Makinda anawabeba waliombeba


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Mtazamo
Spika wa Bunge, Anne Makinda

MWAKA 1995 wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walipata fursa ya kumuuliza Mwalimu Julius Nyerere maswali mengi kuhusu uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Mhariri mmoja alimuuliza Nyerere kama ilikuwa sahihi kwa mgombea urais kujiachia kubebwa na watu katika mikutano yake. Mgombea huyo hakutajwa jina, lakini alimlenga Augustine Mrema alipogombea kupitia NCCR-Mageuzi.

Mwalimu Nyerere alijibu, “Kama mtu anataka kubebwa kama maiti mwache abebwe”. Wahariri wakacheka ila mchoraji maarufu wa katuni Masoud Ali ‘Kipanya’ alichekelea zaidi.

Katuni iliyofuata katika gazeti la Majira, ilimwonyesha Mwalimu Nyerere amembeba, mgombea urais kupitia CCM, Benjamin Mkapa, huku akisema kama mtu anataka kubebwa kama maiti mwache abebwe. Kando Kipanya kilikuwa kinasema “Mwalimu mwache mtoto atembee mwenyewe”.

Japokuwa ni kweli Mrema alikuwa anabebwa na watu na gari lake likisukumwa katika kila mkutano, Kipanya alitaka kuonyesha uamuzi wa Nyerere kumpigia debe Mkapa ulikuwa wa kumbeba kutokana na ushawishi wake.

Dhana hiyo ndiyo ninayopata kwa mwanasiasa wa siku nyingi Spika Anne Makinda ambaye analipa fadhila kwa waliombeba – CCM.

Spika wa zamani Samweli Sitta na Andrew Chenge ndio waliomba nafasi hiyo. Lakini katika mazingira tatanishi, tena dakika za mwisho, wenye CCM wakadai wanataka spika mwanamke. Anne Makinda akapaishwa kiaina na akasubiri wingi wa kura za CCM bungeni; ikawa hivyo.

Kazi kubwa anayofanya bungeni ni kuruhusu vijembe, kebehi, shutuma kutoka kwa wabunge wa chama chake kwenda kwa wapinzani, huku akizima vijembe, kebehi, shutuma na maswali mazito ya wapinzani kwenda kwa wabunge wa CCM na serikali.

Makinda, na wenyeviti wake wanaruhusu wabunge wa CCM kulaani mandamano ya wapinzani kwamba eti yatachangia kupunguza kasi ya ukuaji uchumi nchini, lakini wanazuia wapinzani kutetea au kuelezea mchango na lengo la maandamano yao. Huu ni udikteta wa hali ya juu.

Kana kwamba haitoshi, Makinda amejitokeza kumzuia hata Waziri mkuu, Mizengo Peter Pinda kujibu maswali muhimu ya wapinzani.

Februari mwaka huu, Makinda alifoka kwa jazba pale Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alipoomba mwongozo wa Spika kwa kile alichoamini Waziri mkuu Pinda alisema uongo.

Katika majibu yake Pinda alisema kwamba polisi waliua Watanzania watatu katika vurugu za Arusha. Ukweli ni kwamba waliouawa ni Watanzania wawili na Mkenya mmoja.

Badala ya kutoa mwongozo alioombwa, yeye alimtaka Lema athibitishe kauli yake juu ya uongo wa waziri mkuu. Makinda hajasoma majibu ya Lema hadi leo.

Makinda ameonyesha jazba tena Alhamisi iliyopita, pale aliposimama kuzima maswali ya wabunge wa upinzani waliyomuuliza Pinda. Maswali yaliyozimwa ni ya Tundu Lisu (Singida Mashariki) na Esther Matiko (Viti Maalum) CHADEMA.

Lisu alitaka kujua sababu za serikali kutowafikisha mahakamani askari polisi waliohusika katika mauaji ya raia 72 yaliyofanyika katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 na mwaka huu; na Matiko alitaka maelezo ya kutofikishwa mahakamani askari waliohusika na mauaji ya raia katika eneo la Nyamongo, wilayani Tarime.

Makinda aliibuka kwenye kiti chake cha enzi na kusema kesi ziko mahakamani. Kama kesi ziko mahakamani, Pinda alishindwa kweli kujibu hivyo? Kwa nini Makinda ajue kwamba kesi ziko mahakamani lakini msimamizi mkuu wa serikali ashindwe kujua?

Makinda atakanusha vikali, ataruka kimanga na haraka atakimbilia kanuni za Bunge na kujificha humo, lakini hataweza kujinasua katika mtego aliojitengenezea yeye mwenyewe kwamba anafanya kazi ya kuua, kudhalilisha kambi ya upinzani ili kufurahisha waliombeba.

Makinda ajue kila anapotoa maamuzi ya jazba dhidi ya wapinzani, ndipo na wao wanapata fursa adhimu ya kuiaibisha serikali. Jazba bwana!

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: