Makamba kumsifia Lipumba ni uchuro


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

UKIMUONA Yusuph Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anasifia mwanasiasa mwenzake, ama chombo cha habari au mwandishi wa habari binafsi, basi jua hapo kuna jambo.

Si kawaida ya Makamba kusifia yule aliyepo nje ya mkondo wake. Vinginevyo, atakuwa ameagizwa na wale anaowatumikia.

Ni nadra sana kwa Makamba kusifia hata mwanachama wa chama chake anayejitolea kukirejesha kwenye mstari.

Anachoweza kuambulia mwanachama wa aina hiyo, ni shutuma, lawama, vitisho na mizengwe. Anaweza hata kuzushiwa mambo ambayo hayamhusu.

Lakini juzi, Makamba amemwagia sifa mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.

Amesema, “Profesa Lipumba ndiye mgombea urais tishio kwa CCM na mgombea wake, Rais Jakaya Kikwete.”

Kwamba chama chake hakina hofu na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, bali kina hofu na Lipumba.

Sasa swali ni hili: Makamba amelenga nini? Jibu liko wazi: Anataka kumjengea matumaini Profesa Lipumba kuwa anakubalika na hivyo asikubali kumuunga mkono Dk. Slaa katika kinyang’anyiro cha urais kijacho.

Mradi huu ukikamilika, Makamba atakuja na sura yake halisi. Atasema, tena bila kutafuna maneno, kwamba “Wapinzani ni waroho wa madaraka.” Hapa atalenga CUF.

Atasema pamoja na Profesa Lipumba kushindwa mara tatu, bado ameng’ang’ania kugombea. Makamba atafika mbali zaidi.

Atasema, ndiyo maana CUF wamekubali kushirikiana na chama chenye sera tofauti, malengo tofauti na mtazamamo tofauti – CCM – visiwani Zanzibar, lakini wamekataa kushirikiana na wapinzani wenzao Tanzania Bara.

Makamba atasema hawa ndiyo walioteseka pamoja. Waliokamatwa pamoja na kuumia pamoja kwa miaka yote hii tangu vyama vingi virejeshwe na waliounda upinzani wa pamoja bungeni. Lakini kwa ubinafsi, ameamua kugombea.

Huo ndio msingi wa sifa ambazo Makamba anamshushia Lipumba. Ndiyo maana baadhi yetu tunajiuliza: Tangu lini CUF na hasa Bara, ikaheshimiwa na Makamba? Hata kwa maendeleo ya visiwani, Makamba atakuwa ameburutwa tu.

Ni lini Makamba ameanza kubadilika na kusifia watu makini, wanaopambana na ufisadi na waliotayari kulikomboa taifa?

Mbona ni Makamba huyuhuyu na chama chake, waliovumilia usambazaji taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari, kwamba Profesa Lipumba na chama chake, “ni wadini?”

Ni Makamba na chama chake, wakisaidiwa na aliyekuwa mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP), Omari Mahita, walioonyesha kile walichoita, “majambia ya CUF” – picha za visu zenye rangi ya chama hicho, tena siku moja kabla ya siku ya uchaguzi?

Si Makamba, CCM na serikali yao walioachia usambazaji vitaarifa kwamba “CUF ni chama cha kidini; kilichosheni vurugu na kilicholenga kuvuruga amani na utulivu?”

Je, si Mahita, mkuu wa polisi wa serikali ya CCM aliyetangaza kuwa “Visu hivyo vimeingizwa nchini na CUF kwa kazi maalum ya kuua watu?”

Kama madai ya Mahita yalikuwa ya kweli, mbona hadi leo hii, miaka mitano baada ya kutoa taarifa ile, hakuna aliyekamatwa?

Kama kila “jambia” lenye rangi nyeupe na bluu ni la CUF, mbona Mahita na wenzake hawajasema “majambia” yaliyojaa madukani na ambayo yana rangi ya njano na kijani ni mali ya CCM?

Makamba amebadilika lini hadi kuaminika? Si Makamba huyuhuyu 16 Septemba mwaka jana, aliyetinga jimboni Urambo na kummwagia sifa Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, kwamba “CCM ipo pamoja naye katika kutekeleza majukumu yake?”

Alisema, “Sitta ni muelewa; na anachokifanya ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama chake.”

Alifika hadi nyumbani kwa mama mzazi wa Sitta na kulalamika, kwamba kuna “watu wananigombanisha na Sitta.” Alizungumza mengi.

Lakini ni Makamba aliyesimama kidete ndani ya vikao vya CCM mjini Dodoma kutuhumu Sitta kuwa “anadhoofisha chama; amejenga mtandao nje ya chama” na hivyo akataka afukuzwe uwanachama.

Kinachompata Sitta leo, ni matunda ya undumila kuwli wa Makamba.

Ni Makamba huyuhuyu aliyeshiriki kuangamiza kisiasa, Nape Nnauye ambaye alisimama imara kupinga ubadhilifu katika mradi wa kitapeli wa uwekezaji wa kitegauchumi cha Umoja wa Vijana wa chama chake, UV-CCM.

Nape alitaka chama chake kinufaike na mradi huo, badala ya kikundi kidogo cha watu.

Awali Makamba alimmwagia sifa Nape, akisema amekisaidia chama kujisafisha. Lakini siku chache baadaye, akaibuka na kumtuhumu “kuangamiza chama na kushambulia viongozi wastaafu.”

Makamba alikuwa akimtetea Edward Lowassa, mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya UV-CCM.

Kama hiyo haitoshi, ni Makamba aliyesimamia kufukuzwa kwa Nape uanachama wa UV-CCM. Tabia na matendo ya Makamba bado vinamwandama Nape hadi sasa.

Makamba anafahamu kuwa CUF ya mwaka 2000 ni tofauti na ya sasa. Wala Lipumba wa 2000 na 2005, ni tofauti na huyu wa 2010.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, CUF iliungana na CHADEMA. Ni hapo kiliposhinda ubunge katika majimbo ya Bukoba Mjini na Kigamboni.

Lakini katika uchaguzi wa mwaka 2005, CUF ilisimama pekee yake. Hapa ilishindwa kupata jimbo hata moja Tanzania Bara. Si hivyo tu, ilishindwa hata kutetea majimbo yake ya Bukoba na Kigamboni.

Kingine kinachotofautisha CUF ya mwaka huu na ile iliyopita ni kwamba hii ya sasa imekimbiwa na makada wake wengi.

Miongoni mwao ni hao ambao Makamba amewapa kazi – Tabwe Hiza, Shaibu Akwilombe, Hamisi Katuga, Mohamed Shamte na wengineo.

Hata Wilifred Lwakatare, aliyekuwa naibu katibu mkuu, mbunge wa Bukoba Mjini na kiongozi wa upinzani bungeni, hayuko tena ndani ya CUF.

Inawezekana CUF imejijenga upya kwa kupata wanachama wapya, wenye uwezo na ushawishi.

Lakini kule kuondoka kwa Lwakatare ndani ya chama, kumekidhoofisha kwa kiwango kikubwa CUF na Lipumba mwenyewe.

Kura zaidi ya 400,000 ambazo Profesa Lipumba alizivuna katika mkoa wa Kagera kutokana na ushawishi wa Lwakatare, hawezi kuzipata tena katika uchaguzi huu.

Angalau kuwapo kwa Lwakatare kulisaidia kujibu hoja za udini zilizoibuliwa na Makamba na wenzake. Kuliweza kuonyesha kuwa hiki si chama cha Visiwani pekee. Ni chama cha kitaifa.

Hivyo basi, katika mazingira haya, Profesa Lipumba ana nafasi ya kudhihirisha usomi wake na ukomavu.

Bali kwa waliokaa karibu na Lipumba, kama mimi, tunajua kwamba hawezi kukubali kuvishwa kilemba cha ukoka na Makamba.

Lipumba atatafakari kwa makini sifa za Makamba zimelenga nini na zinatoa ujumbe gani. Lipumba hawezi kujiangamiza yeye na chama chake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: