Madhara ya serikali ya kishikaji


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version

TUNASHUHUDIA madhara ya serikali ya kishikaji. Kila mwenye uhusiano na mteule mkuu serikalini anajitutumua kutoa ushauri wa kisheria kuhalalisha wizi wa kodi za wananchi.

Washkaji wanadai: Serikali isipowaibia wananchi Sh. 94 bilioni na kuwapa Dowans watumbue kwa raha zao, itaitia nchi kwenye matatizo makubwa.

Miongoni mwao ni Mwanasheria mkuu wa kwanza, Jaji Mark Bomani na wakili maarufu wa kujitegemea nchini, Kennedy Fungamtana. Wamepigilia misumari kwamba fidia kwa Dowans haikwepeki.

Sawa. Hivi karibuni Jaji Bomani alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Madini iliyoundwa na Rais Kikwete. Fungamtama amejitosa katika sakata hili kutetea maslahi ya mteja wake – mfanyabiashara na Mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz.

Fungamtama ni wakili anayetumiwa na Rostam katika kesi mbalimbali, ikiwemo aliyoishitaki MwanaHALISI katika mahakama kuu Dar es Salaam.

Kwa hiyo, ushauri wake ni wa kimaslahi. Ndiyo maana anapinga kusajiliwa nchini kwa hukumu ya ICC iliyoipa Dowans ushindi dhidi ya TANESCO, akidai “hakuna sababu za msingi.”

Wakati Jaji Bomani anasema serikali ikikataa kulipa Dowans inaweza kusababisha mali zake zilizoko nje kukamatwa, Fungamtama anasema serikali ikikataa kulipa itakatisha tamaa wawekezaji.

Sijui ni wawekezaji gani anaozungumzia wakili huyu maana walikuwepo wawekezaji ATC, TTCL na TRL. Waliondoka na kuyaacha hoi mashirika ya Watanzania. Walihofu hatima ya Dowans?

Je, anazungumzia wawekezaji wa TICTS na IPTL? Hivi ni nani asiyeona maumivu makali yatokanayo na mikataba ya TICTS na IPTL?

Je, anamaanisha uwekezaji katika mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira? Mwekezaji gani makini ataondoka eti kwa kuwa serikali imekataa kulipa Dowans?

Ilipoingizwa nchini kampuni ya Richmond na magazeti kumtaja Rostam, mbunge huyo alikataa, ingawa ndiye aliyekuwa mratibu. Ghafla ‘bin vuu’ Richmond ikachubua magamba na kujiita Dowans huku Rostam akibaki mratibu. Kampuni zote hizo zilitumia anwani yake.

Baada ya mkataba wa Dowans kusitishwa kutokana na kuingia kwa mguu mbaya, ikaenda ICC ambako imerudi na tuzo ya Sh. 185 bilioni au Sh. 94 bilioni.

Swali: Nani anayelipwa? Mtu yuleyule aliyekana kuwa na uhusiano na Richmond/Dowans ndiye amepewa mamlaka ya kisheria – Powers of Attorney – kukinga mabilioni hayo. Ni halali kweli?

Swali: Nani alimpa mamlaka? Hakuna anayejibu maana yeyote atakayedai alipewa na waliotajwa kuwa wamiliki wa Dowans ataumbuka; si walikataa kuijua Dowans.

Swali: Rostam alipewa mamlaka hayo lini? Nyaraka za ICC zinadai alipewa tarehe 28 Novemba, 2005. Lini? Mwaka 2005? Ni kichekesho.

Alipewa mamlaka hayo akinge fedha za wapi? Dowans iliingia nchini mwaka 2007. Ilikuwa asimamie mradi gani wa Dowans?

Kwa hiyo, wote wanaojitokeza kutetea Dowans ilipwe mabilioni ya shilingi, wanataka kuhalalisha utapeli huu. Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ameshika bango akisaidiwa na Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema ambao ni wateule wa Rais.

Hivi ni waziri gani msomi anayeshindwa kuona ufisadi huu?

Mnyukano huu wa hoja unatokea Rais akiwa ametulia. Huku anasumbuliwa na Dowans na katiba, kule amebanwa na mauaji ya Arusha na kwingineko na uchakachuaji matokeo. Amejichokea.

Wapo wanaompa nguvu, lakini wengi wanamtazama; ayumbe na kudondoka chini na Dowans.

Rais Kikwete ana kawaida ya kusingizia kuwa ukosefu wa wataalamu katika majadiliano ya mikataba ndio kiini cha serikali kuingia mikataba mibovu.

Mwaka 1994; Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa Nishati na Madini aliingiza IPTL;

Mwaka 2006; Waziri mkuu, Edward Lowassa, alipanda pipa hadi Thailand kuomba mvua. Serikali ikaacha mradi huo ikabariki Richmond/ Dowans.

Mwaka 2007; Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi aliruka na mafaili ya mgodi wa Buzwagi hadi Uingereza kutia saini hotelini, tena usiku;

Kama mawaziri walijua wao si watalaam waliruhusiwaje kuingia mikataba ya kitaalam? Mbona wale wa TANESCO waliposhauri Richmond haifai, serikali ya Kikwete iling’ang’ania?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: