Lowassa afute mpauko huu wa mawazo


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Wazo Mbadala

TAKRIBAN vyombo vyote vya habari; magazeti, redio, televisheni, blogu na ‘twita’ zilikariri habari za mahojiano kati ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1) na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Gazeti moja liliandika katika utangulizi, “Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amesema hulka yake ya kuwa tayari kuchukua maamuzi magumu pasipo kuhofia matokeo mabaya ndiyo iliyomsukuma kulishughulikia kwa ujasiri tatizo la mgawo wa umeme na sakata la Richmond, ambalo hatimaye lilimlazimisha ajiuzulu nafasi hiyo miaka karibu mitatu iliyopita.”

Gazeti nyingine lilianza kwa kusema; “Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ameibuka na kusema hajutii kuileta Kampuni ya Richmond nchini wala uamuzi wake wa kujiuzulu kwa kuwa bado anaamini yuko sahihi.”

Mtu yeyote akisoma habari hizo kwa kina analazimika kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukubali, bila kusita ombi la Lowassa kujiuzulu.

Kwa nini? Kwa sababu Rais Kikwete alifikishwa mahali pagumu na swahiba wake katika maamuzi mengi yenye matokeo mabaya. Rais Kikwete alipima akaona njia pekee ya kuinusuru serikali yake iliyodaiwa ya kishikaji na kukiokoa Chama Cha Mapinduzi ni kumtosa Lowassa.

Hiyo ndiyo njia aliyotumia JK kumweleza swahiba wake huyo kwamba “mchezo aliofanya ni mauti kwa taifa”. Hebu tujikumbushe.

Mara baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu, Lowassa aliwaita maofisa elimu wa mikoa, wilaya na halmashauri kama afanyavyo mkuu wa shule anapowaita wanafunzi na kuwasomea sheria. Akawapa malengo ya kujenga shule.

Ni katika kipindi hicho tulichoshuhudia wananchi wakikamatwa na kutozwa faini, kuwekwa ndani na wengine kulazimishwa kuuza mifugo wapate pesa za kuchangia ujenzi wa shule. Adha hii iliyofanana na enzi wa ‘kodi ya kichwa’ ilidumaza maendeleo kwani wengi walitoroka au walijificha kuwakwepa mgambo.

Lowassa akabuni mpango wa kupata walimu chap chap (waliitwa Vodafasta). Akabuni walimu wa leseni (siyo cheti wala diploma) wa kufundisha sekondari, halafu akapunguza muda wa kozi za diploma na cheti kutoka miaka miwili hadi mmoja.

Maamuzi hayo yalifanywa kwa nguvu kwa sababu ya hulka ya mtoaji kwamba hakuwa anajali matokeo mabaya.

Kuthibitisha kwamba Baraza la Mawaziri halikuwa linaridhishwa na maamuzi yake, alipokaa kando, utaratibu wa zamani ukarudi hata shule zinajengwa kwa staha.

Suala la umeme. Baada ya kufanikisha ‘mradi’ tata wa Richmond, Lowassa alisafiri hadi Thailand kukutana na wataalamu wa kutengeneza mvua.

Ilidaiwa kwamba mradi wa kutengeneza ‘mawingu’ ya wakati mmoja katika eneo lililoainishwa, kama vile Bwawa la Mtera, ungegharimu dola milioni 2 sawa na takriban shilingi bilioni mbili kwa siku.

Uamuzi wa kuwaleta ulifikiwa licha ya taarifa kwamba kuna wakati wingu hilo lingeweza kutengenezwa kwa gharama hiyo lakini lisitoe mvua iliyokusudiwa.

Ndiyo kusema, mvua hizo hazikuwa za uhakika wala jibu la matatizo ya ukame.

Tujiulize, nchi ngapi duniani zinatumia mtindo wa Mvua za Thailand? Kwa nini Misri isitumie mvua hizo badala yake inalazimika kutumia sheria kuwa na haki ya maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Mto Nile?

Je, aliyetoa uamuzi wa kufuata mvua za Thailand alikuwa anajua matokeo mabaya ya uamuzi huo? Sasa kwa vile amesema anachukua maamuzi mazito bila kujali matokeo mabaya, anaisadia vipi serikali kiongozi kama huyu?

Kwa kumpoza tu, Kikwete alisema tukio hilo ni ajali ya kisiasa. Sawa, lakini ni ajali ya bahati mbaya au ya kujitakia? Hapa alijiandalia ajali kama alivyowaandalia ajali wanaotumia njia tatu kutoka Mwenge hadi Morocco katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Mwisho amesema akiteuliwa katika nafasi hiyo leo atafanya yale yale. Sawa, ni kwa vile hajali matokeo mabaya.

Lowassa ajue madhara ya kutojali matokeo mabaya ya maamuzi yake ndiyo yamemfikisha hapo. Namuomba ajifunze kanuni isemayo kwamba mtu akifikiri vibaya, atazungumza vibaya; akizungumza vibaya, atatenda vibaya kwa hiyo haya yanayompata ni kutokana na kufikiri vibaya. Ushauri, Lowassa afute mpauko huu wa mawazo ili afikiri vizuri, azungumze vizuri na awajibike vizuri.

0
0
Your rating: None
Soma zaidi kuhusu: