Makinda - jazba na makundi maslahi, atavivuka vipi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version

WATANZANIA wengi walijiuliza maswali mengi mwaka jana mwishoni alipojitokeza Anne Makinda kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri wa Tanzania . Walijiuliza maswali haya kwa sababu, katika mazingira ya kawaida, isingewezekana kujitokeza kupambana na bosi wake, Samuel Sitta. Ndiyo maana watu wakawa wanajiuliza kulikoni?

Kwa bahati nzuri uvumi ulitanda kiasi cha kuingia magazetini na Spika Makinda aliamua kuvunja ukimya na kufanya mkutano na waandishi wa habari akisema kwamba ‘katu hakutumwa.”

Makinda alikwenda mbali zaidi na kueleza kwamba amejipatia sifa nchini kwa kuishi kwa uadilifu na hata nyumba zake alizojenga amejenga kwa mkopo kutoka benki.

Ingawa hakuna ubishi juu ya mambo mawili kuhusu Makinda; moja, kwa kuwa alisema mwenyewe hakutumwa na yeyote kuwania nafasi hiyo; mbili, kwamba kuwania nafasi hiyo, ilikuwa ni haki yake ya kimsingi, lakini kila siku mambo yanayotokea bungeni maswali mengi yanajitokeza juu ya utendaji wa Spika huyu.

Katika mambo ambayo yamegubika Mkutano wa Pili wa Bunge la 10, ni suala la kubadili kanuni za Bunge kuhusu ‘upinzani rasmi’. Ingawa inawezekana kabisa kwamba kila zama na vitabu vyake, bado haja ya nyakati pekee imekwama kutibu kiu ya maswali haya.

Hata hivyo, kwa kuwa watu waliowasilisha maombi ya kurekebishwa kwa kanuni za Bunge yaani, Mbunge wa Wawi- CUF, Hamad Mohamed Rashid, na David Kafulila, Kigoma Kusini – NCCR-Mageuzi, ni watu ambao kwa njia moja au nyingine walikuwa wamekwaruzana na CHADEMA, chama ambacho kimsingi ndicho kilikuwa kina sifa za kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni, ingekuwa ni busara zaidi kama Spika Makinda angelichukulia maombi yao kwa hadhari kubwa.

Lakini la umuhimu zaidi ni ukweli kwamba Makinda katika Bunge la Tisa ambalo marekebisho makubwa ya kanuni za Bunge yalifanyika mwaka 2007, alikuwa Naibu Spika. Alikuwa msaidizi namba wa Sitta, alishiriki kwa kina katika mchakato mzima wa kupitishwa kwa kanuni hizo.

Kwa kuwa alikuwako wakati huo, inakuwa ni vigumu kujua ni kwa nini wakati huo hakuona sababu ya kufanywa kwa marekebisho ambayo juzi yalionekana dhahiri kulenga kukidhoofisha chama kimoja cha siasa, zikiwa ni siasa za kihafidhina na ulipizaji wa kisasi kama si kukomoana?

Marekebisho ya kanuni za Bunge juzi si tu yamepora nafasi ya CHADEMA kuchanua katika kutimiza wajibu kama chama kikuu cha upinzani, bali yamefanywa kama adhabu ya kukiadhibu chama hicho kwa kuwa tu kuna hisia kwamba ndicho kimekuwa chimbuko la kupotea kwa umaarufu wa CCM kiasi cha kupoteza mvuto na kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Lakini pia, CHADEMA kinaangaliwa kama chama ambacho kinataka kuifanya nchi isitawalike, si kwa sababu ya kuendesha hila na uzushi, ila kwa sababu inadhaniwa kwamba chini ya bunge lililopita, baadhi ya wabunge waliachwa tu kuiadabisha serikali na kwamba bila kuwafunga ‘speed governor’ hali ya CCM inaweza kuwa mbaya zaidi mwaka 2015.

Ni kwa mkakati huo, kwa CCM ya wahafidhina, ambayo kila uchao wanawaza kubakia madarakani si kwa kuwa ni utendaji wazuri, ila kwa kulinda maslahi hao, ilionekana wazi kwamba moto wa CHADEMA ni lazima upunguzwe kama si kuzimwa kabisa ndiyo maana Makinda akajikuta anatumbukia kwenye mtego wa kupora nafasi ya CHADEMA kusimamia kamati zote matumzi ya fedha za umma.

Hali hii ikitazamwa vizuri zaidi inamweka Makinda kwenye mtihani mgumu zaidi, kwamba sasa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa iliyokuwa chini ya Dk. Wilibroad Slaa katika Bunge la Tisa, itaweza je kuvuka pale ilipofikishwa chini ya uongozi mpya wa Mbunge wa Vunjo –TLP, Augustine Mrema?

Maamuzi ya kubadili kanuni wiki iliyopita wakati wote ni lazima yatazamwe kwa mapana ya kutafakari na kuangalia ni kwa kiwango gani yalilenga kulipa nguvu Bunge dhidi ya serikali na hasa juu ya matumizi ya ovyo kabisa ya kodi za wananchi.

Kwa kupima huko kutampa Makinda nafasi ya kuonekana ni kiongozi anayesukumwa na nia ya kuwaletea maendeleo wananchi zaidi na si kutetea maslahi ya kundi fulani ndani ya Bunge.

Ukiweka pembeni suala la marekebisho ya kanuni, utendaji wa Makinda katika vikao viwili vilivyofanyika chini yake, ameonekana kuwa kiongozi ambaye hana uvumilivu. Mara kadhaa amekuwa mkali katika mambo ambayo kwa kweli angeliweza kabisa kuyafanya kwa wepesi na kuyamaliza bila kuamsha hisia za kimakundi.

Ukichukuliwa jinsi Makinda alivyolishughulia suala la Mbunge wa Arusha Mjini – CHADEMA, Godbless Lema, alipotaka kujua hatua ambazo anaweza kuchukua mbunge endapo atagundua kwamba kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu amelidanganya Bunge, Makinda badala ya kuonyesha uvumilivu wa kiuongozi, alijikuta analipuka na kukemea jambo ambalo halikuwa na sababu kukemea.

Lakini hakukemea tu, alimpa changamoto Lema kuandaa maelezo yake na kuyawasilisha bungeni, kuthibitisha kwamba Waziri Mkuu alikuwa amesema uongo. Makinda kwa muonekano, yaani kile wanachosema Waingereza ‘paralinguistic gestures’ alionekana dhahiri kukerwa na Lema.

Ukitafakari kwa kina hali ya mambo ilivyo katika kuendesha Bunge kwa sasa, walau kwa mikutano hii miwili, kuna kila dalili kwamba Makinda atakuwa na kibarua kigumu sana katika utawala wake wa miaka mitano hivi ijayo, kikubwa kitakachomsumbua ni, moja; jazba za mara kwa mara hata kwa mambo madogo ambayo angeliweza kuyamaliza kwa kutabasamu tu; mbili, bado hisia kwamba Makinda alisukumwa kwenye nafasi hiyo na kundi moja lenye maslahi makubwa kuelekea mwaka 2015, ni hoja ambayo haiwezi kumalizwa kwa kauli za kusema ‘sikutumwa tu’ ila kwa matendo na maamuzi halisi yanayotafsiri kauli zake.

Haya ni mambo ambayo Makinda kama anataka akumbukwe kwa lolote jema katika Bunge la 10 hana budi kuyazingatia wakati wote; ni jambo la bahati mbaya kwamba mwanzo wa Makinda umeonyesha dalili mbaya; na kama ataendelea hivi basi kuna hatari ya Bunge la 10 kuwa la rabsha, vijembe na pengine kuhujumiana si kwa sababu ya kuwasaidia na kuwatumikia wananchi, ila kutimiza matakwa na maslahi ya makundi. Tuvute subira tuone kama Makinda atavuka vikwazo hivi.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: