Madega alipania "kuiuza" Yanga

SAFARI ya Yanga katika michuano migumu, yenye mvuto na utajiri mkubwa wa fedha katika ngazi za klabu barani Afrika, Ligi ya Mabingwa imefikia mwisho.
Kipigo cha bao 1-0 jijini Dar es Salaam ndicho kilichokamilisha safari hiyo, baada ya kushindwa kuyapiku matokeo ya kipigo cha 3-0 ilichokipata katika mchezo wa kwanza huko Cairo, Misri.
Kwa Yanga ambayo tayari ina tiketi ya michuano kama hiyo mwaka kesho, imedhihirika si lolote si choichote mbele ya timu za Waarabu. Mbele ya Ahly pekee, hii ni mara ya sita kukutana nayo, mara zote ikishindwa kufurukuta.
Ushindi mkubwa kwa Yanga mbele ya Ahly ni sare, tena mara mbili tu mwaka 1982 ambako ilitoka 1-1 baada ya kuwa imefungwa 5-0 huko Cairo.
Mwaka 1988 zilishindwa kufungana Dar es Salaam, baada ya Ahly kushinda 4-0 huko Cairo.
Mwaka huu tumeshuhudia Yanga ikigeuzwa asusa nyumbani na ugenini katika kampeni za kuusaka ubingwa unaokwenda sambamba na donge nono la dola milioni moja za Kimarekani (sh bilioni 1.3).
Siyo siri, kwa kutolewa na Ahly Yanga wanaweza kuanza kushikana uchawi, lakini ukweli utabaki pale pale, Ahly ni maji marefu kwa Yanga.
Ni timu bora katika kila hali, na kama isingekuwa kufuata utaratibu, Ahly wangeweza kucheza katika ligi yoyote kubwa duniani na kutikisa. Wana uwezo huo.
Watawala katika soka ya Afrika, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wanautambua ukali wa Ahly na hata kuitangaza kuwa Klabu Bora ya Karne Afrika mwaka 2000.
Ni klabu pekee ya Afrika kuwahi kuwakilisha mara nyingi katika michuano ya FIFA ya Klabu Bingwa ya Dunia. Imeshiriki mara tatu kati ya tano za michuano hiyo, na mara moja ilitikisa na kushika nafasi ya tatu mwaka 2006.
Mwaka huo pia ilitoa mfungaji bora, bilionea Mohamed Aboutrika kutokana na mabao yake matatu, akiwafunika nyota kama wa Barcelona ya Hispania walioshiriki pia michuano hiyo na kushika nafasi ya pili, bingwa akiwa Internacional ya Brazil. Ahly imeshiriki pia mwaka 2005 na 2008.
Pia ina tiketi ya michuano ya mwaka huu. Vigezo hivyo, klabu hiyo iliyoanzishwa zaidi ya miaka 100 iliyopita, yaweza kuonyesha jinsi isivyo timu ya kubahatisha kama zilivyo klabu zetu kubwa zinazokaribia kusherehekea miaka 100 tangu kuanzishwa, lakini zikipata `sifuri’ katika maendeleo ndani na nje ya uwanja.
Ni kweli katika soka lolote linaweza kutokea, lakini kauli ya Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega baada ya kuchapwa 3-0 kwa kweli iliwaduwaza wengi na kuwajaza `ujinga’.
Alitamba Yanga ingelipa kisasi na kuizamisha Ahly kwa 4-0 Dar es Salaam! Kwa wanaofahamu jinsi Ahly na Yanga zilivyo sawa na mbingu na ardhi kwa hatua za soka, waligundua mara moja kwamba Madega alipiga porojo.
Miongoni mwao ni kocha Profesa Dusan Kondic, aliyetamka mara baada ya kipigo cha Cairo kwamba, hawana ujanja wa kuitoa Ahly kutokana na kiwango alichokishuhudia.
Alionekana mbaya na asiyejua majukumu yake, huku Madega akizidi kuwajaza mashabiki ujinga kuwa utawala wa Waarabu kwa Yanga sasa utaishia Dar es Salaam.
Alishikilia msimamo huo kiasi cha wengi kuamini huenda ndoto zikatimia, lakini maswali yakaja, kwa soka ipi ya Yanga ya kuitoa Ahly?
Mbona haikuwa na mikakati ya kiufundi zaidi ya porojo za uwanja, hasa za kuung’ng’ania ule wa zamani wa taifa eti wachezaji wameuzoea na kuamini utakuwa kaburi la Waarabu?
Yanga ilionekana kuwa na mbinu zile zile, sana sana ilizidisha uchovu kwa wachezaji kwa kuwapa mazoezi ya ziada, lakini yasiyo na mabadiliko makubwa na yale yanayoonekana wakati klabu hiyo inapojiandaa kwa mechi za Ligi Kuu ya Bara.
Kikubwa kinachotafsiriwa ni kwamba, Madega alilenga zaidi kuitangaza mechi ya Ahly na `kuiuza’ ili mashabiki wafurike uwanjani ili kutunisha mapato ya klabu, lakini suala la ushindi lilishaota mbawa.
Tujiulize, Yanga au klabu zetu kwa ujumla zitakuwa dhaifu katika michuano ya kimataifa mpaka lini?
Mbona zina muda wa maandalizi, hasa baada ya mabadiliko ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi? Mathalani, Yanga ingawa imeshatolewa, ina miezi tisa ya kujiandaa kwa michuano ya mwaka 2010.
Kama timu ina nguvu ya kiuchumi inayotoka kwa mfadhili wake Yussuf Manji, kwanini viongozi na benchi la ufundi wasione mbali na kujipanga mapema kufanya vizuri mwaka kesho?
Kwa kuwa tumezoea kuendesha mambo kwa staili ya `Bora Liende’, haitashangaza kusikia mbwembwe za usajili unaotafuna mamilioni ya shilingi, lakini nguvu kubwa ikielekezwa katika Ligi Kuu ya Bara ambayo bingwa hupata kiasi kidogo cha fedha, badala ya kuhamishia makali na mikakati katika michuano ya kimataifa ambako licha ya kuwa na ushindani, kuna fedha na soko kwa wachezaji.
Huko ndiko tunakopaswa kuelekeza macho kwa sasa, si kuinama chini na tukiinua kichwa ni kuipangia mikakati Simba au Yanga, basi? Tutawaacha Ahly na wengine wakitamba Afrika hadi lini?
Tukumbuke nao hawakuibuka na kuyafikia mafanikio, walituliza akili, wakapanga mikakati na ikapangika, ndiyo maana leo wanalia kivulini.
Wakati umefika sasa nasi tuondokane na ulimbukeni wa kusaka heshima kwa Simba na Yanga na kuvizia mapato ya milangoni pekee kama tulivyoshuhudia Madega akiipigia debe mechi ilimradi timu ivune pesa kwa kuwavuta mashabiki wengi uwanjani.