Machinga Complex limejaa kasoro


Adam Maleta's picture

Na Adam Maleta - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version

WIKI kadhaa zilizopita Rais Jakaya Kikwete alihoji kwa nini mpaka sasa biashara katika jengo la Machinga Complex lililopo Ilala, Dar es Salaam hazifanyiki kama ilivyotarajiwa ilhali serikali imetumia fedha nyingi tena za mkopo kulijenga.

Jengo lile lilijengwa kwa ajili ya kuwapunguzia adha wafanyabiashara ndogondogo, na katika kampeni zake za mwaka jana, Rais Kikwete aliahidi kujenga majengo mengine katika kila wilaya.

Hata hivyo, Machinga Complex jengo la kwanza kubwa kujengwa kutokana na ahadi zake za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, limemsononesha. Halitumiki ipasavyo na hivyo kuonekana ni upotevu tu wa fedha.

Watendaji wakuu wa serikalini na viongozi wa jengo lile, walitoa majibu wakidai kuwa biashara hazifanyiki kama ilivyotarajiwa kwa sababu chini, kuzunguka jengo, kuna wafanyabiashara wasio rasmi, wanaosababisha wateja wasipande juu ghorofani, hivyo kusababisha biashara juu kuzorota.

Pamoja na sababu hizo, kwa mtazamo wangu mambo kadhaa ya kitaalamu hayakuzingatiwa kabla ya kujengwa jengo lile kubwa na la aina yake nchini kwa ajili ya biashara.

Kwanza ni jengo lenyewe kujengwa refu bila kuwa na lifti. Kukosekana kwa lifti ni kikwazo kwa biashara kwani wateja hajisikia tabu kupanda hadi ghorofa ya tano, kwa miguu, kununua shati la shilingi elfu mbili au soksi za shilingi elfu moja au akale ubwabwa wa ‘buku’.

Pili ni udogo wa vizimba vya kufanyia biashara. Hatua ya kumpa mtu kizimba chenye upana wa futi mbili eti afanyie biashara ni mzaha.

Tatu ni urasimu katika ugawaji vizimba. Kulikuwa na urasimu mkubwa katika kupata nafasi ya kufanyia biashara katika Machinga Complex. Wafanyabiashara wengi wenye sifa za kupata nafasi pale hawakupata.

Nafasi ziligawiwa kwa kujuana. Walisema nafasi zitagawanywa kwa vikundi, hivyo wafanyabiashara walishauriwa kujiunga katika vikundi ili wapate nafasi.

Walifanya hivyo, lakini cha kushangaza ni kwamba kikundi chenye wanachama 400 kimepewa nafasi sabini tu, kingine kina wanachama 40 kimepewa nafasi kumi na saba tu, kingine kina wanachama 20 kimepewa nafasi tano. Hii maana yake nini?

Ni kweli si wafanyabiashara wote waliohitaji nafasi wangeweza kupata, lakini pia mgawanyo walioufanya haukuwa sawa. Nafasi nyingi zilihodhiwa na “wakubwa” wenyewe.

Nne ni kwamba soko limejengwa bila ya kuzingatia jiografia na mahitaji ya eneo husika. Jengo limejengwa katika mtaa wa Lindi, mtaa ambao ni mashuhuri kwa biashara ya spea za magari.

Kuanzia barabara ya Kawawa, kushuka na mtaa wa Lindi mpaka kona ya Lindi na Msimbazi, kote kuna maduka ya spea za magari. Sasa kwenda kujenga soko la nguo katika eneo lile sidhani kama ilistahili.

Hii inasababisha soko kukosa ushirikiano toka kwa wafanyabiashara wanaolizunguka kwa sababu biashara zao hazina mwingiliano; spea za magari  na nguo wapi na wapi?

Ukweli kukosekana kwa mwingiliano wa kibiashara ni sawa na kujenga kiwanda cha kubangua korosho Nzega mkoani Tabora badala ya Masasi, Mtwara, au ilikuwa sawa na kujenga kiwanda cha kusindika machungwa Mbarali, Mbeya badala ya Muheza, Tanga ambako yanapatikana kwa wingi.

Ushauri

Moja ya sababu kubwa za wafanyabiashara wadogo kupendelea Mtaa wa Kongo ni kwa vile eneo lile lina huduma nyingi hivyo linavutia watu wengi.

Nashauri, ili biashara zifanyike kama ilivyokusudiwa katika Machinga Complex, zitafutwe huduma kama ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zitakuwa za lazima kwa wateja kuzifuata ziwekwe juu  kwenye ghorofa kuanzia ya tatu na kuendelea.

Wakati wafanyabiashara wakifuata huduma juu, wakati wakipanda au kushuka wataweza kuona, kuvutiwa na hatimaye kununua bidhaa.

Aidha, serikali iangalie upya ule utaratibu wa vizimba kama kuna uwezekano tukubali hasara, tuondoe vile vizimba na tuweke meza kama tulivyozoea.

Vilevile, uangaliwe upya utaratibu wa mgawanyo wa nafasi za kufanyia biashara. Wale wenye sifa na uwezo wa kufanya biashara wapate nafasi na si kama ilivyo sasa, wengi wa waliopata vizimba hawana sifa wala uwezo wa kufanya biashara.

Kadhalika siafiki kusudio la serikali kulivunja soko la Mchikichini ili wafanyabiahara wake wahamishiwe Machinga Complex kama mkakati wa kuimarisha biashara katika jingo hilo. Hilo haliwezi kuwa suluhisho.

Lengo la kujenga Machinga Complex lilikuwa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo wanaotembeza nguo na ambao kimsingi hawana nafasi za kufanyia biashara. Vipi Mchikichini wahamishwe wakati tayari wana maeneo rasmi ya kufanyia biashara?

Mwandishi wa makala hii maarufu kama Kaboyashi ni mfanyabiashara wa spea za magari katika mtaa wa New Kisutu karibu na Machinga Complex na ni msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa simu 0715 368185 / 0754 368185
0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)