Machifu Jeep, wananchi nyoka

- Ndani ya utajiri wa dhahabu Ghana
GAZETI la MwanaHALISI linafanya utafiti kuangalia matatizo mbalimbali yaliyopo katika sekta ya madini nchini Tanzania.
Lakini mwandishi wetu, EZEKIEL KAMWAGA, anahudhuria mafunzo Accra, Ghana, yanayohusiana na mapato katika madini, mafuta na gesi. Wiki iliyopita alitembelea vijiji vinavyopakana na mgodi wa dhahabu wa Kenyasi. Fuatilia alichogundua
WAKATI Chifu (Nana) Akumfi Ameyaw, wa eneo la Kenyasi ndani ya utawala wa Brong, anapohudhuria katika sherehe, mavazi yake mwilini huwa yamepambwa na dhahabu tupu.
Kiwango cha dhahabu inayosarifiwa kwenye mavazi hayo huwa kikubwa kiasi cha mavazi kuwa mazito. Anahitaji msaada kumudu kunyanyua mikono.
Kwa hivyo, wasaidizi wake ndio hufanya kazi hiyo kila Chifu Akumfi anapotaka kutembea. Wanafanya hivyo pale chifu anapotaka kusalimia ‘watu wake.’
Eneo la Kenyasi liko ndani ya manispaa ya Sunyani, katika Jimbo la Ashanti, ambalo ndilo linaloongoza katika majimbo ya Ghana kwa utajiri wa dhahabu.
Nyaraka zinaonyesha jimbo hili lina historia ya kuzalisha dhahabu kwa zaidi ya miaka 100 sasa.
Upande wa pili kutoka mgodi wa dhahabu unaoendeshwa na Newmont – kampuni ya wawekezaji kutoka Marekani – uliopo Kenyasi, wananchi wa kijiji cha Ahapo wanalalamika kuwa dhahabu inayochimbwa karibu nao imewaletea laana.
Kwamba kwa mara ya kwanza katika historia yao, wameanza kukumbwa na balaa la njaa, magonjwa mageni ya ngozi na mwili. Pia wanalia na hali ngumu ya maisha.
“Hadi miaka kumi iliyopita, hali yetu hapa haikuwa mbaya sana. Hata kama kulikuwa na shida, si kwa kiwango cha sasa maana hali ni mbaya sana,” anasema Kofi Kodjo, mwanakijiji aliyezungumza na MwanaHALISI wiki iliyopita.
Nilikuwa nimefuatana na kundi la waandishi wa habari na wanaharakati wa masuala ya kijamii wanaoshiriki mafunzo ya wiki mbili kuhusu utawala bora katika mapato yanayotokana na madini, mafuta na gesi nchini Ghana.
Mgodi huo unaozalisha aunsi (wakia) 515,000 za dhahabu kwa mwaka, ulianza kazi mwaka 2006 kwa ahadi mbalimbali zikiwamo za wawekezaji kuwapa wenyeji ajira, kulipa kodi kwa serikali itakayowezesha kuimarishwa kwa huduma za jamii.
Ahadi nyingine ya wawekezaji ni kulipa fidia wananchi watakaohamishwa katika eneo hilo kwa ajili ya kupisha shughuli za uchimbaji mkubwa kwenye mgodi huo.
Hata hivyo, Kodjo na wananchi wengine wanasema hawajalipwa fidia yoyote hadi leo – miaka minne baadaye – ingawa mgodi umeshaanza shughuli na kulipa baadhi ya waliokuwapo.
“Mimi na familia yangu tulikuwa tukitegemea shughuli za kilimo cha kokoa kabla ya kuja kwa mgodi huu lakini ardhi yote sasa imechukuliwa na sisi hatuna pa kulima wala shughuli nyingine ya maana ya kiuchumi,” anasema.
Hali ya kiuchumi ya wanakijiji wa Ahapo inatia huruma. Kodjo mwenyewe alizungumza na waandishi na wanaharakati, akiwa nje ya nyumba yake ya udongo, na pekupeku miguuni.
Shati alilovaa lina kifungo kimoja tu huku suruali yake ikionyesha imechakaa mno. Ni dalili za ufukara ndani ya hazina kubwa ya dhahabu.
Uhamishaji huo wa wananchi pamoja na uchimbaji wa madini umesababisha kukatwa kwa eneo kubwa la msitu lililokuwa linahifadhi wanyama wa aina mbalimbali, wakiwamo wa hatari.
Kwa mujibu wa Felicity Kwadwo, sasa nyoka wanavamia maeneo ya makazi ya watu baada ya kulazimika kukimbia mapori yaliyoteketezwa.
“Hivi ninavyozungumza nanyi, waume zetu wanaogopa kwenda kutafuta riziki nje ya makazi tunayoishi, kwa kuogopa watoto wataliwa na nyoka na chatu. Kuna chatu wakubwa sana wanaokuja vijijini siku hizi,” anasema Felicity.
“Chatu wamekosa vyakula kwa kuwa mapori yamekatwa… wanakula chochote kilicho mbele yao na watoto ni rahisi kuwafikia wasipokuwa katika uangalizi wa wazazi.
“Hivi leo (siku hiyo) tumeua (chatu) mmoja na tumempiga picha,” alisema huku akionyesha picha hiyo.
Hakuna takwimu halisi za mapato kutokana na mgodi huo, lakini ipo ripoti inayoonyesha Newmont wamelipa kwa serikali dola 47.8 milioni za Marekani kama mrahaba kutoka walipoanza uzalishaji mwaka 2006 mpaka mwaka huu.
Umbali wa kilomita moja kutoka eneo la mgodi wa dhahabu, hakuonekani nyumba ya kisasa, ambayo angalau imejengwa kwa matofali na kuezekwa kwa mabati. Umasikini unaonekana wazi kila mahali.
Hata hivyo, wenye mgodi wanajitetea. Wametoa ajira kwa watu 4,000 tangu walipoanza kazi. Asilimia 96 ya waajiriwa hao ni raia wa Ghana, asilimia 36 yao ni watu wenye asili ya eneo la Sunyani.
Hata hivyo, mwanaharakati wa masuala ya jamii, Hannah Okarang, anasema wakati wananchi walipokuwa wakiruhusiwa kuchimba dhahabu, kabla ya wawekezaji wa sasa (Newmont) kufika, watu wengi zaidi walipata ajira kuliko sasa.
Nasoma kipeperushi kilichotolewa na Newmont kikieleza kwamba kampuni hiyo inalalamikia tatizo kubwa la wananchi kuongeza thamani ya mali zao wanapojua kuna kazi ya kutathmini mali kwa ajili ya wawekezaji kulipa fidia.
Tatizo hilo, wanasema Newmont, limechochea migogoro mingi kati yao na wananchi na kwamba hiyo wandai ndio sababu kubwa ya ulipaji fidia kwa baadhi ya wenye mali, kuchelewa.
Hali mbaya hiyo tuliyokuta katika vijiji tulivyobahatika kufika, ni tofauti na tulipokuwa kwenye ofisi za halmashauri ya mji. Hapa tulikwenda kuonana na machifu wa eneo.
Machifu watatu walikubali kukutana nasi. Lakini baada ya kuwa wameonyesha bashasha na uchangamfu mkubwa wakati wa kutambulishana, walibadilika ghafla walipoulizwa maswali.
Walianza hofu walipobaini wageni wao ni waandishi wa habari na wanaharakati wa masuala ya kijamii. Tulitaka waeleze kinachowapa jeuri ya kutapanya mapato yatokanayo na dhahabu huku wakiwaacha wananchi hohehahe.
Wakati wanawasili halmashauri walifika kwa magari ya kifahari aina ya Jeep na Damler yaliyotengenezwa nchini Marekani.
Wamevalia mikufu, pete na shanga hadi mguuni, zote zikiwa zimetengenezwa kwa dhahabu. Mavazi yao ya jadi yalionesha baadhi ya sehemu za miili yao. Hali za machifu hao zilionesha dhahiri wana afya nzuri.
Zogo lilianza mara baada ya wanaharakati kutaka kujua ni kwa vipi machifu hao wanatumia kwa matanuzi fedha zinazolipwa na makampuni ya madini kama kodi mbalimbali.
“Nyie ni kina nani?,” alihoji Chifu Ameyaw. Akaendelea, “Sisi tuko hapa kwa ridhaa ya nchi yetu, ninyi ni nani hata mtake kutukagua? Nani amewapa idhini hiyo? Hivi wewe unaweza kumkagua chifu huko (kwenu) unakotoka?”
Ni mgogoro sasa. Maelewano hayakuwapo. Hoja yao machifu ikawa “ugomvi wetu ni dhidi ya wazungu wanaokuja kutwaa mali zetu na siyo wa sisi kwa sisi.”
Chifu Ameyaw hakustahili kusema kuna “usisi” kati yake na sisi wanaharakati au wananchi walio chini yao. Yeye nyumbani kwake ana dhahabu kibao, anapanda gari la bei mbaya na ana huduma ya uhakika ya umeme.
Bali kina Kwadwo wanafukuzana na nyoka na chatu. Hawana umeme, hawana baiskeli na hawana hospitali kwa wagonjwa mahututi. Hizi ni dunia mbili tofauti ndani ya eneo moja katika nchi hii inayosifika kwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki miongoni mwa nchi za Afrika.
Wakati nikipanda basi kurudi Accra Jumapili iliyopita ili kuendelea na mafunzo, kwa mara ya kwanza, nikasema kumbe Tanzania hatukukosea kuachana na uchifu.
Au machifu wanaiba kidogo kuliko wasio na damu ya uchifu?