Makinda anzisha mgogoro wa maslahi


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

KIU ya nyongeza ya posho kwa wabunge haielezeki. Hoja juu ya umuhimu wa posho hizo imejengwa na baadhi ya wabunge ambao wanaamini kuwa hiyo ni ngazi ya kufikia neema bila hata kujali kwamba uchumi wa taifa hili umesimama wapi.

Kelele za kutaka nyongeza kubwa ya posho za vikao zimepalizwa na wabunge wenyewe, si kwa bahati mbaya, ila ni kwa sababu moja kubwa; wameamua kujiona kwamba ndani ya jamii wao ni aina maalum ya viongozi na wangependa kuishi kama wanavyojihisi, si kama wanavyoonwa na wananchi na kutambuliwa kwa huduma yao kwa jamii.

Suala la posho hizi limekuwa na msukumo wa aina ya kipekee kiasi cha kujenga picha ya mgawanyiko baina ya mihimili miwili ya dola – Bunge na Serikali (Utawala) katika kufikiwa kwa uamuzi sahihi.

Wakati serikali imejiweka pembeni na kujionyesha kuwa kimsingi nyongeza ya posho hizo kwa sasa haiwezekani, Bunge si tu linasema posho hizo zinastahili kuongezwa kwa sasa, bali pia kuna taarifa kwamba wapo baadhi ya wabunge walioanza kupata nyongeza hiyo mwaka jana mwishoni.

Mvutano wa nyongeza ya posho ulikuwa mkali sana mwezi huu kiasi cha kusababisha Ikulu kutoa taarifa ikijitenga na madai kuwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa amebariki na badala yake ikaelezwa kuwa alipopelekewa mapendekezo ya Bunge, ingawa aliona yana mashiko, alishauri busara itumike.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwaambia waandishi wa habari kuwa suala hilo Rais alikuwa amelielekeza kwake ili alitolee uamuzi. Alipozungumza na wabunge kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Sita wa Bunge alisema kuwa posho hizo zilipata baraka ya rais, kauli ambayo pia ilitolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Kauli za viongozi hawa ndizo zilizosababisha kuibuka kwa hisia kwamba mihimili ya dola sasa inasigana.

Juzi Makinda ameripotiwa akieleza jinsi wabunge wanavyoishi kwa shida, kisa wanalipwa posho na mshahara mdogo mno. Makinda, ambaye ni mbunge tena wa siku nyingi wa jimbo, alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa nusu ya wabunge wanatamani kuacha kazi hiyo ila amewabembeleza wasifanye hivyo kwa kuwa watasababisha hasara kubwa kwa serikali kutokana na kuendesha chaguzi ndogo nyingi!

Kila nikitafakari kauli hii mpya ya Spika Makinda napata shida kujua kama kweli wabunge wanaotafuta ubunge wanategemea kwa maisha yao yote ubunge ili waishi.

Pamoja na ukweli kwamba wana muda mrefu wa kufanya vitu vyao binafsi wengine wakikwepa kufika kabisa kwenye majimbo yao, bado wanalipwa mshahara ambao kwa viwango vya watumishi wa umma ni wa juu.

Lakini hata kama mshahara huo ni mdogo kama Makinda anavyotaka kuuaminisha umma, wana vikao vya Bunge, vikao vya kamati, safari mbalimbali za nje, semina, ujumbe wa bodi za taasisi na mashirika ya umma na makongamano mbalimbali; vyote hivi vinafanya shajala ya mbunge ijae mwaka mzima, na kila kimojawapo katika hivyo wanalipwa posho.

Makinda anasema kuwa wabunge wana mikutano mifupifupi mitatu, yaani Februari, Aprili na Novemba; kila mmoja siku tisa, na vikao hivyo ndivyo wanalipwa posho hizo.

Unaweza kusema  9X3 = 27 ujumlishe mkutano mrefu wa bajeti ambao wabunge hukaa kuanzia Juni wiki ya pili hadi Agosti. Hapa nako kuna posho za vikao vya kutosha.

Kadhalika, Makinda hakusema habari za kamati za Bunge ambazo nyingine ni sawa na kazi ya kudumu mwaka mzima, kila siku wakaayo ni posho.

Inawezekana fedha zote wanazosaini wabunge haziwatoshi, lakini ni vema wakajua kuwa fedha kwa kawaida hazitoshi kwa sababu nadharia za uchumi zinasema kuwa kadri kipato cha mtu kinavyoongezeka ndivyo mtu huyo anavyoachana na mfumo wa maisha wa hali duni.

Ni sawa na kusema kama alikuwa anaendesha Toyota Corolla ghafla atajiona saizi yake ni Toyota Land Cruiser; kama alikuwa amepanga Mbagala Rangi Tatu, ghafla atajiona saizi yake ni Oysterbay au Masaki au Mikocheni au Mbezi Beach. Huo ndio ukweli.

Kinachosumbua wabunge si fedha kutosha ila ni kwa kiwango gani wamebadili mfumo wao wa maisha na kuanza kuishi kama wafanyabiasha wakubwa wenye fedha zao ambao wanamudu maisha ya ukwasi kwa sababu wanatengeneza faida.

Nimeambiwa kuna wabunge wamekopa benki kati ya Sh. 200 milioni na 400 milioni. Wamepeleka wapi fedha hizo? Kama ni kuwekeza ni jambo jema, lakini kama ni kujitakatisha ni jambo jingine. Mwisho wa yote fedha hizo ni mikopo ambayo italipwa kwa kukatwa kwenye mishahara yao na kwa kipindi kisichozidi miaka mitano. Kwa hali hiyo fedha zao si kwamba hazipo, zilikuwako ila wamezichukua mapema kwa madhumuni wanayojua wao.

Kilio cha posho cha wabunge ni matokeo ya mfumo mpya ulioanza kujengwa miaka ya 1990 juu ya nafasi ya ubunge katika jamii. Kwamba ni lazima awe na fedha zake za kununua watu, awe na maisha ya ukwasi wa hali ya juu, na kwamba yeye ni ATM inayotembea katika jimbo lake. Ni lazima awe na fedha za kugawa. Mfumo huu ndio unawatokea puani sasa.

Kwa kuwa Rais ameonyesha kutokuwa nao katika hili, na kwa kuwa Spika anaonyesha dhahiri wao kama wawakilishi wa wananchi wamefikishwa hapo kwa sababu ya umaskini wa wananchi ambao huwageuza ATM ndogo zinazotembea, na ni matokeo ya mfumo wa kununua kura na si kuchaguliwa kwa sifa ya ubora wa mgombea na uwezo wake wa kuwa kiongozi, basi sasa Bunge litangaze mgogoro wa maslahi na Utawala. Hili linawezekana kabisa kufanyika.

Bunge lina uwezo wa kutangaza mgogoro na rais kama ataonekana ameshindwa kutekeleza majumu yake; na hili ndilo ningemshauri Makinda sasa aanze kulichukua. Akutane na wabunge wenzake, wako wengi – nusu ya wabunge wote – wazungumze ili waanze mchakato wa kutangaza mgogoro na rais kwa kuwa amekwamisha Bunge, hali iliyosababisha wabunge wakose sifa ya kuwa ATM kwa wapigakura wao.

Hatua kama hii ningeiona ya kijasiri kwa Makinda kuliko kuendelea tu kulalamika kuwa wabunge wana njaa huku wakijua aliyezuia wasishibe ni nani. Hakuna uchawi hapa, Rais ndiye amewakwamisha wasiendelee kuwa ATM, lakini wakati huo huo wakiulizwa kama kweli nyakati hizi ni sahihi wao kujiongezea posho wakati mamilioni ya Watanzania wakishindwa kupata japo mlo mmoja kwa siku.

Ningemwona Makinda ana ujasiri kama sasa ataanzisha mchakato wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais kama kweli anaamini posho kwa wabunge ni muhumu kiasi hicho, vinginevyo anyamaze milele kwani kelele za posho zinaudhi na kuonyesha ubinafsi wa hali ya juu wa watu ambao walipaswa kuwa watetezi wa wananchi lakini wamegeuka.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: