Mafisadi hawanitishi - Kilango


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 24 June 2008

Printer-friendly versionSend to friend
Anne Kilango Malecela

"SITISHIKI. Siogopi vitisho. Sikuja hapa kutumikia maslahi binafsi. Niko hapa kutetea nchi yangu na chama changu. Wanaodhani wanaweza kunirudisha nyuma kwa kutumia vitisho, hao hakika hawanifahamu."

Hiyo ni kauli ya Anne Kilango Malecela, mbunge wa Same Mashariki (CCM). Kilango, katika mahojiano ya Ana kwa Ana na MwanaHALISI, Ijumaa iliyopita, pamoja na mambo mengine, anajibu swali la kwa nini anasema "bungeni hapatatosha."

"Ni aibu hata kuzungumza jinsi fedha zile zilivyochukuliwa. Rais ametoa miezi sita kutaka hela zake. Sisi kama wabunge, hatuwezi kunyamaza. Ndiyo maana nasema, fedha hizi za EPA zisiporudishwa, pale bungeni hapatatosha,' anafafanua.

Kauli za Kilango zinatokana na yaliyokwishatokea. Katika vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wabunge, baadhi ya wajumbe walitaka CCM iwamulike wabunge machachari kama Kilango na Cristopher ole Sendeka (Simanjiro).

Wito huo ulitolewa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Zanzibar, Catherine Peter Noni. Alitaka chama kimmulike Kilango ili mwaka 2010 kisimpitishe kutetea ubunge wake.

Lakini mwenyewe anasema, "Hakuna wa kunirudisha nyuma. Sitishiki na lolote. Mimi si lele mama. Nasema, kama fedha hizi hazitarudishwa, hapa bungeni kamwe hapatatosha."

Kilango anasema hapatatosha kwa sababu wabunge hawatakubali. Wataungana na kuhakikisha kwamba wahusika wote wanarudisha fedha za wananchi.

Je, fedha zikisharudishwa ataridhika, au atataka kuchukuliwa kwa hatua nyingine zaidi? Anajibu, "Kwanza zirudi, kisha tutajadili hayo mengine. Ni vema tukaenda hatua kwa hatua."

Kuhusu wanaomsakama, Kilango anasema, "Mimi si msaliti; ni mzalendo wa kweli wa nchi yangu. Siogopi vitisho, pamoja na kwamba nimekuwa nikivipokea tangu nilipochangia mjadala wa Richmond."

Tangu wakati huo, Kilango anasema, amekuwa akipokea vitisho mbalimbali vikiwamo vile vya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms).

Kilango anasema ana imani kubwa kwamba fedha hizo zitarudi kutokana na kile alichoita, "kutakiwa na rais."

Kuhusu mgawanyiko uliolikumba Bunge na chama chake katika suala la ufisadi, Kilango anatoa wito kwa jamii kuwasamehe wale wote wanaounga mkono ufisadi.

"Kama mtu atakuwa anatupiga vita, huyo ni mtu wa kusamehe. Nataka kukuhakikishia kwamba iwapo Bunge litapiga kura, zaidi ya robo tatu ya wabunge wataunga mkono hoja ya kushughulikia mafisadi. Wengi watataka fedha zetu zirudi," anasisitiza.

Anne Kilango Malecela, alizaliwa miaka 52 iliyopita. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Jitengeni kutoka mwaka 1964 hadi 1970.

Alijiunga na shule ya Sekondari ya Weruweru mwaka 1971 ambako alimaliza mwaka 1974.

Kutoka hapo alijiunga na shule ya Sekondari ya Biashara ya Shinyanga (Shycom) kwa masomo ya kidato Tano na Sita hadi 1976.

Mwaka 1978 hadi 1979 alijiunga na Chuo cha Ualimu Chang'ombe ambapo alipata cheti cha ualimu.

Kutoka changombe alipangiwa kufundisha katika shule ya Sekondari ya Wasichana, Kisumu jijini Dar es Salaam. Alifanya kazi hiyo kutoka mwaka 1979 hadi 1983.

Mwaka 1983 aliacha kazi katika shule hiyo na kujiunga na Shirika la Ndege Tanzania (ATC). Mwaka 1991 hadi 1993 alifanyakazi katika Shirika la Ndege la Gurf la Arabuni.

Pamoja na kufanya kazi Gurf kwa mafanikio, Anne Kilango aliacha kazi mwaka 1994 na kujiumnga na Shirika la Ndege la Uholanzi – KLM.

Aliingia rasmi katika ulingo wa siasa kwaka 1997 ambapo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa CCM katika wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam .

Kilango aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2000 kupitia sanduku la Viti Maalum. Hii ni baada ya kushindwa katika kura za maoni katika jimbo la Ubungo.

Mwaka 2005 aliamua kugombea kupitia jimbo la Same Mashariki. Alishinda.

Akizungumzia kauli ya mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah, kwamba hakuna mbunge anayetishwa; kwamba baadhi ya wabunge wanazungumza sana, Kilango anatema:

"Sijui alikuwa anakusudia nini. Lakini mimi sina muda wa kubishana na mama yule. Niseme tu kwamba, kauli yake imenisikitisha."

Hivi Kilango anapata wapi nguvu na ujasiri wote huo? Je, ni kule kuolewa na mwanasiasa mkongwe nchini, John Malecela?

Anajibu, "Hapana. Malecela amenikuta hivi. Mimi ni mwanaharakati tangu zamani. Wanaonifahamu wanajua jinsi nilivyopambana katika kinyang'anyiro cha kura za maoni katika jimbo la Ubungo mwaka mwaka 2000. Alichofanya Malecela, ni kunipa baraka za kugombea ubunge katika jimbo langu la Same Mashariki."

Akizungumzia fununu kwamba baadhi ya wapinzani wao wa kisiasa wameamua kuwashughulikia kwa kuwachongea kwa wapigakura katika majimbo yao, Kilango anasema, "Kila anayetaka kugombea na aje. Mimi sina hofu na hilo."

Kilango anasema amesimamia miradi mingi jimboni kwake, ikiwemo ya ujenzi wa barabara na ujenzi wa kiwanda cha kusindika tangawizi.

Kata nane katika jimbo la Kilango linalima tangawizi kwa wingi. Hata hivyo, anasema kwa muda mrefu wakulima hao wamekuwa wanapunjwa na wafanyabiashara wa zao hilo.

Wakulima wamekuwa wakiuza tangawizi kwa Sh. 200 kwa kilo, huku wafanyabiashara wakiuza kwa Sh 1000.

Ni kutokana na hali hiyo, Kilango ameamua kushirikiana na halmasahuri ya wilaya na serikali kuu, kuandaa mipango ya kujenga kiwanda cha kusindika tangawizi katika jimbo lake.

Katika hilo anamshukuru mkuu wa wilaya, Ibrahim Marwa na mwenyekiti wa halmashauri, Agostine Kessy na mkurugenzi wa halmashauri aliyemtaja kwa jina moja la Lukumu.

Anasema ujenzi wa kiwanda hicho tayari umeanza, na kwamba ujenzi unatarajiwa kukamilika muda si mrefu. Kwa upande wa madawati, Kilango anasema hakuna tatizo kutokana na sera waliojiwekea ya kila mwanafunzi kuja na dawati lake.

Kuhusu taarifa kwamba anataka kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake na kwamba ndiyo chanzo cha yeye kupigwa vita, Kilango anasema kwamba kamwe hana mawazo ya kuwania nafasi hiyo.

Anasema, ukigombea nafasi ile na kushinda, unachopata ni uhakika wa kuwa mbunge. Maana mwenyekiti wa UWT, anakuwa mbunge moja kwa moja.

Anasema, "Mimi sitaki ubunge wa aina hiyo. Bado mimi nataka kuwa mbunge wa jimbo. Wanaonifikiria mimi, nawambia mimi simo."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: