Lucy Owenya: Ninastahili, sikubebwa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 August 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
Lucy Fidelis Owenya

"SIKUINGIA bungeni kwa bahati mbaya." Hiyo ni kauli ya Lucy Fidelis Owenya, mbunge Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Owenya ni mmoja wa wabunge sita wa CHADEMA waliopatikana kupitia "dirisha" la viti maalum. Katika bunge la sasa, CHADEMA ina wabunge 11.

Katika mahojiano na MwanaHALISI wiki iliyopita, Owenya anasema, hakupata ubunge kwa kubebwa. "Sikubebwa. Nimeteuliwa kutokana na sifa nilizonazo. Mimi ni mwanachama wa CHADEMA na nilijaza fomu kuomba nafasi hii."

Anasema fomu zake zilipitia taratibu zote ikiwamo kujadiliwa na vikao vya juu vya chama chake. Hata hivyo ni mwanachama wa muda mrefu.

Owenya ni mtoto wa pili wa Philimon Ndesamburo, mfanyabiashara na mbunge wa Moshi Mjini (CHADEMA). Ndesamburo ndiye mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kilimanjaro.

"Nimekuwa mwanachama mwaminifu na nimejitolea kwa hali na mali katika ujenzi wa chama changu," anasema.

Owenya anasema inawezekana wakati jina lake linajadiliwa na vikao vya juu vya chama chake, Ndesamburo alikuwamo katika vikao hivyo lakini

kuwamo siko kulikoleta muwafaka wa vichwa vyote juu yake.

"Wale ni watu wenye heshima; waadilifu. Waliangalia sifa zangu na uwezo wangu," analeza Owenya.

Anasema, "Hoja ya kupendelewa na baba yangu haina mashiko. Amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC) ya CHADEMA tokea chama hiki kianzishwe. Kama alikuwa na uwezo wa kumpitisha mtu kuwa mbunge, kwa nini hakufanya hivyo 1995 au 2000 nilipotaka kuwa mbunge?" anahoji.

Ndani ya Bunge, Owenya ni msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Viwanda na Biashara. Anasema anafurahia kuteuliwa na viongozi wenzake kuwa msemaji wa wizara hiyo.

Anasema kwa jinsi alivyokuwa anafuatilia maendeleo ya viwanda nchini kabla hajaingia bungeni, amefurahi sana kuteuliwa kushika nafasi hiyo kutokana na kile alichoita, "CCM kushindwa kazi."

Anasema, "Pamoja na mali ghafi nyingi za viwandani kupatikana nchini, serikali bado imeshindwa kusimamia sekta hiyo." Anatoa mfano wa mwaka 2008 wakati sekta ya viwanda ilichangia chini ya asilimia 9.4 ya pato la taifa.

Akiongea kwa uchungu, Owenya anasema serikali imehujumu kiwanda cha matairi cha General Tyre cha Tanga hadi kusababisha kiwanda hicho kufungwa.

Miongoni mwa hujuma zilizofanywa katika kiwanda hicho ni ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 10 bilioni uliofanywa na wanaojiita wawekezaji ambao baadaye walitorokea nchini India.

Kuondoka kwa wawekezaji hao kulikofuatana na kiwanda kusimamia uzalishaji, kutafanya serikali kulipa mkopo wa Sh. 4.98 bilioni uliokopwa na wanaojiita wawekezaji katika mabenki ya Citi Bank na Hsbc ya nchini Marekani.

"Huu kama si ujuha ni kitu gani. Serikali imetelekeza kiwanda hiki kana kwamba nchi hii inatawaliwa na raia wa kigeni," anasema Owenya kwa uchungu.

Anasema mbali na kiwanda hicho, serikali imetelekeza shamba la mpira la Kihuhwi, lakini papo hapo inaagiza mpira kutoka Malasia na Brazil na kuacha mashamba ya mpira yavunwe kwa ajili ya kampuni ya Big-G zinazotengenezwa Kenya.

Anasema, "Hapa kuna ufisadi mwingine. Hatuwezi kukubali hali hii kuendelea. Nimejiandaa katika mkutano ujao wa Bunge, kuwasilisha hoja binafsi. Nataka serikali ifufue viwanda hivi na vingine kwa ajili ya uchumi wa taifa."

Owenya anarudia kauli za kila mwananchi, kwamba zoezi zima la ubinafishaji halikufanywa kwa makini, matokeo yake uchumi wa nchi umezorota. "Viwanda vingi vilivyobinafsishwa, kikiwamo kiwanda cha ngozi cha Moshi na kile cha magunia, vinafanya kazi chini ya viwango vilivyotarajiwa," anafafanua.

Badala ya kuongeza thamani na kuuza ngozi iliyokamilika, kiwanda hicho kinauza nje ngozi isiyosindikwa, jambo ambalo linapunguza mapato kwa taifa.

Hali kama hii ipo katika viwanda vingi ambavyo serikali imeingia ubia au imebinafisha. Ni viwanda vichache sana, tena vinavyoweza hata kuhesabika, ndiko ubinafishaji unaonekana kuleta tija.

Anasema kufungwa kwa viwanda viwili vya kutengeneza magunia kikiwamo cha Moshi ambacho kina uwezo wa kutengeneza magunia milion sita kwa mwaka, kumepunguza ajira ya wananchi kwa kiwango kikubwa. Watu 500 tayari wamepoteza ajira katika kiwanda hicho.

Owenya anasema hata kiwanda cha Morogoro cha magunia ambacho serikali inajitapa kuwa kinafanya vizuri, hakifanyi kazi kama inavyotakiwa. Kiwanda chenye uwezo wa kutengeneza magunia milion 10 kwa mwaka, hivi sasa kinafanya kazi chini ya asilimia 20.

Kutokana na hali hiyo, Owenya anaonya kwamba hata kauli mbiu ya "Kilimo Kwanza," haiwezi kufanikiwa iwapo serikali itaendeleza utamaduni wake wa kutelekeza viwanda vyake.

Matokeo ya kutelekeza viwanda tayari yameathiri upatikanaji wa magunia hasa ya mkonge ndani na nje ya nchi. Anasema hakuna nchi yeyote duniani ambayo imefanikiwa kutoa ajira za kutosha kwa wananchi wake bila kuimarisha viwanda vyake.

Aidha, Owenya anasema serikali inapoteza mabilioni ya shilingi kutokana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa nguo na kusababisha ushindani haramu wa biashara hiyo.

Kwa mfano, kontena la nguo ghafi (Grey cloth) linaloingizwa nchini kutoka nje kwa ajili ya kutengeneza vitenge na khanga, sehemu kubwa ya mzigo huo unakuwa nguo zilizokwishatengenezwa.

"Jozi moja ya kitenge kilichopitishwa kwa njia kama hii huuzwa hadi Sh. 3,000, wakati kitenge kilichoingia kihalali kinauzwa kati ya Sh.4000 na 4,500. Hii siyo njia sahihi ya kukuza uchumi," anasema.

Akizungumzia hali ya chama chake katika mkoa wa Kilimanjaro ambako yeye ndiko anatoka, Owenya anasema CHADEMA hakina mpinzani katika mkoa huo.

Anajitapa hilo litathibitika katika uchaguzi ujao wa mwakani.

"Pale Kilimanjaro, CHADEMA hakina mshindani. Hata uchaguzi ukifanyika leo, tuna uhakika wa kushinda. Mwaka 2010 upinzani unataka kuweka historia kwa kushinda majimbo mengi zaidi ya yale yaliyopatikana mwaka 1995," anasema kwa kujiamini.

Lucy Fidelis Owenya alizaliwa 2 Februari 1964 na ana shahada mbili, moja ya uzamili. Alipata shahada zote mbili nchini Uingereza.

Owenya amekuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Keys Hotels Travel and Tours kuanzia mwaka 2002 hadi 2005. Aliwahi pia kuwa meneja wa masoko wa kampuni hiyo kutoka mwaka 1995 hadi 1999.

Amewahi kuwa mshauri wa siasa wa CHADEMA mkoani Kilimanjaro. Lucy ameolewa na ana mtoto mmoja wa kiume – Yohane Owenya.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: