Lowassa, Rostam, Chenge bado


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Edward Lowassa

PAMOJA na tambo za viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka kuwafukuza ndani ya chama hicho watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini, Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge, bado kimeshindwa kuwapa barua za kuwafukuza.

Kufumuka kwa taarifa hizo kumekuja wiki moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaambia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake kuwa “chama hiki hakiwezi kubaki na wezi.”

Akiongea kwa kujiamini, Kikwete alikiambia kikao cha Kamati Kuu (CC) na baadaye NEC, kwamba zama za CCM kulea wale aliowaita mafisadi zimekwisha.

Taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na viongozi hao zinasema, hadi juzi Jumatatu, ofisi ya katibu mkuu wa CCM, chini ya Wilson Mukama ilikuwa haijatoa barua kwa yeyote kati ya Lowassa, Rostam na Chenge.

Habari zinasema kigugumizi cha CCM kimetokana na kile kinachoitwa, “hofu ya kuumbuana.”

“Yule Lowassa anafahamu mengi ya Kikwete. Siku akiongea, ikulu inaweza kuwaka moto. Katika mazingira hayo, hakuna uwezekano wowote wa Kikwete kuagiza Mukama kuandika barua hizo,” ameeleza kigogo mmoja wa ngazi ya juu serikalini.

Anasema kwa ufahamu wake, Lowassa tayari amejiandaa kukabiliana na yeyote ambaye anataka kumtoa ndani ya chama hicho na kuua ndoto yake.

“Nakuambia, Lowassa akizungumza, Kikwete hatakuwa salama. Kuanzia uchaguzi ndani ya chama chake, hadi mbio za urais mwaka 2005, vyote hivyo vilisimamiwa na Lowassa. Sasa akiamua kufungua mdomo, mengi yanaweza kuibuka na kumbomoa hadi Kikwete mwenyewe,” ameeleza mtoa taarifa wa gazeti hili aliyepo karibu na Lowassa.

Anasema, “Hata ujio wa Richmond na jinsi ilivyopewa mkataba, Kikwete hawezi kutoka.”

MwanaHALISI lilipowasiliana na Nape Nnauye, katibu mwenezi wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, kujua kilichosababisha chama hicho kushindwa kuwapa barua viongozi hao, haraka alijibu, “Kwa sasa suala hilo la kuandikiwa na kupewa barua zao lipo kwenye sekretarieti. Sasa kama wamewapa hizo barua au hawajawapa bado sina taarifa; lakini ninachojua ni kwamba ni lazima wapewe barua hizo.”

Alisema kwa mujibu wa taratibu za chama chao, maamuzi yakishafanyika ndani ya vikao, sharti wahusika wafahamishwe, tena kwa barua.

“Nakuambia, lazima hizo barua tutawapa. Hakuna njia ya kuzuia hilo kufanyika,” ameeleza Nnauye.

Gazeti limeshindwa kumpata Lowassa kueleza atachukua hatua gani mara atakapokabidhiwa barua ya kumtaka kujiuzulu ndani ya chama chake, lakini kiongozi mmoja aliyekaribu naye amesema, “Anachosubiri Lowassa ni hiyo barua.”

“Haraka ya nini? Subirini barua itoke kwanza. Hapo ndipo Lowassa atakapoeleza hatua itakayofuata,” ameeleza kiongozi huyo.

Naye Rostam Aziz alipoulizwa iwapo amepata barua, haraka alisema, “Naomba mniache. Niko nje ya nchi nauguza mke wangu.”

Juhudi za kumpata Chenge zilikwama kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: