Maandamano – Intelijensia = Utulivu


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Polisi wakiwashambulia waandamanaji Arusha

MARA hii tuanze na hesabu. M – i = U. Maana yake ni: Maandamano kutoa intelijensia ni sawa na Utulivu. Ukijibu namna hii umepata. Ukijibu tofauti, umekosa.

Usiende kubukua vitabu vingi. Nenda kwa yaliyotendeka; uliyoyaona na kushuhudia. Wala si zamani. Usidai kuwa umesahau. Ni wiki iliyopita na wiki hii.

Wiki iliyopita, mjini Mwanza, wananchi walifanya maandamano makubwa. Ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mashabiki na wengine waliojisikia kuungana na wabunge na viongozi wa chama hicho.

Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe ainaaina, walitembea hadi uwanja wa Furahisha, Kirumba. Wakasikiliza hotuba za viongozi. Wengine wakaitikia kwa kushangilia.

Wakati wote huo askari polisi wameangalia. Nia yao kuu ikiwa kuhakikisha kuwa ile shabaha ya kuitisha maandamano na mkutano wa hadhara, inatekelezwa bila mtu yoyote kuingilia kati; kuzuia waandamanaji; kuwapiga mawe, kutumia fursa hiyo kupora madukani au kuanzisha rabsha kwenye tukio hilo.

Waulize polisi nao watakwambia. Maandamano yalifanyika kwa utulivu. Hotuba zilitolewa. Kuna waliokubaliana na wahutubiaji. Kuna ambao hawakukubaliana lakini hawakujizuia kutekenyeka. Ni kanuni ya kutofautiana bila kupigana. Hilo ni darasa juu ya kuvumiliana.

Ningekuwa na tabia ya kupongeza, basi ningepongeza polisi. Ni bahati nzuri sina tabia hiyo. Hii ni kwa kuwa polisi walikuwa wanatenda wajibu wao na mara hii, walionyesha ujuzi wa kazi yao bila kutanguliza vizingiti vya “huenda kutakuwa na fujo.”

Vizingiti hivi ambavyo huko nyuma tuliviita “taarifa za intelijensia,” ndivyo chanzo cha kutosikilizana, gadhabu za baadhi ya askari, vurugu na hata vita vya maneno, mawe na silaha kati ya raia na polisi. Pale Mwanza hakukuwa na intelijensia.

Kwa hiyo, kwa mwendo wetu na kwa mujibu wa hesabu zetu, Maandamano-intelijensia= Utulivu au kwa ufupi: M - i = U. Mwanza wamepata. Wapi pengine?

Baada ya Mwanza, msafara wa CHADEMA uligawanyika, hawa huku hawa kule. Lakini mkutano mkubwa wa aina yake ulikuwa mjini Musoma, kwenye viwanja vya shule ya msingi ya Mukendo. Yalianza maandamano. Ukafuatia mkutano mkubwa.

Waulize polisi watakwambia. Hakukuwa na vurugu katika maandamano na kwenye mkutano mjini Musoma, kama ambavyo hakukuwa na vurugu Bunda. Viongozi wa CHADEMA waliandamana na wananchi na kufanya mikutano bila rabsha. Wakati wote huo askari polisi walichunga nani ataingiza kiza kwenye “vitu vya watu.”

Nia ya kuu ya polisi ilikuwa kuhakikisha kuwa ile shabaha ya kuitisha maandamano na mkutano wa hadhara, inatekelezwa bila mtu yoyote kuingilia kati; kuzuia waandamanaji; kuwapiga mawe, kutumia fursa hiyo kupora madukani au kuanzisha rabsha kwenye tukio hilo.

Kote ambako viongozi wa CHADEMA wamekwenda, wamepata ile hesabu ngumu ambayo imekuwa ikishinda wenye gadhabu na wasiotaka kusikiliza ujumbe tofauti. CHADEMA wameshinda: M – i = U. Wengine walioshinda hesabu hii ni polisi kote ambako chama hicho kimefanya mikutano na wananchi walioshiriki maandamano na mikutano.

Bado CHADEMA ina safari ndefu ya kuzunguka nchi nzima. Nimeambiwa na kiongozi mmoja wa chama hicho kuwa moja ya sababu zao kuu ni “kuwashukuru wananchi kwa kuwapa kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.”

Nimeambiwa ndio maana viongozi wamebeba kundi kubwa la wabunge wao ili wananchi wawaone na hao wabunge waweze kuongeza shukrani kwa wapigakura.

Basi funzo limepatikana. Vyama vya siasa visinyang’anywe haki yao ya kuandamana na kufanya mikutano ya hadhara kwa madai ya taarifa binafsi za intelijensia. Hii ni kwa sababu, wenye nia nzuri katika maandamano na mikutano, ni sehemu ya ulinzi wa mikutano hiyo.

Ni vema Rais Jakaya Kikwete ametambua na kusema, “Kufanya maandamano na mikutano ni haki ya msingi ya vyama vya siasa na raia.” Huu basi ni wakati mzuri wa vyama vya siasa na vingine vya kijamii kutoa wananchi katika giza lililowaghubika kwa karibu miaka 50 sasa.

Wananchi wapate fursa ya kusikia maoni tofauti na yale waliyosokomezwa kooni na masikioni kwa miaka hamsini. Wapate kujenga maoni yao wenyewe. Wapate kusema kilichoko moyoni; kujadiliana na hata kubishana ili kuwepo na “Taifa Linaloongea.”

Kama hatakuwepo wa kuleta rabsha, kwa nia ya kuharibu hesabu ambayo CHADEMA, polisi na wananchi tayari wameshinda, basi uhuru wa kutoa maoni – matamu, machungu, makali, mazito au vyovyote  yatakavyokuwa –  utakuwa umeandaliwa fursa nyingine ya kushamiri.

0713 614872
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: