyesha mfano wa utendaji bora, na pale anapotokea kiongozi ameshindwa kuwajibika, ni kumtimua pasina kusita.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: