Makinda, Werema wataficha nyuso zao


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version

KITENDAWILI cha Katiba ya Tanzania kuwa bubu juu ya uteuzi wa mawaziri ambao hawajaapishwa kuwa wabunge, kimeanza kuteguliwa.

Sasa ni dhahiri kwamba kuna utata katika uteuzi huo na kwamba mawaziri watatu walioteuliwa kwa mtindo huo hawatashiriki vikao vya kamati za bunge vinavyotarajiwa kuanza karibuni.

Kauli ya Naibu Spika, Job Ndugai iliyokaririwa na vyombo vya habari imeweka suala hilo wazi. Kwamba, mawaziri hao hawataruhusiwa kufanya shughuli yoyote ya bunge bila kuapa kiapo cha utii bungeni.

Mawaziri wanaohusika na sakata hilo ni Prof. Sospeter Muhongo wa nishati na madini na naibu mawaziri wawili wa fedha, Janet Mbene na Saada Mkuya Salum. Mawaziri hulazimika kuingia katika kamati za bunge kuwasilisha rasimu za bajeti ya serikali,  miswada ya sheria na kujibu hoja za wabunge kwa niaba ya serikali.

Ndugai akikariri katiba amesema, “mbunge yeyote ambaye hajaapa kiapo cha utii mbele ya spika ataruhusiwa kuchagua spika tu, lakini hataruhusiwa kufanya kazi nyingine za bunge hadi awe ameapa bungeni.”

Kauli ya naibu spika imenyosha mambo, baada ya bosi wake, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kuyapindisha kwa kutetea kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuteua wabunge na kuwapa uwaziri kabla ya kuapishwa bungeni.

Tanzania ya sasa inahitaji wanasiasa aina ya Ndugai, ambaye walau kwa hili, ameweka kando ushabiki na tabia ya wanasiasa na watendaji kufumbia macho maovu yanayofanywa na viongozi.

Naibu Spika ameonyesha kukerwa na kitendo cha Jaji Werema kumshauri rais afanye kitendo hicho kinachopindisha kanuni za bunge na kuleta mkanganyiko.

“Hili swali ungemuuliza mwanasheria mkuu wa serikali kwa kuwa ndiye mshauri wa sheria wa rais, kwa nini aliamua kufanya hivyo, lakini kwetu bungeni halijakaa vizuri kwani kanuni za bunge ziko wazi haziruhusu kabisa,” Ndugai alikaririwa na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kitu ambacho Spika Makinda ama hakukiona au naye ameamua kukifumbia macho makusudi, ni kwamba uteuzi wa Rais Kikwete, mbali na kukinzana na kanuni na utamaduni wa bunge, pia utaathiri ratiba na shughuli za bunge kwa ujumla.

Ndugai amefafanua kuwa uteuzi huo unaweza kusababisha vikao vya kamati kuahirishwa kusubiri hadi mawaziri wanaohusika waapishwe na spika katika mkutano wa bunge wa bajeti unaoanza 12 Juni 2012.

Njia nyingine inayoelezwa na naibu spika, ni uwezekano wa Waziri Muhongo kuwatumia manaibu wake wawili, George Simbachawene na Stephen Maselle ambao wamekwishaapishwa bungeni, kujibu hoja za wizara hiyo.

Hata hivyo, upo uwezekano wa naibu mawaziri hao kukwama kusimamia shughuli za wizara kwenye kamati, kwa kuwa iliwahi kutokea kamati kuwatimua watendaji wa wizara pale waziri asipoonekana bila sababu ya msingi.

Njia nyingine mbadala ya kuepukana na upofu huo wa sheria, ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kumteua waziri mwingine yeyote kusimama kwenye kamati badala ya waziri wa Nishati na Madini.

Ufafanuzi huu wa Ndugai, unawaweka pabaya Makinda na Werema kwa kushindwa kuona kasoro hizi za wazi.

Hata wanasheria mbalimbali na wananchi wa kawaida wamekuwa wakihoji suala hili huku wakihoji Rais Kikwete alikuwa na haraka gani kufanya uteuzi huo, badala ya kusubiri bunge likutane ili pamoja na mambo mengine, “wabunge wake” waape.

Siku chache baada ya Rais Kikwete kuteua wabunge hao na kuwapa uwaziri kabla ya kuapishwa bungeni, Makinda aliibuka na kumtetea kuwa hajavunja kipengele chochote cha sheria kwa sababu aliowateua amewapa uwaziri ili wawajibike katika serikali yake.

Kwa mujibu wa Makinda, wateule hao wakishaapishwa kuwa mawaziri, wana haki ya kuanza kufanya kazi za kiwaziri kwenye wizara walizopangiwa.

Hata hivyo, Makinda amesema kanuni za bunge zitakuwa zinawafunga wateule hao wa rais kuingia bungeni na kujibu maswali bila kuapishwa kuwa wabunge.

Mawaziri hao wataapishwa na Spika 12 Juni 2012 kabla ya kuanza vikao vya bunge la Bajeti.

Akijibu maswali ya mwanaHALISI, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah ameibua utata mpya, kuwa mawaziri ambao hawajaapa bungeni, wanaweza kushiriki shughuli za kamati za bunge “kwa kutumia utaratibu mwingine wa kikanuni.”

Amesema chini ya utaratibu huo wa kikanuni, hata wananchi wengine ambao si wabunge wanaweza kuitwa kwenye kamati na kutoa maelezo ambayo kamati husika inayahitaji.

Kwa upande wake, Jaji Werema amezidi kutetea kile watu wengine wanakiona ni makosa, kuwa Rais Kikwete hajavunja sheria kwa kuwaapisha wabunge wateule kuwa mawaziri kabla ya kiapo cha bunge.

Amesema kitendo hicho ni sahihi. Hata hivyo, ameahidi kutoa elimu kwa umma kuhusu mamlaka ya rais ya uteuzi wa wabunge kwa sababu ni jambo lenye maslahi ya jamii na linalohitaji kufafanuliwa.

“Msingi wa katiba tunaoanza nao ni maelekezo ya masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 55(4) kwamba. “Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge,” alisema Jaji Werema akinukuu katiba.

Ameeleza kuwa wabunge wanaohusika hawahitaji kuapishwa kwanza bungeni ili wawe wabunge na kwamba kiapo cha mbunge bungeni kinamwezesha tu kushiriki katika shughuli za bunge.

Hata hivyo, Jaji Werema katika taarifa yake hakugusia kama vikao vya kamati za bunge ni sehemu ya shughuli za bunge au la.

Vile vile, Jaji Werema amesimamia Ibara ya 56 ya Katiba inayosema, anayeteuliwa kuwa waziri lazima awe ameapa kwanza mbele ya rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na bunge.

Hapa mwanasheria mkuu haelezi “kiapo kingine chochote kilichowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na bunge” ni kipi, na huenda ndo hiki cha utii bungeni.

Watu mbalimbali wenye taaluma ya sheria, wamejadili suala hili kupitia vyombo vya habari wakisema tatizo hili ni matokeo ya ubovu wa katiba iliyopo kwa kuwa ni vigumu kusema rais alivunja katiba au la.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla amekaririwa akisema katiba haisemi kama hatua hiyo ya rais ni uvunjaji wa katiba au la.

“Katiba yetu haimkatazi wala kumruhusu Rais kuwaapisha mawaziri aliowateua ambao hawajaapa kuwa wabunge,” Stolla amekaririwa akisema.

Stolla naye anahoji kama “kiapo kingine chochote” anachotakiwa kuapa waziri, si kile cha Bunge?

Dawa ya haya yote ni katiba mpya, ambayo itaangaza mianya kama hii inayotumiwa na watawala kufanya mambo watakavyo, na kuziba. Pia, kupata viongozi wanaofuata katiba katika uongozi wao, maana kuwapo katiba ni jambo moja, na kuifuata ni jambo jingine.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: