Madudu ya DAWASCO na hasira za CEO


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

KAMA unafanya kazi Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani (DAWASCO), huwezi kukosa “hela ya sigara.”

Unabisha? Nenda kwa mkaguzi wa hesabu wa Dawasco au pata mtumishi wa kukufunulia mafaili ndani ya ofisi ya Ofisa Mkuu Mtendaji (CEO) au Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi.

Utakuta haya: Kupata hela ya sigara, unaweza kudai kuwa stesheni moja ya mtambo wa kusafisha na kusukuma maji kwa watumiaji, kwa mfano Ruvu Juu au Ruvu Chini au Mtoni, unatumia usafiri wa “bajaji.”

Hivyo utaandika tarehe 20 Januari 2011, bajaji imetumia mafuta ya Sh. 21,480. Utachukua fedha. Utaweka kibindoni. Utanunua sigara au mboga au bia.

Waweza kufanya hivyo pia tarehe 1 Februari 2011 na kurudia hivyo tarehe 10 mwezi huohuo; ukichota kiasi hichohicho.

Ukweli ni kwamba stesheni ya mtambo huo, ina bajaji; lakini bajaji hiyo ni mbovu hadi leo unaposoma hapa. Sasa, ama hakuna anayejua unavyochota fedha; au anajua lakini anakulinda mtindo wa ki-Dawasco.

Hebu angalia huyu anayechota Sh. 53,700 kila anapotaka “hela ya sigara.” Anadai kuwa kituo kimojawapo kinanunua mafuta ya jenereta.

Kwa tarehe zilezile za kuchota lita za mafuta ya “bajaji mfu,” naye anachota pia mafuta kwa matumizi ya “jenereta.” Lakini kituo hakijawahi kununua jenereta.

Januari inakwisha. Inakuja Februari. Inakuja Machi. Inakuja Aprili. Jamaa wanachota fedha za kununulia mafuta ya “bajaji mfu” na “jenereta” ambayo haijawahi kununuliwa.

Angalia hati za manunuzi. Siyo ya mafuta peke yake, hata bidhaa nyingine. Ama hati hazina saini kabisa; au saini iliyopo haifahamiki. Lakini fedha zinakwenda na siku inatokomea.

Uchunguzi katika taarifa ndani ya ofisi ya mkaguzi wa fedha zinaonyesha, kuna malalamiko yaliyowahi kufikishwa kwenye ofisi hiyo ili iyashughulikie.

Kwa mfano, kuna nyaraka za malipo ambazo zina jina la anayeomba bidhaa lakini hazina jina wala saini ya aliyeidhinisha malipo au anayelipwa.

Kuna nyaraka, kwa mfano, za kuwasilisha bidhaa zilizonunuliwa lakini hazina tarehe; vilevile stakabadhi isiyokuwa na tarehe.

Nyaraka nyingine ambazo MwanaHALISI imeziona mikononi mwa aliyetakiwa kujibu tuhuma dhidi yake na aliyetakiwa kuchunguza madai haya, zinaonyesha ununuzi wa spea za zaidi ya Sh. 11 milioni kwa ajili ya mtambo wa Ruvu Chini.

Spea hizo, hata hivyo, imeelezwa kwamba hazikuwa zikihitajika. Aidha, hakukuwa na ombi rasmi la kununua spea hizo; na hakuna spea hata moja iliyopelekwa kiwandani ingawa ofisa mmoja alisaini “kupokea” spea hizo.

Ofisa mmoja ndani ya ofisi ya CEO amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa anajua yote hayo na kwamba wanasubiri uchunguzi wa taratibu zote za manunuzi katika kampuni.

Kasheshe ipo kwenye manunuzi ya kinachoitwa bearings (beringi) za kufungia pampu za maji. Taarifa zilizoko mikononi mwa mmoja wa watuhumiwa (majina yanahifadhiwa kwa sasa), zinasema zilinunuliwa beringi 28 kwa Sh. 59,600,000.

Maelezo yanayotakiwa ni kwa nini beringi hizo zilinunuliwa kwa bei ya juu “kuliko kawaida;” na kwa wingi kiasi hicho.

Mtoa taarifa anasema beringi hazikuwa zikihitajika kwa kuwa hakuna zilizokuwa zimeharibika; na hakukuwa na sababu ya kuagiza beringi na pampu zote saba za mitambo.

Kinachouma zaidi ni kwamba huenda beringi hizi zisitumike, kwa kuwa baada ya miezi michache, pale kazi ya upanuzi wa mtambo itakapokuwa imeanza, mabomba yote yaliyopo sasa hayatakuwa yakitumika.

Mwandishi ameona nyaraka nyingi za Dawasco ambazo hazina majina wala saini; hazionyeshi mamlaka ya mnunuzi na hata nyingine hazionyeshi nani alipokea malipo.

Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika habari za uchunguzi zikinukuu wataalam wakieleza “hali ya maji ya Ruvu” na matumizi ya dawa za kusafishia maji ambazo hazimalizi tope lote katika maji.

0
Your rating: None Average: 4 (3 votes)