Lowassa apania urais


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version
Akutana na washirika wake
Aunda kamati kutimiza lengo
MBUNGE wa Monduli, Edward  Lowassa

MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa ameshauriwa kukaa kimya kuhusu siasa zinazoendelea hivi sasa nchini ili akija kuibuka awe na kishindo kipya.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa akifuata ushauri huo, wananchi watasahau haraka yale yaliyotokea na hatimaye Lowassa ataibukia kwenye kinyang’nyiro cha urais.

Taarifa za kuaminika zinasema aliyempa Lowassa ushauri huo ni askari mstaafu wa cheo cha juu (jina linahifadhiwa kwa sasa), mwenye ushauri mkubwa katika siasa za nchi hivi sasa.

Askari huyo ni mwana-kamati ya wafuasi wa Lowassa ambayo imeundwa rasmi kuratibu mipango na mbinu za kuhakikisha Lowassa anarejea katika ulingo mkuu wa siasa.

Miongoni mwa kazi za kamati hii ni kuhakikisha wabunge wote, ambao ni wapinzani wakuu wa Lowassa, hawarejei tena bungeni katika uchaguzi ujao.

Mtoa habari ameliambia gazeti hili, “Mbinu hii itasaidia katika kampeni za uchaguzi za 2010, iwapo hali itaonekana muwafaka na Lowassa kuamua kugombea urais mapema.”

Mkakati huu utasaidia kupunguza nguvu za wabunge wapinzani wakuu wa Lowassa katika majimbo yao, ili washindwe kupata muda wa kumsakama.

Hatua hii pia inalenga kupunguza ushawishi wa wabunge hao katika vikao vya maamuzi hasa Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na Mkutano Mkuu, ameeleza kiongozi mmoja wa kambi ya Lowassa.

Bali iwapo hali haitaruhusu Lowassa kugombea mwaka 2010, kwa kuona hajajisafisha kikweli na bado ananing’inizwa na wapinzani wake, basi atajitosa katika kinyang’anyiro cha mwaka 2015 ambako washindani wake wengi ndani ya bunge wanasemekana watakuwa wamepungua.

Tayari Lowassa ameanza kuchukua hatua mbalimbali ili kujiweka sawa na kinyang’anyiro kijacho cha urais, ikiwa ni pamoja na kukutana na watu mashuhuri.

Miezi miwili iliyopita, Lowassa alimwalika Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo kuzindua kitabu kilichoelezwa kuwa kimetungwa na mkewe, Regina Lowassa.

Viongozi wengine wa kidini wa ngazi ya juu waliokuwepo ni pamoja na Askofu Alex Malasusa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Mwinjilisti Christopher Mwakasege.

Lakini wiki iliyopita Lowassa alionekana kwenye uzinduzi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria ambao utanufaisha vijiji 54  kwa njia ya umwagiliaji mkoani Mwanza. Mradi huo ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Uzinduzi wa mradi huu ulileta pamoja viongozi wakuu wa serikali ya sasa na iliyopita, akiwemo rais mstaafu Benjamin Mkapa. Mradi ulianza wakati wa utawala wa Mkapa na Lowassa akiwa waziri wa maji.

Haikufahamika iwapo Lowassa alipata fursa ya kuongea faragha na Rais Kikwete na Benjamin Mkapa au mmojammoja, lakini taarifa zimeeleza kuwa tukio hilo lilimrejeshea Lowassa mataumaini kwa vile alialikwa kushuhudia mradi mkubwa aliosimamia.

Taarifa zinasema tayari Kamati ya Lowassa imeanza vikao na Lowassa mwenyewe amekutana na baadhi ya washirika wake ndani ya Chama Cha Mapinduzi kutoka mikoa ya  Shinyanga, Mwanza na Mara na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa katika mikoa hiyo.

Mtoa habari ameeleza kuwa kikao cha Lowassa na viongozi na wafanyabiashara (majina tunayo) kilifanyika katika Hoteli ya Tilapia, barabara ya Nyerere mjini Mwanza.

Lowassa alikuwa mwenyekiti wa kamati ya kampeni iliyomwingiza madarakani Rais Kikwete.

MwanaHALISI liliwahi kuandika kuwapo kwa mbinu za kumwengua Kikwete kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2010, jambo ambalo lilielezwa pia na baadhi ya wenyeviti wastaafu wa CCM, wakiwemo Hemed Mkali wa Dar es Salaam na Pascal Ndejembi wa Dodoma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: