Mafisadi wanatusingizia uhaini


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Mtazamo

WAZIRI mkuu Mizengo Pinda aliposema mafisadi ni hatari, wachambuzi wa masuala ya kisiasa walimrukia na kudai ni kauli ya kusalimu amri.

Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo aliunga pia mkono hoja ya Pinda akisema unahitajika umakini kuwashughulikia mafisadi waliokwapua fedha za EPA.

Tahadhari hiyo ilitolewa wakati linaibuka sakata zito la kampuni feki ya Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura.

Iliposomwa bungeni ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Richmond iliyojichibua na kujiita Dowans, wamiliki hawakutajwa japo walijulikana.

Jamaa hao, wamejiviringisha katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaendesha serikali kwa remote na sasa wanahaha kupindisha ukweli ionekane waliofichua ufisadi wa Richmond ndio wanaoisababishia matatizo nchi hii.

Wanaolengwa katika vita hii mpya ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na MwanaHALISI.

Kwa wasomaji wapya, kashfa ya Richmond iliibuka baada ya Kamati ya Madini na Nishati, chini ya Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo kushtukia mchakato wa kuipa zabani kampuni  isiyo na fedha, uwezo wala uzoefu. Ikapendekeza ichunguzwe.

Bunge liliafiki, likaunda kamati chini ya Mbunge wa Kyela, Dk. Mwakyembe. Kamati ikasafiri, ikakusanya taarifa zote muhimu ndani na nje; ikawasilisha ripoti bungeni.

Sitta, aliyekuwa Spika wa Bunge, kwa ujasiri aliruhusu mjadala wa wazi.

Moto wa mjadala wa ripoti hiyo ukambabua aliyekuwa Waziri mkuu, Edward Lowassa; akajiuzulu pamoja na mawaziri waliowahi kusimamia Wizara ya Madini na Nishati, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Katika hali ya kushangaza, akina Richmond, ambao hawakutajwa popote, wamevaa magwanda ya unafiki.

Wanajidai ni watetezi wa Rais Jakaya Kikwete wakati wanamsubiri mlangoni kwake awachotee Sh. 94 bilioni eti Dowans ilishinda kesi dhidi ya TANESCO. Halafu wanataka Rais Kikwete awatimue uwaziri Sitta na Dk. Mwakyembe na alifunge MwanaHALISI kwa uhaini.

Makamba

Mchezo mchafu umemshtua mwenyekiti mpya wa Kamati ya Madini na Nishati, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba. Amehoji uadilifu wa kampuni ya mawakili iliyoitetea TANESCO.

Kampuni hiyo ndiyo ilishauri kuhalalisha mkataba wa Richmond; ndiyo ilishauri mkataba kati ya serikali na Dowans uvunjwe; na ikatumika kutetea TANESCO katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).

Ikumbukwe Makamba aliwahi kuwa msaidizi wa Rais Kikwete, hivyo kuna siri anaijua.

Anajua baada ya Bunge kupendekeza watumishi wa umma wa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuiingiza nchi katika mkataba feki, serikali ilipuuza.

Ikaacha baadhi ya viongozi wakastaafu na wengine wanaendelea kazini hadi leo. Hata ilipoamua kuvunja mkataba wa Dowans ilipata ushauri wa kisheria kutoka kampuni ambayo sasa anahoji uadilifu wake.

Nguvu ya fedha

Isitoshe baada ya Kamati Teule kuwasilisha ripoti yake ilibaki kuwa ya Bunge na siyo kamati, Mwakyembe wala Sitta. Mafisadi wanajua hilo ila kwa kutumia nguvu ya fedha wanageuza ukweli.

Kamati Teule ilipokwenda Marekeni kufuatilia uhalali wa kampuni ya Richmond, ilielezwa kwamba haipo ‘kisheria’ na haikutimiza taratibu za kisheria kujisajili.

Lakini katika mazingira yanayojenga shaka hata kwa Makamba, mawakili wa TANESCO wakakubaliana na mafisadi,  mmoja wa majaji wa ICC atoke Marekani. Huyo ndiye anadai kampuni ya Richmond ipo ‘isipokuwa’ eti inatumia jina la kibiashara badala ya jina halisi.

Kwa nguvu hii ya fedha, haishangazi kwa nini wanataka MwanaHALISI lifungwe kwa uhaini wakisingizia kuwa linashirikisha na mfanyabiashara mmoja na vigogo wa CCM kuiangusha serikali ya Rais Kikwete.

Kama kutoa elimu hii kwa wananchi ni uhaini basi wa kwanza kuingia jela wawe mafisadi wanaotishia usalama wa nchi. Sisi hatutaacha kumkosoa na kumshauri Rais Kikwete na tunamtaka ajali maslahi ya taifa asiwalipe Dowans.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: