Lowassa hakuonewa, alichelewa kujiuzulu

EDWARD Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu, hakuonewa na mtu yeyote kabla ya kujiuzulu kama ambavyo amekuwa akidai. Hakika alitakiwa kujiuzulu hata kabla ya Kamati Teule kuundwa.
Madai kuwa alionewa yanatokana na mtazamo finyu, wenye ushahidi dhaifu, na kwa kipimo chochote unaojaribu kutengeneza kitu ambacho hakipo.
Ni makusudio yangu kuonesha kuwa Lowassa alistahili kujiuzulu mapema zaidi na hata pale alipochelewa alitakiwa kukubali adhabu aliyojipa yeye mwenyewe kutokana na kutokuwajibika kwake, uzembe wa ofisi yake, na kutokuonesha usimamizi unaomstahili waziri mkuu katika jambo nyeti kama la nishati.
Kwanza, Lowassa alifanya makosa makubwa kisheria kuingilia mchakato wa tenda; alitenda hayo kwa nia ya kutaka Richmond ipendelewe kupata tenda ya kuzalisha umeme huku akijua kwamba kampuni hiyo, haikuwa na uwezo wa sifa ya kufanya kazi iliyoomba.
Pili, Lowassa alistahili kujiuzulu mapema kwa sababu alikiuka sheria, alijipa madaraka asiyokuwa nayo, na alishindwa kutumia nafasi aliyopewa kujitetea kujenga hoja kwanini ripoti ya Kamati Teule haikumtendea haki.
Ni lazima ifahamike kwanza kwamba tatizo la ukosefu wa nishati Tanzania siyo geni na hakuna mtu mwenye akili timamu ambaye anaweza kudai kuwa hatukujua kuwa tutakuwa na tatizo hilo kama vile lilivyotokea tena mwaka huu na kama itakavyotokea mwakani.
Zaidi ya yote ni muhimu kutambua kuwa tatizo la nishati la Tanzania halitokani na upungufu wa maji kwenye mabwawa yetu. Sababu hii imekuwa ikitajwa mara nyingi na watawala na wananchi wa kawaida wamekuwa wakikubali. Hiki ni kisingizio dhaifu cha tatizo kinachotumiwa na watawala.
Tatizo letu ni uongozi usio na maono; dhaifu kuamua, legelege katika kutenda na usiothubutu kujaribu mambo makubwa na kuishia kujaribu vitu vidogo kwa sababu vikubwa vinatisha. Tanzania haina sababu hata moja ya kuwa na tatizo la nishati ya umeme.
Tukielewa hilo tutaona kuwa mwitikio wa waziri mkuu wakati wa upungufu wa nishati hiyo mwaka 2006 ulikuwa ni wa jazba, hamaki, na uliojaribu kutengeneza kimbunga ndani ya kikombe cha chai au maporomoko ya maji kwenye kijiko.
Idara zote na taasisi zote za serikali zinaongozwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2004. Sheria hii imeweka utaratibu wa jinsi gani wizara, idara, wakala au taasisi ya serikali inavyoweza kununua vitu mbalimbali au kuuza vitu hivyo.
Hii ni sheria inayohusu vyombo vya umma na hata vya binafsi ambavyo vinahusisha fedha za umma. Hivyo hii ndiyo sheria iliyotakiwa kufuatwa mwaka 2006.
Lakini sheria hii haikufuatwa ilivyotakiwa. Ni kutokana na kutokufuatwa huko ndiko kulisababisha kampuni ya Richmond kupewa tenda na kushindwa kupatikana kwa majenereta katika muda uliotakiwa. Kama sheria hii ingefuatwa Lowassa asingekuwa katika masaibu yaliyomkuta.
Kipengele (a) cha sheria ya manunuzi kinasema wazi kuwa hakuna tenda yoyote itakayotolewa kwa mtu au taasisi yoyote isipokuwa kama imeidhinishwa na bodi ya tenda husika. Katika suala hili chombo kilichotakiwa kusimamia mchakato wa upatikani wa tenda ni Bodi ya Tenda ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Ni chombo hicho peke yake, kuanzia mwanzo hadi mwisho, kilichotakiwa kutangaza, kuchuja, kupima na hatimaye kuingia mkataba na kampuni iliyotimiza vigezo vya tenda hiyo kuleta majenereta ya umeme. Hii ina maana siyo wizara ya nishati na madini, wala ofisi ya Lowassa au ikulu waliokuwa na nguvu ya kuingilia mchakato wa tenda.
Ibara ya 38 ya sheria ya PPRA inataja vyombo vyote vinavyohusika na masuala ya tenda na kwamba vyombo hivyo vitafanya kazi yake kwa “uhuru.” Lakini tumeona jinsi Lowassa alivyoingilia mchakato; alivyonyang’anya kazi Bodi ya Tenda ya Tanesco na alivyoshinikiza Tanesco kusaini mkataba na Richmond.
Kisingizio cha Lowassa na wapambe wake ni kuwa kulikuwa na dharura. Kwamba “dharura” ile ndiyo iliyompa nguvu waziri mkuu kuingilia utaratibu wa tenda. Kwamba kutokana na hali hiyo sheria ya PPRA ilisimamishwa kwa muda na hivyo kumhukumu Lowassa ni kumuonea. Huu ni utetezi dhaifu.
Hadi sasa, hakuna mahali popote tunapoelezwa kwamba serikali ilisitisha sheria ya PPRA. Wala Lowassa mwenyewe hajawahi kusema hivyo na bila shaka hawezi kusema hayo kwa sababu anajua kuwa sheria hiyo haijawahi kusitishwa wala haijafutwa na hakuna afisa yoyote wa serikali akiwemo rais anayeweza kuisimamisha kiholela au kuifuta kwa kisingizio cha “dharura.”
Kwa msingi huo, Lowassa alivunja sheria na hiyo peke yake inatosha kujiuzulu.
Utetezi kwamba Lowassa alikuwa na nia njema wakati wa kushughulikia suala hili wala hauna mashiko. Nani aliyewahi kuingia moyoni mwa Lowassa na kujua nia yake njema?
Hata kama alikuwa na nia njema, lakini alipokula kiapo chake cha kuwa waziri mkuu hakula kiapo cha “kulinda, kutetea na kuhifadhi nia njema.” Waziri mkuu wetu, kama walivyo watumishi wengine wakuu, wanakula kiapo cha kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri na kiapo cha utii kwa rais aliyemteua na vilevile kile cha usiri kama mshiriki wa Baraza la Mawaziri. Hivyo, nia yake njema haikumzuia kuwajibika au kujiwajibisha yeye mwenyewe.
Lakini waziri mkuu hana uwezo wa kutangaza dharura inayoweza kusababisha baadhi ya sheria kutokutumika na maagizo yake yakatosha kuwa sheria. Kwa sheria zetu, ni Rais peke yake mwenye madaraka ya kutangaza dharura au hali ya hatari.
Ninaamini janga la umeme la 2006 na hata la mwaka huu yanaweza kutosha kabisa kutangaza hali ya dharura, lakini ni rais wa Jamhuri ndiye mtu pekee ambaye aweza kutangaza hali hiyo na ndiye pekee anayeweza kutoa mamlaka yake hayo kwa mtu mwingine kwa mujibu wa sheria.
Na ikimbidi kufanya hivyo basi hilo linatangazwa kwenye gazeti la Serikali na siyo kwa simu au kwa mdomo tu. Ni lazima iwe kwa maandishi.
Hadi sasa Lowassa hajasema mahali popote kuwa alipewa madaraka hayo na Rais; jambo hilo la kuwapo kwa dharula lilitangazwa katika gazeti la serikali. Sasa kama Lowassa hakupewa madaraka hayo yeye aliyapata wapi?
Hilo ndilo swali la karne. Ninachoona nikuwa “dharura” tunayoisema ni dharura kwa maana ya kawaida ya jambo lenye kuhitaji uangalizi wa haraka na siyo kwa maana ya kisheria.
Hata akitaka kujitetea kwamba alitumia sheria ya Kusimamia Majanga ambayo iko chini ya wizara yake, sheria hiyo nayo haimpi waziri mkuu uwezo wa kuingilia tenda ya chombo chochote. Sheria hiyo imeweka utaratibu wa kufuata wa kushughulikia majanga.
Pendekezo la Kamati Teule kuhusu waziri mkuu lilisema, “Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Mhe. Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za serikali na uongozi wa nchi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge. Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge.”
Kamati Teule haikuitisha kujiuzulu kwa Lowassa. Ilimpa nafasi ya “kupima uzito” wa matokeo ya uchunguzi na kwa Bunge “kuangalia” kama matokeo ya uchunguzi hayajaathiri hadhi na uzito wake bungeni.”
Lowassa angeweza kufanya mambo kadhaa. Angeweza kutoa hoja asubuhi kuwa “baada ya kupima uzito” wa ripoti ya Kamati Teule anamuomba Spika mjadala uahirishwe japo kwa siku moja ili aweze kupitia vielelezo mbalimbali na kuandaa majibu yake. Hakufanya hivyo.
Kama tayari alikuwa anajua msimamo wake angeweza asubuhi ile kuanza kupangua hoja moja baada ya nyingine, kuanzia barua zinazodaiwa kutoka kwake kwenda maafisa mbalimbali wa wizara na za kutoka kwao kwenda kwake. Angeonyesha kuwa hakuvunja sheria yoyote na angeweza kutetea madaraka yake ya kuingilia utaratibu wa tenda kuwa aliyapata wapi.
Lowassa angeweza kuomba Bunge liahirishe mjadala ili aweze kufanya mazungumzo na Rais (aliyekuwa tayari Dodoma wakati ule) ili aweze kumueleza upande wake na kupata msimamo wake na kumtaka asimame upande wake atakapojitetea bungeni. Hakutumia nafasi hiyo kufanya hivyo.
Kwa msingi huo, hoja ya kuwa Lowassa alionewa kwa kuwa hakusikilizwa haina msingi isipokuwa kwa watu ambao hawataki kukumbuka kilichotokea siku ile.
Lowassa angeweza kujitetea vizuri kabisa siku ile, angeweza kupangua kila hoja iliyotajwa dhidi yake, angeweza kuhutubia kutwa nzima bungeni na kuonesha mapungufu kiasi cha kusababisha Bunge kupiga kura ya kukataa ripoti ya Kamati Teule. Lakini hilo hakulifanya. Aliamua kuzira kujitetea.
Katika hili Lowassa wala hana wa kumtwisha mzigo. Hawezi kusema kwamba alikuwa anawasiliana kila hatua na rais na hivyo alifanya hayo kwa baraka zake. Ni kweli kuna mawasiliano kati ya waziri mkuu, wizara na ikulu.
Hatujaona mawasiliano ya Lowassa kwa rais kwamba anataka kufuta mkataba na mawasiliano yakaonyesha kuwa Rais Kikwete binafsi au ikulu imemzuia kufanya hivyo.
Lakini kwa kukubali kusimamia kitu ambacho hakukiamini ili tu mambo yaendee, ni sifa mbaya ya kiongozi na ninaamini kabisa kuwa ingetosha kuwa sababu nyingine ya kujiuzulu.
Tanzania inahitaji viongozi ambao wako tayari kuwajibika kwa makosa yao na kuwajibika vilevile pale inapobidi kwa makosa ya wengine ili kulinda usafi wao. Lowassa hakufanya lolote kati ya hayo mawili. Alichosubiri ndicho alichopata.