Mabadiliko madogo ya mawaziri mzaha


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

HALI inaonesha kuwa wananchi hawajaelewa hasa ni nini lengo la Rais Dk. Ali Mohamed Shein kufanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri kwa kuwabadilisha nafasi mawaziri sita.

Lakini, mchambuzi mmoja ametokea kuamini anachokiona kwa kunieleza, “Sina shaka, Rais Shein alitaka kuwahifadhi mawaziri wawili. Waziri mmoja ni mzoefu; mwengine ni mwanagenzi.”

Ufafanuzi wake ni kwamba Dk. Shein ametaka kubaki na Ali Juma Shamhuna, ambaye hatima yake imekuwa ikisubiriwa kuwadia baada ya kutuhumiwa na wawakilishi wenzake kuwa amedharau azimio la Baraza la Wawakilishi.

Pia Dk. Shein ameamua kumpa muda zaidi Abdillah Jihad Hassan, ambaye amethibitisha kupwaya katika kusimamia wizara ya habari, utalii, utamaduni na michezo.

Kwa hivyo, alichokifanya Dk. Shein ni kumlinda Shamhuna sasa kabla ya serikali kuwasilisha msimamo rasmi wiki hii kuhusu uamuzi wa (Shamhuna) kushiriki kupeleka ombi Umoja wa Mataifa la Serikali ya Muungano kuongezewa eneo la bahari kuu kwa shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia.

Akiwa waziri anayesimamia ardhi, makaazi, maji na nishati, Shamhuna alijiingiza kichwakichwa kutoa ushirikiano kwa waziri wa eneo hilo kwa serikali ya Muungano, Profesa Anna Tibaijuka katika kuandaa na kuwasilisha ombi hilo.

Shamhuna amekiri ndani ya Baraza la Wawakilishi kushiriki kuandaa ombi na kutoa ofisa wake wa kufuatana na ujumbe aliouongoza Waziri Prof. Tibaijuka jijini New York, Marekani yalipo makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kuliwasilisha.

Hoja hiyo ilipoingizwa barazani na mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, ilileta mjadala mkali na wajumbe wengi wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walimtaka ajiuzulu au awajibishwe na rais.

Mwisho wa mjadala ni uamuzi wa Spika Pandu Ameir Kificho kuridhia hoja ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi, ambaye ndiye kiongozi wa serikali barazani, kuwa serikali ipewe nafasi ya kufuatilia suala hilo na itakuja kutoa msimamo rasmi.

Taarifa za ndani ya Ofisi ya Baraza la Wawakilishi, zinasema serikali itatoa msimamo kabla ya mkutano unaoendelea kufungwa mwisho wa wiki hii.

Inaonekana Rais amekusudia kwamba msimamo huo utakapowasilishwa, wawakilishi wasije wakakumbuka shinikizo za kumtaka amtupe Shamhuna.

Kumhamisha ni kumkwepesha na ghadhabu mpya za wawakilishi za kutaka awajibishwe. Wachambuzi wanasema hatua hiyo, “angalau itapumbaza wawakilishi kwa muda.”

Ila sasa, kuna mtizamo kwamba huko alikopelekwa, wizara ya elimu na mafunzo ya amali, ni eneo muhimu linalohitaji mwanasiasa mwenye uzalendo wa kweli.

Ipo shaka kama Shamhuna hatajisahau kama atendavyo au hataongoza kwa kutumia ubabe na jeuri kama ilivyo kawaida yake.

Zinapokuja taarifa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad, amelia ukumbini wakati akichangia muswada wa sheria ya bodi ya mitihani, ni dhahiri ameona mtihani kuwa chini yake.

Japo ni waziri mzoefu na kada mkubwa CCM, Shamhuna anasifika kwa uongozi wa mabavu na jeuri; na hayo huzidi anapokuwa na viongozi kutoka Chama cha Wananchi (CUF) anachokibeza.

Yawezekana Zahra, amegundua kuwa ule utulivu na mashirikiano ya kikazi alokuwa akiyapata kwa waziri Ramadhan Abdalla Shaaban, hatayapata tena.

Pale akifundishwa na kuelekezwa na labda kuvumiliwa na mwalimu huyo, bali sasa apaswa kujiandaa vizuri kutenda kwa kujiamini zaidi huku akikabili kauli za jeuri za Shamhuna.

Wala si peke yake mwenye hofu. Baadhi ya watendaji wa wizara nao wanasema wanajipanga kukabiliana na misimamo mikali ya waziri Shamhuna.

Wakati akiwa naibu waziri kiongozi, Shamhuna alikuwa akipatisha shida maofisa usalama waliokuwa wakimlinda. Baadhi yao waliwahi kumwambia mwanakolamu kuwa wanakosa utulivu wakimuona.

Huyo ndiye Ali Juma Shamhuna, mwanasiasa anaendeleza utamaduni uliomfikisha kuitwa ujanani octopus, pweza, ambaye anapopata moto, ile mikia hugandamana pamoja kwenye kifua – ishara ya ubinafsi.

Hii ina maana sekta ya elimu itakuwa kwenye mtihani vilevile. Hicho ni kizaazaa maana elimu ndio ufunguo wa maisha; ndio nguzo kuu ya maendeleo.

Waziri Jihad ni kama vile amefeli kiutendaji. Kama hana uwezo wa kutenda, ni bahati mbaya sana kwa kijana kama yeye. Niamini kuwa kilichomtatiza hasa, ni kuzidiwa mbinu na watendaji.

Niliwahi kumwambia asipokuwa makini atashindwa kazi. Ameteuliwa watendaji wenye elimu ingawa hawana historia ya kuleta ufanisi pale walipopangwa kuongoza.

Wao ni watendaji-wanasiasa. Wapenzi wakuu wa CCM na wahafidhina. Hawaamini katika mabadiliko kutoka siasa chafu na za husda, na kuingia kwa siasa za maridhiano, zilizoasisiwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Wiki kadhaa tangu nilipokutana naye, nikaanza kusikia ameshindwa kurekebisha mambo katika mkataba wa kubinafsisha vitengo vya kibiashara vya Hoteli ya Bwawani.

Tena nikabaini amedanganywa na watendaji wake katika kuipeleka barazani sheria mpya ya haki ya habari iliyoridhiwa na washiriki mbalimbali.

Tamati ya ujahili (taz., ujinga) wake ikawadia pale aliposakamwa hadharani na Maalim Seif Shariff Hamad, katibu mkuu wa CUF, ambaye alimsema katika nafasi yake ya makamu wa kwanza wa rais kuwa hawajibiki kufuatilia majukumu yake.

Yaliyomkuta, ni dhahiri yamewapendeza katibu mkuu, Ali Mwinyikai, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) linalojumuisha Televisheni (TvZ) na Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ).

Wakurugenzi wake, Hassan Abdalla Mitawi (ZBC) na wa Idara ya Habari (MAELEZO), Yussuf Omar Chunda nao ni watendaji wasiopenda mabadiliko.

Hawa ni tofauti na Rafii Haji Makame, mwandishi wa habari mkongwe kama wao ambaye anaongoza STZ huku akisifiwa kwa mafanikio yaliyokwishaanza kuonekana.

Dk. Shein amemtoa Mansour Yussuf Himid ndani ya Baraza la Mawaziri akisimamia kilimo na maliasili, na kubaki waziri asiyekuwa na wizara maalum. Nafasi yake ameteuliwa Suleiman Othman Nyanga.

Inasemwa kuwa Mansour ameomba kupunguziwa majukumu kutokana na ugonjwa wa miguu. Lakini hata Nyanga amekuwa mgonjwa kwa muda sasa. Haijaeleweka ugonjwa unaomsumbua.

Waziri Jihad amebadilishwa wizara na mwana-CUF mwenzake, Dk. Said Ali Mbarouk, mwakilishi wa Gando aliyefana katika wizara ya mifugo na uvuvi.

Wakati sekta hizi za kichocheo cha ukuaji wa pato la taifa na uchumi wa familia za wananchi, zimeanza kufaidi matunda ya uongozi mzuri, kuondolewa kwa daktari, ni faraja kubwa kwa watendaji wahuni ambao aliwadhibiti.

Bado waziri Jihad amepewa mtihani mpya hapo.

Na haya ndiyo yanayothibitisha kuwa mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), si mali kitu. Hayataleta mabadiliko ya ufanisi wala hayataondoa watendaji wakorofi.

0
No votes yet