Makundi ya wabunge yajirudia


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 April 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Dk. Mwakyembe

MGAWANYIKO mpya umeibuka kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wenye mtizamo wa kizalendo dhidi ya wale wanaofikiria zaidi maslahi ya kibiashara, MwanaHALISI imebaini.

Mgawanyiko huo umethibitika katika kikao cha kamati ya wabunge wa chama hicho walipojadili muswada wa sheria ya madini, kabla ya kuwasilishwa kwake bungeni wiki iliyopita.

Kulingana na vyanzo vyetu vya habari, kipengele kilicholeta mvutano mkali kikaoni ni Ibara ya 43 ya muswada kuhusu Leseni Maalum ya Uchimbaji (SML), inayozungumzia ukomo wa leseni ya mwekezaji aliyeruhusiwa kuchimba madini.

Katika muswada huo uliopitishwa baada ya mvutano mkali, Ijumaa iliyopita, serikali ilipendekeza kusiwe na ukomo wa leseni ya uchimbaji.

Muswada ulikuwa ukitaja kuwa leseni iwe kwa muda wote hadi madini yaliyopo eneo husika yatakapokuwa yamekwisha.

Kwa mfano, iwapo utafiti utaonyesha kuwa madini yatadumu kwa miaka 100, basi leseni itolewe kwa kipindi chote hicho.

Hata hivyo, vyanzo vya habari vya gazeti hili vimesema wabunge waligawanyika katika hilo. Baadhi yao walijenga hoja kwa hisia za kizalendo za kulinda raslimali ya taifa lakini wengine walipinga.

Wabunge wanaotajwa kuwa walitaka ukomo wa leseni uwe wa milele ni Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Chrisant Mzindakaya (Kwela), George Simbachawene (Kibakwe) na Siraju Kaboyonga (Tabora Mjini).

Upinzani ulitoka kwa Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela) na Christopher ole Sendeka (Simanjiro), wanaofahamika kwa ujasiri wa kutetea raslimali za taifa.

Waliotaka ukomo wa leseni walikuwa wakijaribu kuhakikisha raslimali za nchi haziachwi milele mikononi mwa wageni.

Bali wale waliokuwa wakitetea kusiwe na ukomo walikuwa na mtizamo kuwa wawekezaji wasiwekwe katika mazingira yatakayowatia hofu na hatimaye kukimbia.

Hisia za mitizamo hiyo tofauti zilianzia kwenye Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini na baadaye kuendelea katika mkutano wa bunge tarehe 16 Aprili.

Kwa mujibu wa vyanzo, Chenge na Mzindakaya walinukuliwa wakisihi kusifanyike mabadiliko “yatakayokimbiza wawekezaji” ambao serikali inawahitaji kwa manufaa ya kiuchumi.

Chenge alinukuliwa akitetea muswada kwa kusema umelenga kuweka vivutio kwa wawekezaji ili wawekeze na wanawekeza kweli na kwamba wanaingiza faida kubwa kwa taifa.

Kwa upande wa Mzindakaya, alikaririwa akisema kikaoni kwamba wasifanye makosa ya kufanya mabadiliko yatakayokimbiza wawekezaji.

Kabla ya kikao cha wabunge wa CCM, Chenge na Mzindakaya waliripotiwa kukutwa nje ya ukumbi wakibadilishana mawazo na wageni.

Miongoni mwa waliotajwa kuwa nao walikuwa Deo Mwanyika, mdogo wa mwanasheria mstaafu Johnson Mwanyika na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Goldmine – moja ya makampuni yaliyowekeza katika migodi nchini.

Hoja nyingine iliyoleta mjadala mkali na kuonyesha tofauti za misimamo miongoni mwa wabunge ni iliyohusu uwezekano wa ubia wa serikali katika kuendesha migodi.

Kwa mkondo wa kupishana kauli na utashi, wabunge waligawanyika pia; hawa wakitaka serikali iwe na hisa huku wengine wakipinga.

Kundi la Chenge lilipinga ubia wa serikali, lakini lilipinga pia pendekezo jingine la serikali kutaka madini kama ya vito yanayopatikana juu kidogo (siyo chini sana migodini), yachimbwe tu na Watanzania.

Naye Dk. Mwakyembe alipojadili suala hilo alipendekeza waziri anayehusika na madini apewe mamlaka ya kumshauri mzalendo kutafuta mgeni wa kuwekeza naye, huku yeye akimiliki asilimia 60 na mgeni 40.

Mjadala wa muswada wa sheria ya madini ulikuwa mkali kiasi kwamba wabunge walikutwa wakishindwa kupeana mikono baada ya bunge kuupitisha.

Baadhi ya wabunge wamesema walisikia mmoja wa mawaziri akisema nje ya bunge, “Acha tu. Tutairudisha sheria hii na kuifanyia marekebisho haraka iwezekanavyo.”

Haikufahamika waziri huyo, anayetoka kanda ya ziwa, alikuwa na uhakika gani kama angechaguliwa kuwa mbunge au waziri baada ya uchaguzi ujao.

Mivutano ya wabunge ilimaanisha kwamba ule mgawanyiko uliokuwepo, kuhusiana na sakata la mkataba wa kitapeli wa Richmond, ulikuwa haujaisha.

Kadhalika, hii ina maana kwamba kazi ya kutafuta chimbuko la mgawanyiko wa wabunge, waliyopewa wazee wakiongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi, bado haijafanikiwa.

Mzee Mwinyi, rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwaongoza Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa kuchunguza mgawanyiko miongoni mwa wabunge na wawakilishi wa CCM.

Kamati yao ililazimu kuongezewa muda wa kuwasilisha ripoti yake mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), lakini ripoti hiyo ilizusha mashaka makubwa.

Baadhi ya wabunge waliohojiwa walisema wazi kwamba wao hawana ugomvi na wenzao isipokuwa tatizo lililopo ni kwamba baadhi yao wanapinga ufisadi huku wengine wakijitahidi kuutetea na kutaka kusafisha watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama.

Mgawanyiko ulikuwa wa makundi yaliyotambuliwa kuwa chini ya Edward Lowassa kwa upande mmoja; Spika Samwel Sitta kwa upande mwingine.

Sitta amekuwa akishutumiwa na kundi jingine kwa kuruhusu chama na serikali kuchafuliwa wakati wa mijadala ya bunge.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: