Lwakatare atikisa uongozi CUF


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 June 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
Wilfred Muganyizi Lwakatare

MWANACHAMA Na. 146 na mmoja wa waasisi wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilfred Muganyizi Lwakatare (47), amejiuzulu nafasi zote za uongozi ndani ya chama chake.

Lwakatare alikuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu na mjumbe katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya CUF.

Alitoa uamuzi wa kujiuzulu nyadhifa zake ndani ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kilichokuwa kinafanyika makao makuu ya CUF, Buguruni Dar es Salaam, Jumanne 9 Juni 2009.         

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, mjini Dar es Salaam, Lwakatare amesema amechukua uamuzi wa kujiuzulu nyadhifa zake katika chama ili kupata nafasi ya kupigania jimbo lake la uchaguzi la Bukoba Mjini.

Amesema, “Nimejiuzulu ili nipate nafasi ya kupigania jimbo langu. Ninaamini kwamba hili ni jimbo langu na kwamba katika uchaguzi uliopita ushindi wangu uliporwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).”

Lwakatare alikuwa mmoja wa waanzilishi, mwaka 1991 wa Chama Cha Wananchi (CCW) ambacho kilikuwa chini ya James Mapalala na Ludovick Bazigiza. Ndani ya CCW, Lwakatare alikuwa mratibu wa mkoa wa Kagera.

Ni CCW ya Mapalala ambayo mara baada ya kuruhusiwa vyama vingi nchini mwaka 1992, iliungana na KAMAHURU ya Zanzibar iliyokuwa inaongozwa na Shaaban Khamis Mloo na wanasiasa wengine visiwani humo.

Baada ya CUF kuzaliwa, Lwakatare akawa Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho mkoani Kagera. Alishika nafasi hiyo mwaka 1992 hadi 1994.

Mwaka 1994 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC), nafasi ambayo aliishika hadi mwaka 1998. Mwaka 1999 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu akiwakilisha Wilaya ya Bukoba. 

Vilevile kutoka mwaka 1999 hadi Aprili mwaka huu, Lwakatare alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF.

Lakatware amevuka mabonde na milima. Mwaka 1994 hadi 1999 aligombea uenyekiti wa Mtaa Omukituli, wilayani Bukoba kupitia chama chake.

Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Lwakatare alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge jimbo la Bukoba Mjini ambapo alishindwa kwa kura chache na mgombea wa CCM, Mujuni Kataraia.

“Sikukata tamaa. Nikajipanga na kujitosa katika kinyang’anyiro cha mwaka 2000 na nilifanikiwa kumchakaza Kataraia,” anasimulia.

Akiwa bungeni, wabunge wenzake wa Kambi ya Upinzani walimchagua kuwa kiongozi wao. Alishika nafasi hiyo mwaka 2002 hadi 2005.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Lwakatare alishindwa na Balozi Khamis Kagasheki aliyegombea kupitia CCM. Hakukubali matokeo na kesi ya kupinga ushindi wa Kagasheki bado inanguruma mahakamani.

Mbali na nafasi hizo za uongozi ndani ya CUF, Lwakatare amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam wa vyama vinne vya kujenga ushirikiano (CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na TLP).

Je, nini kimemtoa CUF? Amefukuzwa? Amesema, “Hapana. Kwanza, sijaondoka CUF. Mimi bado ni mwanachama wa chama hiki. Nilichofanya ni kujiuzulu nafasi zangu za uongozi ili nipate nafasi ya kujenga jimbo langu.”

Amesema hajafukuzwa na wala kushinikizwa kujiuzulu. “Uamuzi wa kujiuzulu ni wangu binafsi,” anaeleza.

Alipong’ang’anizwa kwamba anafikiria kwenda wapi baada ya kujiuzulu nafasi zake za uongozi katika CUF, Lwakatare hakutaka kujibu kwa haraka.

Alisema, “Mafanikio yote haya niliyopata yametokana na wananchi wa Bukoba. Nimekuwa mbunge kutokana na nguvu za wananchi. Hivyo, uamuzi wa mimi kuondoka CUF au kubaki, utatolewa na wananchi wa Bukoba ambao ni wapigakura wangu, wazazi wangu na washirika wangu wa kisiasa.”

Alipoulizwa kama hivyo ndivyo ilivyo, kwa nini ameamua kujiuzulu, Lwakatare alijibu, “Ni uamuzi wa kawaida. Ni labda kwa vile watu hawanifahamu.”

Amesema, “Mimi nimekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama (mtu wa pili kimamlaka katika shughuli za kiutendaji) kuanzia 1999 hadi 2009; shughuli niliyoamua kuifanya kwa dhati na kuisimamia.

Lwakatare amesema aliingia siasa moja kwa moja baada ya kujiuzulu kazi serikalini kwa kutoa notisi ya saa 24 na kuilipa serikali, mwajiri wake wakati huo, mishahara ya miezi mitatu.

“Sasa kama niliweza kuyafanya haya, kuna ajabu gani leo nikiamua kujiuzulu nafasi zangu za uongozi katika CUF,” anahoji.

Amesema, “Kama nilivyokwishasema, nimejiuzulu ili kuhakikisha narudisha jimbo langu na napata nafasi ya kuwatumikia wananchi wangu wa Bukoba, ambao naamini kuwa bado wanahitaji niwatumikie.”

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya CUF, Buguruni Dar es Salaam, wiki iliyopita, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba alithibitisha kujiuzulu kwa Lwakatare.

Alisema hakukuwa na shinikizo lolote kutoka kwa uongozi wake la kumtaka Lwakatare ajiuzulu. “Hakuwezi kuwa na shinikizo kwa kuwa Lwakatare hakuwa na tuhuma. Ni uamuzi wake binafsi,” alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alikiri nguvu ya Lwakatare katika siasa za kanda ya Ziwa Viktoria na hasa mkoani Kagera, na kwamba chama chake kilikuwa kinaangalia uwezekano wa kukutana naye.

Alisema Lwakatare alifanya uamuzi wa kujiuzulu muda mfupi kabla ya kikao cha Baraza Kuu kumalizika. Aliomba nafasi kwa mwenyekiti kutoa shukurani zake kwa wajumbe kwa kukitumikia chama hicho kutokana na kushindwa kufanya hivyo katika kikao kilichopita.

Lwakatare alipata elimu yake katika shule mbalimbali kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1985 ambako alipata shahada ya kwanza ya Elimu ya Utawala na Mahusiano ya Kimataifa (B.A. Public Admininstration and International Relations).

Baada ya kuhitimu chuo kikuu mwaka 1988, aliajiriwa serikalini. Alianza kazi ya Afisa Utumishi Mkuu mwandamizi katika Halmashauri ya Wilaya Iringa, kutoka mwaka 1988 hadi 1990.

Kutoka Iringa alihamishiwa Halmashauri ya Mji Bukoba ambako alikaa hadi 1998 alipohamishiwa Halmashauri ya Wilaya Urambo, mkoani Tabora.

Akiwa Tabora ndipo aliacha kazi kwa kutoa notisi ya saa 24 baada ya kuombwa na viongozi wa CUF kusaidia uendeshaji wa chama chao.

Lwakatare aliyezaliwa 4 Januari 1962, amepata mafunzo mbalimbali ya uongozi na utawala ndani na nje ya nchi. Ameoa na ana watoto.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: