Maalim Seif anashia Muungano


Rugemeleza Nshala's picture

Na Rugemeleza Nshala - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, ametoa kauli mbili tofauti kuhusiana na muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwanza, amesema mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano lazima yaweke kipengele cha kubadilishana nafasi ya urais kati ya Bara na Visiwani. 

Hii ni kwa vile katika miaka 45 ya Muungano, Zanzibar imetoa rais mara moja tu, wakati Bara imetoa rais mara tatu.

Pili,  amenukuliwa akisema, “Ni lazima Zanzibar iwe na benki kuu yake ili kulinda maslahi ya wananchi wake.” Amedai kuwa masilahi ya Zanzibar yanaminywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kauli ya Maalim Seif, kwanza ni mwendelezo uleule wa watu kutoka Zanzibar kutaka kuvunja Muungano na pili, makamu huyo wa kwanza wa rais anataka Zanzibar iendelee kupata upendeleo mwingine mkubwa kwenye serikali ya Muungano.

Muundo wa sasa wa Muungano umeiwezesha Zanzibar kuwa na wabunge 80 licha ya kuwa na watu wasiozidi 1 milioni. Hii inamaanisha kuwa mbunge mmoja wa Zanzibar anawakilisha watu 12,048.

Kwa upande wa Bara kuna wabunge 270, huku idadi ya watu ikiwa ni zaidi ya 45 milioni. Hivyo basi, kwa wastani kila mbunge mmoja wa Bara anawakilisha watu 166,666. Kwa mtu makini ataona wazi kuwa muundo huu si wa haki.

Utetezi wa wanasiasa wa Zanzibar na hata Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa wanaojiita, “Wazee wa Dar es Salaam,” Oktoba 2011, akisema Zanzibar ni nchi na ni lazima iwakilishwe kikamilifu katika Bunge, unapingana na ukweli.

Uwakilishi mkamilifu si kuwa na utitiri wa wawakilishi bali nguvu na mamlaka ambayo wawakilishi hao wanayo.

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri, hakuna mabadiliko yoyote ya katiba yanayohusu mambo ya Muungano yanayoweza kufanywa bila kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge kutoka kila upande – Bara na Zanzibar.

Kwa hiyo, hata kama Zanzibar ingekuwa na wabunge 20 katika Bunge la Muungano kigezo hicho cha katiba ni lazima kitimizwe.

Lakini kutokana na kuoneana haya na kuendeleza ulaji na ufisadi, idadi ya wabunge imekuwa kubwa bila sababu. Haingii akilini kuona mbunge kutoka Zanzibar anachaguliwa na watu 3000 au 4,000.

Kwa hiyo, Zanzibar ikichanganya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao ni 81 na wabunge wa Muungano inakuwa na wawakilishi 164 kwa watu milioni moja tu!

Kila mwananchi wa Zanzibar ana mwakilishi katika masuala yasiyohusu Muungano na mbunge katika mambo ya Muungano, wakati wa Bara anawakilishwa na mbunge mmoja tu. Muundo huu ni ukiukaji wa wazi wa kigezo cha usawa mbele ya sheria kwa mujibu wa katiba. 

Vilevile, upendeleo huu unaigharimu nchi fedha nyingi kwa kulipa mishahara na marupurupu ya wabunge na wawakilishi kwa kazi ndogo na huku wengi wao walioko bungeni bila haya wakidai kuongezewa. Huu ni utapanyaji wa rasilimali za nchi yetu unaofanywa na wanasiasa.

Upendeleo mwingine ni uwezo na fursa ya wabunge wa Zanzibar kujadili na kutolea maamuzi masuala yasiyohusu mambo ya Muungano wakati wale wa Bara hawana haki hiyo na hawana wawakilishi wao katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Kitendo hiki ni kinyume cha hati za makubaliano ya Muungano na kinaweza kuwa ni kigezo tosha kwa mwananchi, kutoka Bara, kupinga uhalali wa sheria zote zilizopitishwa na Bunge la Muungano ambazo hazihusu masuala ya Muungano.

Upendeleo wa Zanzibar haliishii katika masuala ya bunge. Wanasiasa kutoka huko wanapewa nafasi za uwaziri na ukatibu mkuu katika wizara ambazo hazihusu mambo ya Muungano.

Lakini hakuna hata mwanasiasa mmoja kutoka Bara ambaye Zanzibar ni waziri au katibu mkuu wa wizara isiyohusu mambo ya Muungano.

Huu ni ukiukaji mwingine wa wazi wa makubaliano ya Muungano na katiba ya nchi; ni mwendelezo wa kile ambacho Jaji Kahwa Lugakingira alikisema mwaka 1994 katika kesi ya Christopher Mtikila v. Mwanasheria Mkuu wa serikali,  kwamba mfumo wa Muungano ni ule wa msemo wa “chako chetu na changu changu.”

Aidha, hoja ya Maalim Seif ya kutaka urais uwe ni wa kupokezana si tu inakiuka haki za wananchi kugombea uongozi bali pia inataka kulinyima taifa uwezo wa kupata viongozi bora.

Haiwezekani kudai uongozi wa juu wa nchi kuwa wa zamu; hata mfumo wa sasa wa kutaka eti mgombea urais na mwenza wake watoke pande mbili za Muungano, ni ukiukaji mwingine wa katiba. Hata viti vya ubunge vya upendeleo ambavyo wagombea wake hawachaguliwi na wapigakura wote, ni wazi kwamba ni  ukiukwaji wa katiba.

Katika mabadiliko ya katiba ya mwaka 2010, Zanzibar imejitangaza kuwa nchi kamili, yenye Amiri Jeshi Mkuu na vikosi vyake vya ulinzi na usalama na sasa inataka Benki Kuu moja ya mambo ya Muungano.

Haingii akilini kwa nchi zilizoungana kisiasa na kiuchumi kuwa na benki kuu mbili tofauti; Bara yake na Zanzibar yake.

Hoja nyingine ni vizingiti vya kwa watu kutoka Bara kumiliki ardhi Zanzibar wakati Wazanzibari wanamiliki ardhi kubwa na vitega uchumi vingi Bara bila vikwazo.

Si hivyo tu: Hata uwezo wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania umepunguzwa na kubakia ule unaohusu kesi za madai na jinai na si masuala ya haki za binadamu.

Sasa hakuna tena kauli moja, sauti moja na ya mwisho, inayotoka kwenye nchi mbili zilizoungana inayoweza kutolewa na mahakama ya rufaa kuhusiana na mambo ya haki. Je, kama hivyo ndivyo, unaweza kusema kuwa nchi hiyo inafuata utawala wa sheria? Sasa kunapotokea mzozo wa kisheria wananchi waende wapi?

Jambo baya ni kwamba Maalim Seif ndiye aliokolewa kifungoni na Mahakama ya Rufaa lakini ndiye anatoa kauli za kutetea jambo kama hili. Inawezekana kuwa ni kwa vile ameshajiona yuko madarakani.

Hata hicho kinachoitwa, “sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011,” inakiuka katiba ya nchi. Imepitishwa bila kuwashirikisha wananchi kama ambavyo ibara ya 21(2) ya katiba inavyodai. Mfumo wa katiba haulipi Bunge au chombo kingine chochote kile, mamlaka ya kutunga katiba mpya. Bunge limepewa mamlaka ya kubadilisha katiba tu.

Lakini serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kudandia hoja hii, imewezesha kupitishwa sheria ambayo inakiuka katiba, jambo ambalo ikitokea mwananchi yeyote yule akifungua shauri mahakamani kupinga sheria hiyo, ataweza kushinda.

Utungaji wa katiba mpya unawezekana tu kama katiba ya sasa ingefanyiwa mabadiliko ili kuruhusu suala hilo pamoja na mchakato wake. Hivyo katiba hii inatakiwa kuwekewa kiraka cha 15 lakini serikali yenye shingo ngumu ya CCM “haiambiliki.”

Mwandishi wa makala hii, Rugemeleza Nshala, ni wakili wa mahakama kuu na msomaji wa siku nyingi wa MwanaHALISI. Kwa sasa, yuko masomoni nchini Marekani
0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: