Madega na vita ya Yanga kwa Ahly


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 March 2009

Printer-friendly version

PRESHA inapanda, presha inashuka. Kwa hakika ndiyo hali inayoweza kufikirika kwa sasa miongoni mwa mashabiki wa klabu za Yanga na Al Ahly ya Misri.

Miamba hiyo itakutana wiki ijayo katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, michuano yenye hadhi, utajiri mkubwa wa fedha na vipaji katika ngazi za klabu barani Afrika.

Yanga itatia mguu wake wa kwanza ugenini Cairo , kabla ya kusubiri kurudiana na Ahly, mabingwa mara sita wa Afrika wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam .

Kwa hakika, ingawa Yanga inakutana na kigogo kwelikweli katika soka ya Afrika, bado imani ya mashabiki wake iko juu kutokana na kuwa na kikosi imara, benchi imara la ufundi, udhamini na ufadhili wa uhakika.

Haya kwa pamoja yanaiweka Yanga juu. Lakini kwa bahati mbaya, bundi mbaya anaonekana kuanza kulia kwa Wanayanga, ikiwa ni siku chache kabla ya vita dhidi ya Waarabu hao wa Misri.

Ndiyo, ni bundi mbaya kwa sababu katika kipindi kigumu kama hiki timu ilipaswa kuwa na mshikamano wa hali ya juu.

Lakini tunachokishuhudia ni kinyume, tunashuhudia viongozi wakiparuana makucha na mastaa wao ambao kwa hakika wakati huu walipaswa kuelekeza akili yao katika mchezo dhidi ya Ahly, na si vita dhidi ya `wakubwa’ wa klabu.

Katika mazingira ya aina hii, ni mchezaji gani ataweza kufanya vizuri uwanjani kama akili yake imeshajeruhiwa kisaikolojia?

Labda tukumbushane yaliyojiri hivi karibuni. Kwamba, Jumatano iliyopita wachezaji wawili raia wa Kenya wanaochezea Yanga, Boniface Ambani na George Owino, walitishia kuondoka na kurejea kwao, baada ya kufukuzwa katika Hoteli ya Lamada, walikokuwa wakiishi.

Wachezaji hao walitoa vitisho hivyo walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli hiyo iliyopo Ilala, mjini Dar es Salaam , baada ya kutakiwa na uongozi wa Lamada kuondoka hotelini hapo, kwa kuwa uongozi wa Yanga umesitisha malipo ya vyumba wanavyoishi.

Mbali na Ambani na Owino, wachezaji wengine wa kigeni waliokuwa wakiishi kwenye hoteli hiyo ni Mike Baraza, Maurice Sunguti, wote raia wa Kenya , na Obren Curkovic, raia wa Serbia .

Walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, wachezaji hao walijifanya hawajui kinachoendelea hadi wao kutupiwa virago Lamada, eti walidhani uongozi wa Yanga umelimbikiza deni.

Kwa waliosikia madai ya wachezaji wakati huo, walikuwa na kila sababu ya kuulaani uongozi kwa kusababisha adha hiyo, lakini majibu yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Yanga baadaye, yalibainisha ukweli.

Ukweli kwamba, kuna mgogoro kati ya uongozi wa klabu hiyo na wachezaji wake hao raia wa kigeni, kuhusu makazi.

Kwa mujibu wa Madega, uongozi umewapangia nyumba wachezaji hao ili waishi kwa pamoja, kuliko kuishi hotelini, lakini wachezaji hao inaonekana hawakubaliani nyumba waliyopangiwa.

Madega, alisema wachezaji hao waligoma kuhamia kwenye nyumba waliyopangiwa, maeneo ya Sinza mjini Dar es Salaam na kutaka kuendelea kuishi Lamada.

Mwenyekiti huyo wa Yanga, alisema uongozi wake hauko tayari kuyumbishwa na wachezaji hao, ndiyo maana uliweka mkakati na uongozi wa hoteli hiyo ili waondolewe kwa nguvu, mkakati ambao Madega alijisifu ulifanikiwa.

“Tulisitisha malipo tulipoona wanagoma kuhama, hatuwezi kubembeleza wachezaji fulani wakati timu ni ya wachezaji wote waliosajiliwa,” alikaririwa akisema Madega.

Kinachoonekana hapa ni kutaka kuonyeshana ubabe kati ya wachezaji hao wa kigeni na viongozi wa klabu hiyo, kwamba nani zaidi, lakini ukweli ni kwamba huu si wakati wa Yanga kuingia malumbano au mgogoro wa aina yoyote, hasa ikizingatiwa wana mtihani mkubwa mbele yao .

Al Ahly ni timu nzuri, yenye uzoefu na ubora wa hali ya juu katika michuano ya Afrika, hivyo makosa kama yanayofanywa na Wanayanga kwa sasa, ni sawa na kuipalilia tiketi ya kutupwa nje ya michuano hiyo.

Hayo si matarajio ya Wanayanga na kamwe matokeo mabaya hayataweza kupokelewa vizuri kutokana na imani waliyojazwa wanazi wa klabu hiyo tangu kuanza kwa msimu huu.

Ilianza kwa kusajili nyota halisi wa soka kutoka mataifa mbalimbali, ya Afrika na Ulaya, tena kwa bei mbaya dhamira ikiwa kufuta rekodi ya kuwa wasindikizaji katika michuano mikubwa ya Afrika.

Ikajaziwa wataalamu wa ufundi kutoka Ulaya, na zaidi ya yote ikapewa jeuri ya fedha kutoka kwa wadhamini na wafadhili kama Yussuf Mehboob Manji.

Kwa mambo haya matatu, ni wachache wanaoweza kuamini kuwa Yanga hii haitakuwa na ubavu mbele ya Al Ahly. Inaweza, tena sana tu, lakini kama watajipanga kutimiza ndoto yao .

Lakini kwa staili hii mpya ya ubabe na kutunishiana misuli baina ya wachezaji na viongozi, kamwe haileti picha nzuri, hasa ikizingatiwa masuala yenyewe ni madogo na yaliyoweza kumalizwa hata kabla ya kuvifikia vyombo vya habari.

Hayo tisa, kumi ni hili la Ambani kwenda majaribio China ! Mbona inashangaza katika saa hizi za mwisho za vita ya Yanga mbele ya Ahly? Kwa ushawishi gani wa soka ya China na utajiri wa fedha waliolishwa viongozi wa Yanga na hata kumruhusu mchezaji huyo kuondoka siku chache kabla ya kuivaa Al Ahly? Kuna soka gani ya ajabu China iliyowanyima usingizi Yanga na hata kumpeleka mmoja wa wapiganaji wake tegemeo katika vita dhidi ya Waarabu?

Mbona Ngassa alibaniwa kwenda Norway , ikidaiwa mipango ilikuwa haijaeleweka, lakini sababu nyingine ikielezwa ni nyota huyo kutakiwa kuitumikia klabu katika Ligi ya Mabingwa Afrika?

Hatuombei, lakini kama ikitokea Yanga ikachemsha kwa Al Ahly, ingawa rekodi inaonyesha siku zote ni wanyonge mbele ya Waarabu, bado viongozi wa Yanga hawatapaswa kukaa mbali sana na lawama, kwani katika madudu haya ya hivi karibuni, ni dhahiri mkono wao unaonekana katika kubomoa mshikamano.

Huu si wakati wa malumbano wala kupangua wachezaji, Yanga inapaswa kuwa kitu kimoja, dhamira ikiwa kumng’oa Ahly.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: