Maji ya Dawasco hatari


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

AFYA za mamilioni ya wakazi wa Dar es Salaam wanaokunywa maji ya DAWASCO ziko hatarini kutokana na ubora wa dawa za kusafishia maji kuwa wa viwango vya chini.

Ubora umo katika makundi mawili. Kwanza, uwezo wa dawa kusafisha maji kwa kiwango kinachotakiwa kitaaluma; na pili, mazingira ambamo dawa zinahifadhiwa.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Dawasco zinasema tangu Juni 2010, kumekuwa na matumizi ya mara kwa mara ya dawa za kusafishia maji ambazo hazina uwezo kamili wa kuondoa tope (turbidity).

Kwa mfano, kabla ya kuingia kwa Ofisa Mkuu Mtendaji (CEO) Bw. Jackson Midala, aina mbili za dawa zilikuwa zinatumika kusafishia maji.

Aina hizo mbili ni Algaefloc na Aquafloc (I01085) zote kutoka kampuni ya Sud-Chemie ya Afrika Kusini.

“Kwa miaka mingi sasa tumekuwa tukitumia dawa hizi ambazo zimethibitika kuwa effective (jalabati). Lakini ujio wa CEO mpya umeanzisha dawa ambazo hazina uwezo wa kuondoa kikamilifu, tope katika maji,” ameeleza mmoja wa wafanyakazi kwenye mtambo wa maji wa Mtoni.

Aina mbili za maji ambazo zimetajwa kuwa siyo nzuri kwa usafishaji maji na haziondoi tope ni Polyaluminium Cloride (PAC) na Aluminium Sulphate (ALUM). 

Wakazi wa Dar es Salaam na sehemu kubwa ya mkoa wa Pwani, wanatumia maji kutoka mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini iliyoko wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani na Mtoni ulioko wilayani Temeke.

Dawa za PAC na ALUM zinatajwa kutoondoa tope kikamilifu katika maji, wakati wadudu wengi na viini hatari katika maji huishi katika tope. 

Aidha, dawa za PAC na ALUM zimekuwa zikiletwa katika viwango vidogo na katika muda usiotabirika.

Katika hali ya kushangaza, kuna wakati madumu ya dawa hizo yalipelekwa kwenye mtambo yakiwa hayana lakiri.

Kawaida huwa kuna mfuniko wa chuma uliosilibwa kwa lakiri. Baada ya kuondoa huo, hufikia mfuniko wa kuzungusha kwa kwenda kushoto na kufungua.

Mara hii, madumu hayakuwa na mfuniko wa chuma ulioshikishwa kwa lakiri maalum na mifuniko iliyokuwapo, ilikuwa imelegea huku ikikazwa kwa msaada wa karatasi za nailoni.

“Katika mazingira haya huwezi kujua kama dawa imetumika; imewekwa maji au chochote kile kinachoweza kudhuru wanaotumia maji,” ameeleza mfanyakazi wa mtambo Ruvu Juu.

Kuna wakati mitambo ilipokea madumu ya dawa ambayo ilikuwa na rangi mbalimbali, wakati walizoea dawa zenye rangi moja.

Kwa mujibu wa wafanyakazi, kuna wakati walipelekewa dawa ya “PAC na ALUM ambayo ilikuwa na harufu inayochoma na kukereketa kooni.”

Mkaguzi mmoja wa mitambo, amemwambia mwandishi huyu kuwa dawa bora waliyozoea kutumia kabla ya kuanza matumizi ya hii ya sasa, ina sura ya mafuta ya uto na haina harufu.

Dawa zote za sasa, PAC na ALUM, wameeleza wafanyakazi, zinawasha kiasi kwamba wafanyakazi wameomba kupewa glovu za kuvaa mikononi.

Kumbukumbu zilizopatikana wizara ya maji zinasema baadhi ya maofisa na wafanyakazi waliishaona kuwa kiwango cha tope katika maji yaliyosafishwa kwa PAC na ALUM kilikuwa kinaongezeka.

Dawa ya Algaefloc ina uwezo wa kutibu maji bila usumbufu na pia katika vipimo inaonyesha matumizi madogo zaidi kuliko PAC na ALUM.

Hivi sasa kuna mvutano wa chini kwa chini wa mawazo miongoni mwa wataalam ndani ya Dawasco kuhusu uamuzi wa kuacha dawa bora - Algaefloc na Aquafloc na kuanza kutumia zile ambazo wanasema haziondoi tope.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya (WHO) linaagiza tope katika maji sharti liwe chini ya kiwango cha NTU 5 (Neutral Turbidity Unit).

Katika Tanzania kiwango kinawekwa chini ya NTU 10. Lakini kwa mujibu wa maofisa na wataalam ndani ya mitambo ya maji ya Ruvu na Mtoni, kiwango cha tope kiko juu ya hapo.

“Hili ni jambo la hatari. Basi hakuna sababu ya kuwa na dawa za kuondoa tope kama tunashindwa kufikia kiwango cha WHO na hata kiwango chetu wenyewe cha NTU 10,” anaeleza mkaguzi wa maji wa Ruvu Chini.

Amesema, “wadudu na microorganism (vimelea) nyingine zisizohitajika hukaa kwenye tope. Sasa kama tope halikuisha, hatari bado ipo palepale na fedha zinatumika bure,” ameeleza na kuomba kutotajwa jina.

Kuna magonjwa mengi ambayo yanaweza kutokana na maji kutosafishwa na iwapo pia hayakuchemshwa, kwa mfano, kuhara, kuhara damu, kipindupindu, homa ya matumbo.

Daktari mmoja jijini Dar es Salaam ameeleza kuwa siyo kila bakteria ni hatari. Amesema bacteria wengine ni rafiki wa mwili wa binadamu, lakini pale wanapobaki wanakostahili kuwa.

Amesema kwa mfano, mtoto akienda haja kubwa na kusafishwa kwa maji ambayo si salama; na maji hayo kugusa sehemu za uzazi, basi mtoto aweza kupata maambukizi katika njia ya mkojo (urinary track infection – UTI).

Uchunguzi wa MwanaHALISI umegundua kuwa dawa ambazo haziondoi tope, zilizoanza kutumika tangu ujio wa CEO mpya, bado zinatumika; bali wiki iliyopita ndipo wamepokea aina ya Algaefloc ambayo wasimamizi wa shifti wanalilia.

Nani ananufaika kwa bei kubwa za dawa?

DAWA za Polyaluminium Chloride (PAC) na Aluminium Sulphate (ALUM) ambazo zinadaiwa kutokuwa imara katika kusafisha maji, ni ghali kuliko za awali ambazo zina uwezo mkubwa wa kutoa tope kwenye maji.

Utafiti wa MwanaHALISI umegundua kuwa dawa ya PAC ambayo haiondoi kabisa matope inazidi dawa bora kwa bei kwa asilimia 120.

Hoja ni kwa nini wahusika wameamua kutumia dawa isiyo bora na ambayo inagharimu kiasi kikubwa cha fedha kuliko dawa bora.

Taarifa zilizopatikana ofisi ya CEO zimeeleza kuwa lita 2,200 za maji ambayo hayajasafishwa huweza kutumia kiasi cha dawa ya Algaefloc ya kusafishia cha kilo 2,661.12 (au madumu 11.09) kwa siku.

Gharama ya kilo moja ya dawa Algaefloc ni Sh. 2,574. Kwa hiyo, kilo 2,661.12 x Sh. 2,574 = Sh. 6,849,723. Lakini dawa isiyo jalabati (isiyoweza kutibu maji kihalisi), inauzwa kwa gharama ya juu.

Kwa mfano, kwa vipimo vilevile vya maji lita 2,200, kiasi cha dawa ni kilo 9,504.00 (au madumu 38.02) kwa siku. Gharama ya kilo moja ni Sh. 1,600.

Kwa hiyo, kilo 9,504 x Sh. 1,600 ni sawa na Sh. 15,206,400. Hii ni zaidi ya asilimia 120 ya bei ya dawa ambayo imethibitisha ubora, zimeeleza ripoti zilizopatikana ofisi ya CEO.

Katika mazingira ya kununua dawa za kulinda afya na uhai wa jamii, “…kwa nini dawa hafifu inunuliwe kwa bei ya juu, wakati kuna dawa bora iliyothibitika na yenye bei nzuri?” anauliza ofisa mmoja wa mtambo wa Ruvu Juu.

Tayari kuna mgogoro unatokota miongoni mwa viongozi na wafanyakazi wa Dawasco juu ya uamuzi unaodaiwa kupuuza afya za wakazi wa Dar es Salaam, wakiwemo wapangaji wa ikulu – rais na familia yake.

Taratibu za ununuzi ‘kitedandawili’

UCHUNGUZI wa MwanaHALISI umegundua kuwa hadi Juni 2010, dawa za kutibu maji kwenye mitambo mitatu, zilikuwa zikinunuliwa kutoka kampuni ya Sud-Chemie ya Afrika Kusini kupitia wakala wake, Procell Company ya Dar es Salaam.

Hivi sasa yanatajwa makampuni mawili ya Mukapar (T) Limited na JUNACO (T) Limited yote ya Dar es Salaam. Wasemaji wa makampuni haya hawakupatikana kwa simu kueleza jinsi wanavyosambaza dawa za kufua maji.

Bali kama ununuzi ungefanywa kwa misingi na kanuni za manunuzi – kuanzia ngazi ya mhitaji, mtoa tenda na mwendesha tenda, mtiririko wa upatikanaji dawa ungekuwa tofauti.

 • Kusingekuwa na kubabaika juu ya dawa ipi inahitajika. Maamuzi yangekuwa yamefanywa mara moja.
 • Kusingekuwa na maamuzi ya kununua aina ya dawa isiyokuwa jarabati kwa fedha nyingi, badala ya kununua dawa inayofaa, tena kwa bei nafuu.
 • Kusingekuwa na ununuzi wa viwango vidogo mara kwa mara na wafanyakazi na mameneja wao kukaa roho juu wakisubiri, dawa italetwa au haitaletwa.
 • Kusingekuwa na gharama za nyongeza za kufuata dawa mitaani na kuzisomba kwa magari ya Dawaso; hivyo kuongeza gharama za dawa ambayo tayari ni ghali. Mwenye tenda angezifikisha kwenye mtambo.
 • Kusingekuwa na ununuzi wa dawa zisizo za viwango – zenye harufu kali inayochoma na zinazowasha.
 • Kusingekuwa na ununuzi wa dawa ambazo hazina lakiri – hazikufungwa kwa mujibu wa ufungaji kitaaluma ili kulinda usafi wa dawa na afya na uhai wa jamii.

Vikao baada ya vikao

WAKATI kila ofisa anakimbia kutoa majibu, kuna taarifa kuwa tayari vikao vimeanza kujadili suala la dawa bora na dawa dhaifu.

“Maji ni security issue (ni suala la kiusalama). Wakuu wa Dawasco hawawezi kupuuza hili,” amesema ofisa mmoja wa kituo cha Boko, wilayani Kinondoni.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, kamati maalum ya Dawasco iliyoundwa mwaka jana kwa shughuli tofauti, imepewa jukumu la kuchunguza “suala la usalama wa maji.”

Katika kikao chake cha 3 Aprili, kamati iliwahoji Mkuu wa Idara ya Utawala, Meneja Ruvu Juu, Meneja Ruvu Chini na dereva wa CEO.

Taarifa kutoka ndani ya kikao ambacho kilikuwa kinaendelea hata kesho yake, katika hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam, zinasema mahojiano yalikuwa juu ya ubora wa dawa na usalama wa maji.

Taarifa nyingine zinasema mwishoni mwa wiki iliyopita, kulikuwa na kikao cha bodi ya wakurugenzi kujadili dawa za maji na usalama wake. Hakuna taarifa zaidi zilizopatikana juu ya kikao hicho.

Hata hivyo, dereva atakuwa alihojiwa juu ya gari  GX SU 37238 ambalo alipata nalo ajali akiwa amembeba CEO na Ofisa Utawala na Fedha, Esther Idabu walipokuwa wakitoka Arusha kurudi Dar es Salaam.

Gari hilo liliharibika kiasi cha kutoweza kutengenezeka. Inadaiwa safari ilikuwa ya binafsi – kati ya maofisa hao wawili.

Wasemavyo wakubwa wa Dawasco

Ofisa Mkuu Mtendaji (CEO)
Jackson Midala

Swali: MwanaHALISI ina taarifa kuwa dawa mnazotumia kusafisha maji siyo bora; kwa hiyo haziondoi tope lote ambalo wadudu hukaa. Hizi taarifa unazifahamu?

Jibu: Huyo aliyekupa taarifa ana uhakika nazo?

Swali: Sisi tunatafuta uhakika kwako, mhusika mkuu.

Jibu:Kwa taarifa na takwimu nilizonazo, maji yanayozalishwa mitamboni ni safi na salama, na yapo katika viwango vinavyokubalika kimataifa.

Meneja, Mtambo wa Ruvu Juu
Khalfan Keha

Swali: Tuna taarifa kwamba dawa mnazotumia kusafisha maji hazina nguvu ya kuondoa tope lote. Ina maana haya maji tunayokunywa kutoka Dawasco hayana usalama. Hili unalifahamu hapo Ruvu Juu?

Jibu:Maji hayana tatizo lolote. Ni safi na salama. Na ninyi njooni mtembelee huku muone tunavyofanya kazi. Dawa tunazotumia…ni nzuri hazina tatizo lolote.

Meneja, Mtambo wa Ruvu Chini
Joseph Bamwenzaki

Swali: Wewe ni meneja wa Ruvu Chini. Kuna taarifa kuwa mtambo wako na ile ya Ruvu Juu na Mtoni, inatumia dawa ghali kusafisha maji; lakini dawa hizo hazimalizi tope lote. Hili linakukabili hap kwako?

Jibu: Linapokuja suala la kutoa maelezo kuhusu uzalishaji na mambo ya mitambo, linakuwa jukumu la CEO kuzungumzia. Mimi siwezi kuzungumzia hilo mpaka nipewe kibali na CEO.

Meneja, Mtambo wa Mtoni
Mohammed Masudi

Swali: Miongoni mwa dawa mnazotumia kusafishia maji, kuna ambazo hazina uwezo wa kuondoa tope lote na ni ghali kuliko zile ambazo ni bora. Hilo limewakuta Mtoni?

Jibu: Siwezi kusema lolote. Msemaji mkuu ni mtendaji mkuu (CEO). Sasa itabidi uombe kibali kwa bosi wangu. Akiniruhusu nitaweza kutoa maelezo.

Swali: Lakini kuna hili lisilohusiana na kibali: Tunaweza kusema hali ni nzuri; hakuna tatizo?

Jibu: Hakuna tatizo. Nimekuwa hapa kwa zaidi ya miaka mitano. Sijaona tatizo.

Swali: Je, kuna haja ya kubadili dawa mara kwa mara, badala ya kuwa na dawa moja kwa kipindi kirefu?

Jibu: Ndiyo. Dawa zinabadilika kufuatana na maji yalivyo. Maji siyo constant. Yale ya Machi mwaka huu siyo ya sasa au yatakavyokuwa mwezi wa sita au wa saba. Sharti kuwepo dawa tofauti kulingana na msimu.

Meneja wa Ubora wa Maji
Emmanuel Makusa

Swali: Kuna taarifa kuhusu dawa zinazotumika sasa kusafisha maji ya Ruvu kuwa hazina uwezo wa kuondoa tope lote. Hili unalifahamu?

Jibu: Hili ndio nalisikia kutoka kwako.

Swali: Wewe ndiye mkuu wa ubora wa maji.

Jibu: Sasa naendesha gari. Naomba unipigie baada ya nususaa; au huwezi kufika ofisini kesho…? Basi nipigie baada ya nususaa kutoka sasa (Alipopigiwa simu hakupatikana).

Hata hivyo, ofisa mwandamizi katika Dawasco amekiri kuondolewa kwa “aina fulani” za dawa baada ya kubainika kuwa hazina uwezo wa kuondoa tope.

Ofisa huyo aliyeomba kutotajwa jina gazetini, amesema dawa hizo, PAC na ALUM zilianza kutumika Juni mwaka 2010.

Amesema, “…sasa tumeamua kurudisha zile za zamani ambazo tunaita jina la utani la silaha za maangamizi. Ilikuwa lazima tutumie zile za awali aina ya Algaefloc na Aquafloc kwa sababu hizi mpya zilishindwa.”

Ofisa amesema hata hivyo, kuwa viongozi wao wamesema “…maji yakipungua, tutakuwa tunatumia na hizi za PAC na ALUM kwa sababu ziko stoo.”

Mwenyekiti Bodi, Dawasco
Suleiman S. Suleiman

Swali: Ni kuhusu suala la dawa zinazotumiwa na Dawasco kusafisha maji kwenye mitambo yake mitatu. Uliahidi kukutana nami leo, Jumatatu. Nimesubiri ofisini kwako bila mafanikio. Nielekeze (sms).

Jibu: Kuna ndege ya ATCL ime-crash (imepata ajali) Kigoma. Nipo bize kidogo kufuatilia. Mpate Bwana Midala, CEO atakupatia taarifa husika. Samahani sana.”

Pamoja na maelezo haya ya viongozi wa Dawasco, MwanaHALISI limepata taarifa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) nayo ilichukua sampuli ya maji ili kuona kinacholalamikiwa.

Mmoja wa wakurugenzi wa EWURA, Mutahekulwa C. Mutegeki, amekiri mamlaka yake kuchukua sampuli, lakini akasema wao hawana maabara; isipokuwa maji yalipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kwamba hawajapata majibu.

Taarifa zaidi zinasema hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilichukua sampuli. Ofisa uhusiano Rhoida Andusamile amesema tayari imefanyiwa kazi na majibu yangetangazwa jana, Jumanne.

Vyanzo vya maji ya Dar

MITAMBO mitatu ina jukumu la kusafisha na kusukuma maji safi na salama katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake.

 • Ruvu Chini: Mtambo unazalisha lita 180 milioni kwa siku. Hii ni sawa na asilimia 72 ya maji yanayosukumwa Dar es Salaam.
 • Ruvu Juu (Mtambo uko Mlandizi). Unazalisha lita 90 milioni kwa siku.
 • Mtoni: Mtambo huu huzalisha lita 7 milioni kwa siku.
 • Dar es Salaam inakunywa lita 80 milioni kwa siku
 • Kwa saa moja, Dar es Salaam inakunywa kiasi cha lita 7.5 milioni.
 • Mtambo wa Ruvu Chini uko kwenye upanuzi chini ya mradi wa Millenium Challenge (MCC) ambapo, baada ya miaka mitatu, utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 270 milioni.

 

Mkuu maabara azungumza

MKURUGENZI wa Maabara katika Wizara ya Maji, Nadhifa Sadick Kemikimba, anahojiana na mwandishi Alfred Lucas.

Swali: Kuna taarifa kuwa maji kutoka vyanzo vya Ruvu Juu, Ruvu Chini na Mtoni ni hatari. Unalifahamu hili?

Jibu: Wewe amekuambia nani?

Swali: Watumiaji na wataalam.

Jibu: Hali hiyo ilitokea zamani. Lakini wanaoweza kuzungumzia hilo kwa ufasaha ni Dawasco.

Swali: Lakini ninyi wataalamu wa wizara; idara ya maabara, mlichukua hatua gani.

Jibu: Technically (kiufundi), na kwa kuwa sisi wizara ndio tunasimamia masuala yote ya maji, tuliamua kuchukua sampuli ya maji hayo kujua kama kuna tatizo.

Swali: Nini kiliwasukuma kuchukua sampuli?

Jibu: Ni hizo taarifa za uchafu wa maji; tena sisi tuliambiwa kabisa kwamba maji yana sumu.

Swali: Sasa mligundua nini?

Jibu: Hatukuona dosari yoyote. Naomba uwaone Dawasco  wanaweza kulielezea vema hili.

Swali: Kuna kitu kinaitwa halogen; wanasema ni kompaundi inayojitokeza pale dawa ya kusafisha maji inapozidiwa nguvu na tope lililosalia majini. Je, hili unalifahamu?

Jibu: Nafahamu, lakini maelezo yake ni marefu sana. Siwezi kueleza sasa hivi maana nina kikao kingine.

Kauli ya mkurugenzi inakiri kuwepo taarifa za dawa kutokuwa salama.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)