Majina kuleta utata Unguja, Pemba


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

MAJINA kufanana Zanzibar ni jambo la kawaida. Kwa mfano, unaweza kukuta Mohammed Khalid Bakari wa Pemba na mwingine mwenye majina hayohayo, Unguja.

Au majina kama Khamis Ali Bakari; Ali Bakari Khamis; Haji Issa Yusuf; Yusuf Haji Issa au Issa Haji Issa yako Pemba na yako Unguja.

Pia majina kama Abdulla Abdalla Hassan; Mussa Nassor Mussa; Hassan Hamad Hamid yanatumiwa na watu kadhaa Unguja na Pemba.

Imebainika majina kama hayo, ndiyo yamejaa katika orodha ya watu waliokuwa abiria katika meli ya m.v. Spice Islander I iliyopata ajali tarehe 10 Septemba 2011.

Meli hii kiufundi, ina uwezo wa  kubeba abiria 645. Lakini kuna taarifa mbili zinatofautiana kuhusu waliokuwa melini.

Taarifa ya serikali inaonyesha watu 941 waliokolewa na abiria 203 walikufa, kati yao maiti 159 zilitambuliwa. Lakini taarifa ya Tume Maalum inaonyesha kulikuwa na abiria 2,470 na kwamba watu 1,370 hawajulikani waliko.

Katika mazingira haya, hasa katikati ya utata wa majina, utakuta kuna majina kwenye orodha ya serikali lakini hayamo katika orodha ya tume; vilevile kuna majina kwenye orodha ya tume lakini hayamo kwenye orodha ya serikali.

Lakini kinachoongeza utata na ambacho kinaweza kusumbua wanaoendelea kutafuti nani alikufa na nani alisalimika, ni baadhi ya majina kujirudia.

Wakati baadhi ya wananchi wanasema kwa uthabiti kwamba idadi ya abiria ilizidi 2,000, ofisa mmoja wa ngazi za juu katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais anahoji, “Je, walikaa wapi? Walikaa vipi na mizigo?”

Kutoonekana au kufichwa kwa orodha ya wasafiri, kutaendelea kuwa kikwazo katika kupata idadi kamili ya abiria katika meli iliyozama.

Kwa hiyo, kile ambacho serikali itaweza kufanya, ni kupitia orodha ya majina yaliyopatikana kutoka orodha mbili, kuona kama majina yanajirudia na kama kujirudia huko ndiko kumekuza idadi ya waliokuwa kwenye meli.

Hapa kutakuwa na kazi ya nyongeza. Hata kama jina moja limeonekana mara mbili, tatu, tano au kumi, haitakuwa sahihi kudai kuwa muhusika aliandikwa mara nyingi.

Itabidi kutafuta makazi ya kila aliyetajwa na hata kufika kila kaya au mtaa kuthibitisha hivyo, kwa kuwa, kama ilivyoonyeshwa kufanana kwa majina, bado kuna uwezekano wa watu watatu hata kumi,wenye majina yanayofanana, kuwa katika eneo moja.

Mfumo wa kwenda nyumba hadi nyumba, kama ofisa wa serikali anavyopendekeza, ili wahakiki waambiwe – katika kila kaya – nani walikufa, nani walipona na nani walipotea – waweza pia kuleta utata na hata mfarakano kisiasa.

Je, kwa mujibu wa utamaduni wa siasa za Zanzibar, sheha wa CCM anaweza kutaka jina la abiria mfuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) na kusiwe na mzozo? Au wafuasi wa vyama hivi wanaweza kutoa ushirikiano wa dhati kupata ukweli? Itahitajika busara kuu.

Spice Islander I  iliyosababisha msiba mkubwa nchini, ilitengenezwa mwaka 1967, Ugiriki na ikapewa jina la Marianna ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 645. Baadaye ilinunuliwa na Theologos P. Naftiliaki wa Piraeus, Ugiriki.

Mwaka 1988, Marianna ikauzwa kwa kampuni ya Apostolos Shipping na ikapewa jina la Apostolos P.  Meli hiyo iliuzwa kwa kampuni ya Saronikos Ferries na ikawa inafanya kazi kati ya bandari za Piraeus, Aegina na Angistri, Ugiriki.

Mwaka 2005, Apostolos P ikasajiliwa na kampuni ya Hellenic Seaways na mwaka 2007 ikauzwa kwa kampuni ya Honduras na kupewa jina la Spice Islander I.

Tarehe 25 Septemba 2007, Spice Islander I ilipofika mwambao wa Somalia, wakati huo ikitokea Oman kuelekea Tanzania, injini zake zilipata matatizo baada ya kuwekewa mafuta machafu. Kikosi kazi cha watu 150 kutoka meli ya USS Stout na Kenya, kilitumwa kuiokoa.

Baada ya kuwekwa mafuta mengine na injini kuwashwa upya, meli hiyo ikaanza safari zake kuelekea kwa mmiliki mpya wa visiwani Zanzibar.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)