Lucas Selelii: Sijawahi kutumia udini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 31 March 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Mbunge  wa Nzenga, Lucas Lumambo Selelii

“MIMI sijawahi kutumia udini kutafuta uongozi. Nimekuwa mbunge kwa vipindi vitatu sasa mfululizo. Katika muda wote huo, hakuna hata mara moja nilipotumia udini kushinda ubunge.

“Siku zote siri ya ushindi wangu imetokana na kuungwa mkono na watu wa madhehebu yote. Hivyo, hoja kwamba natumia udini kama silaha ya kisiasa, ni upuuzi mtupu.”

Ni kauli ya mbunge wa Nzenga, Lucas Lumambo Selelii (49) katika mahojiano na MwanaHALISI wiki hii, kujibu kile alichoita, “mikakati ya maadui zake wa kisiasa.”

Alikuwa akizungumzia taarifa iliyochapishwa gazetini ikidai kuwa Selelii anatumia udini na ukabila kama silaha ya kupambana na maadui wake kisiasa.

Gazeti lilidai kuwa Selelii, akiwa jimboni kwake Nzega, aliwataka wananchi kutokabidhi jimbo hilo kwa mgombea Muislamu wakati ukifika kwa hoja kwamba atashinikiza serikali kuleta nchini Mahakama ya Kadhi.

Aidha, gazeti lilisema Selelii anataka wananchi kutochagua mgombea ambaye hatoki katika kabila la wakazi wa Nzega na kwamba alitoa kauli hiyo katika kilele cha siku ya wanawake duniani.

“Kwanza, mimi mwenyewe baadhi ya ndugu zangu ni waislamu. Kwa mfano, bibi yangu mzaa wa mama, Halima Pambe ni muislamu. Tena bado yuko hai na ninaishi naye hapa kwangu.

Mjomba wa baba yangu, Athumani Kulwa ni muislamu. Baba mkwe wangu, Juma Mangu ambaye sasa ni marehemu, alikuwa muislamu. Sasa iweje mimi Selelii niwapuuze hawa ndugu zangu,” anahoji Selelii kwa uchungu.

Anasema, “Wapo ndugu zangu wengi hawamo katikka madhehebu makubwa lakini siwezi hata siku mmoja kufanya ujinga wa aina hiyo. Kitendo hicho nimekilaani na kusema ni uhuni na uzushi uliolenga kubomoa misingi ya nchi na kuchafua sifa yangu.”

“Mimi niko Nzega, nina vikao vingi. Katika vyote hivyo, sijawahi kuitisha mikutano ya peke yangu. Ninaitisha mikutano inayohusu chama changu. Katika vikao vyote hivyo, mimi sijawahi kutamka meneno hayo,” anasema.

Sasa tuhuma hizi zinatoka wapi? Anajibu, “Sijui. Lakini bila shaka zinasambazwa na kuenezwa na wale wasionitakia mema. Zinatolewa na wale walioshindwa siasa za ustaarabu ambao wameamua kutumia vyombo vya habari kuchafua wenzao.”

Anasema, “mtu kama msafi ni msafi tu. Huwezi kuchafuliwa na watu wenye fedha. Wananchi wanajua mambo tunayoyafanya” na kurejea kauli zinazotolewa na wengine kuwa makundi yanayoitafuna CCM yakiachwa, yanaweza kudhoofisha chama hicho si muda mrefu ujao.

Kutokana na hali hiyo, anatoa wito kwa chama chake kukemea wale anaoita, “wanaotumia silaha chafu dhidi ya watu wasafi.”  Anatoa mfano wake mwenyewe, kwamba anasakamwa kwa msimamo wake.

Anasema anachokumbuka ni kwamba alialikwa katika kilele cha siku ya wanawake duniani kuwa mhamasishaji katika harambee ya kuchangia Mfuko wa Wanawake Wakristo.

Katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Afisa Kilimo na Mifugo wa wilaya, Edith Munuo aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Nzega, Selelii anasema kwamba “hakuna hata sentensi moja alimogusia kuomba kuchaguliwa, uislam wala mahakama ya kadhi.”

Anasema sherehe hizo zilihudhuriwa na madiwani wawili wa viti maalum, Asha Samsambwe na Mwere Igogo ambao mmoja ni mkristo na mwingine muislamu.

Selelii ni mjumbe wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kitapeli kati ya serikali na kampuni ya Richmond; anaamini kuwa chanzo cha chokochoko hizi za sasa ni msimamo wake katika suala hilo.

Hata hivyo, kuna minong’ono kwamba tuhuma dhidi ya Selelii ni sehemu ya siasa za uchaguzi wa mwaka 2010 na tayari kupakaziana kumekuwa fasheni.

Ingawa Selelii hakutaja jina la anayedaiwa kumtuhumu udini, lakini ishara zote zinaelekezwa kwa wanaotajwa kuwa na uwezekano wa kugombea jimbo la Nzega.

Mmoja wa watu hao ni Hussein Bashe, ambaye kwa sasa ni Meneja Usambazaji katika kampuni ya Rostam Aziz (Habari Corporation Limited) inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, The African, Dimba na Bingwa.

Seleli anajigamba kuwa wakati wa ubunge wake, wilaya ya Nzega imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya elimu ya sekondari ambapo katika kata 37 wamefanikiwa kujenga shule zaidi ya 35, zahanati 18 na kituo cha afya kila tarafa. Mkakati sasa ni kupeleka huduma za vituo vya afya kila kata.

Hata hivyo, Selelii anasema huduma ya maji bado haijafika sehemu kubwa ya vijijini pamoja na kwamba wamepata ufadhili kutoka Benki ya Dunia. “Mpaka sasa, kupitia ufadhili huo, chini ya mradi wa Maji na Uhifadhi wa Mazingira (RWSSP), asilimia 40 tu ya wananchi ndio wanapata huduma ya maji vijijini.

Alisema kwa upande wa mijini, ni asilimia 70 ya wakazi wanaopata maji safi na salama.

Kuhusu uhaba wa walimu, Selelii anasema Nzega, kama zilivyo sehemu nyingine za nchi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu. Mpaka sasa wilaya ya Nzega inakabiliwa na uhaba wa walimu 280.

Uhaba wa walimu unaambatana na uhaba wa nyumba za kuishi za walimu. Yote haya anasema yanatokana na kuongezeka kwa shule za msingi.

Lakini anasema tofauti na mwaka 1995 wakati anachaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge, leo hii Nzega imepiga hatua kubwa ya maendeleo.

Anasema, “Wakati nachaguliwa hatukuwa hata na sekondari moja; leo tumejenga sekondari 35. Maji yalikuwa yanapatikana kwa asilimi 20 tu, huku umeme ulikuwa mjini Nzega na viunga vyake. Tulikuwa hatuna barabara, lakini leo unakwenda Mwanza kwa masaa matatu, wakati huko nyuma ilikuwa ni kutwa mzima.”

Anasema sasa umeme umefika hadi Neta, ambayo ni Nzega ndogo. Umefika hadi Mwaluziro, Itiro, Nhele na “sasa tumepata Sh. 400 milioni kwa ajili ya kupeleka umeme Ndala.” Fedha hizi zote zimetoka serikali kuu.

Wilaya imefanikiwa kuchimba mabwawa na malambo mbalimbali yakiwemo Mkiliziwa, Ibako, Igua, Ikindwa na megine mengi madogo, anasema Selelii.

Hata hivyo, Selelii anasema, pamoja na hali hii ya kuchafuana wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi, wananchi wanaona yaliyofanyika akiwa mbunge na wana kila sababu ya kupenda jimbo lao liongozwe na mbunge anayefanana nao kwa fikra na matendo.

Anasema yaliyokwishafanyika jimboni mwake ndiyo yanaonyesha kuwa tabia, mwenendo, fikra na vitendo vyake vinaoana na matakwa na mahitaji ya wapiga kura waliomweka bungeni.

Anaongeza, “Sidhani kwamba wana-Nzega wamebadilika. Bado wanahitaji mtendaji na mfuatiliaji wa viwango vyangu. Wakati ukifika, nasema siyo sasa hivi; wakati ukifika tutawaambia au kuwakumbusha hilo.”

Lucas Lumambo Selelii alizaliwa 4 Oktoba 1960 katika kijiji cha Ndala wilayani Nzega. Ameoa na ana watoto watatu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: