Makani atakumbukwa kwa ujasiri


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
Tanzia

MWASISI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bob Muhammad Nyanga Makani amefariki dunia na anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Shinyanga.

Makani alifariki dunia Jumamosi saa 4.15 usiku kwenye hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikopelekwa haraka kwa ajili ya matibabu baada ya kuzidiwa ghafla nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam, viongozi maarufu wakiwemo Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali, watu maarufu kama Salim Ahmed Salim, Reginald Mengi; viongozi wa CHADEMA kama mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu mkuu, Dk. Wilbrod Slaa walifika juzi kwenye viwanja vya Karimjee kuuaga mwili wa Bob Makani.

Hapo hotuba za vyama vya siasa zilizomwa na wasifu wake ulisomwa. Makani amefariki huku akiacha chama alichoasisi kikiwa na nguvu na kukitikisa chama tawala katika nyanja mbalimbali.

Makani amefariki lakini atakumbukwa kwa mengi, hasa ujasiri wake wa kuingia katika siasa za upinzani huku bado akiwa mtumishi wa umma. Wakati chama hicho kinaasisiwa mwaka 1991, Makani alikuwa naibu gavana wa Benki Kuu (BoT).

Historia inaonyesha, akiwa bado BoT alishirikiana kuasisi chama hicho na watu wengine kama Edwin Mtei (Arusha - mwenyekiti), Brown Ngwililupi (makamu mwenyekiti - Iringa) na Edward Barongo (Kagera).

Wengine ni Costa Shinganya (Kigoma), Evarist Maembe (Morogoro), Mary Kabigi (Mbeya), Menrald Mutungi (Kagera) na Victor Kimesela (Manyara).

Kwa kutambua uwezo na vipaji vya uhamasiahaji na uongozi alivyokuwa navyo, katika kikao cha mkutano mkuu wa kwanza wa CHADEMA Desemba 1991, Bob Makani alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa kwanza wa CHADEMA hata kabla serikali haijarejesha kisheria mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Bob Makani alishikilia nafasi hiyo hadi mwaka 1998 alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wake hadi mwaka 2004.

Katika kipindi chote, chama kilifaidi mengi kutokana na utumishi uliotukuka wa Bob Makani. Chama kilifaidika na utaalam wake wa sheria ambao pamoja na busara zake zilikisaidia chama kutengeneza katiba na taratibu za uongozi.

Bob Makani alikuwa mtu wa watu. Ingawa ameshika vyeo vikubwa ndani ya serikali, alikuwa na kipaji cha kuwaelewa wananchi na kuungana nao katika kutafuta ubora wa maisha kwa ujumla.

Bob Makani alipewa kazi maalum ya kukipeleka chama mikoa ya Morogoro, Kigoma, Tabora, Singida, Mwanza na Rukwa. Kwa kuwa wakati huo, kuanzisha chama kipya ilionekana kama uasi au uhaini, kwenye mikutano mingi ya hadhara katikae mikoa hiyo, alipokewa kwa matusi na mara nyingine na mawe.

Aidha, kwa kuzingatia kuwa chama hakikuwa na ruzuku, alitumia rasilimali zake bila uchoyo ili kukijenga kile alichokiamini kuwa ni chombo cha ukombozi wa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Pamoja na umaarufu mkubwa aliopata katika siasa, kila alipogombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini mara tatu mwaka 1995, 2000 na 2005 kura hazikutosha.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetumia msiba wa Bob Makani kama uwanja wa siasa. Katika salamu za rambirambi, Katibu mkuu wa CCM, Wilson Mukama alisema Makani alikuwa mtu shupavu, katibu mkuu asiyependa kuongea wala kuhubiri “kama mke aliyepoteza mume” au “familia iliyopoteza baba.”

Alidai Makani alikuwa mwadilifu ikilinganishwa na viongozi wa sasa wa CHADEMA na akaongeza kwamba kati ya viongozi tisa walioasisi chama hicho yeye pekee ndiye ndiye aliyekuwa katibu mkuu wa kwanza aliyetoka nje ya kanda ya kaskazini.

Mbowe alisimama na kueleza waasisi wa CHADEMA na mikoa yao akiwemo Steven Wassira.

Lakini Rais Kikwete alisema anasikitishwa na msiba huo na alimtaja Makani kuwa mtu muhimu na aliyetoa mchango mkubwa katika katika kukuza uchumi wa nchi hii.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba alisema, “CHADEMA inatakiwa kuiga mfano wa Makani kwa kuwa hakuwa mdini, mkabila wala chembechembe za kibaguzi.”

Dk. Slaa alisema chama chao kilifaidika na utawala wa sheria na aina ya uongozi wa Makani kutokana ujuzi wake wa masuala ya sheria.

Naibu Gavana, Natu Mwamba akituma salamu kwa niaba ya BoT, alisema kwamba japo Makani hakuwa kazini, lakini walikuwa wakipata msaada mkubwa wa ushauri katika kazi hiyo.

Makani akiwa Naibu Gavana wa BoT wa kwanza alipatwa misukosuko mwaka 1989 benki ilipoungua moto lakini, alihakikisha inarejea katika oparesheni zake.

Bob Makani alizaliwa mwaka 1936 Shinyanga akiwa mmoja wa watoto wa familia ya Chifu Nyanga Makani.

Alisoma katika shule ya msingi Ibadakuli, Shinyanga na alipofaulu, alipelekwa Shule ya Sekondari ya Tabora.

Makani alipata shahada ya kwanza katika uchumi (BA Economics) katika Chuo Kikuu Cha Makerere, Uganda ambako. Baadaye alijiunga Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza ambako alitunukiwa shahada ya sheria (LLB) mwaka 1965.

Aliporudi nchini aliajiriwa kama mwanasheria wa serikali kwa muda mfupi kabla hajapandishwa cheo na kuwa mwangalizi wa mahesabu ya BoT.

Huko ndiko alianza kuwa karibu na Mtei aliyekuwa gavana wa BoT wakati huo.  Ndiyo maana haikuwa ajabu lilipoanza vuguvugu la siasa za mabadiliko nchini Makani na Mtei walikuwa pamoja hadi wakaasisi CHADEMA.

Bob Makani aliwahi kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege Tanzania,  mkurugenzi wa Bodi ya Williamson Diamonds, na mkurugenzi Bodi ya Tanzania Breweries.

Vilevile aliwahi kuwa mkurugenzi Bodi ya Benki ya Taifa ya Biashara na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Law Society.

Afya ya Makni ilianza kutetereka mwaka 2009, alikuwa akisumbuliwa na uogonjwa wa moyo. Mwaka uliofuata alipelekwa India kwa matibabu na alipata nafuu kwa muda.

Mwaka 2010 siku CHADEMA walipozindua kampeni za uchaguzi mkuu kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, Makani alikuwa kwenye meza kuu.

Ilipofika zamu ya kutambulishwa na kupewa fursa azungumze na wananchi, alisimama, akasogelea kipaza sauti, lakini alishindwa kuzungumza akatetemeka na kuanguka. Alishikiliwa akarejea kwenye kiti.

Hali ilipotengemaa alipewa fursa tena, akatoa salamu na kuwatakia wapambanaji ushindi. Januari 17 mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa CHADEMA Regia Mtema, Makani alianguka muda mfupi baada ya kuuaga mwili wa marehemu.

Baada ya tukio hilo, alibebwa na kupelekwa pembeni ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha akarejea katika hali yake ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake.

Mapema mwaka huu Makani alipelekwa Nairobi, Kenya kwa upasuaji mdogo lakini baada ya hapo hakuweza kuendelea na kazi.

Marehemu ameacha wajane, watoto saba na wajukuu wanane. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Bob Nyanga Makani.

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: