Malalamiko ya Mpondela, Akilimali ni uchuro


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend

MIONGONI mwa wanachama mashuhuri katika klabu ya Yanga, ambao wanastahili kufuatwa kutoa ushauri kukiwa na tatizo, ni George ‘Castro’ Mpondela.

Kwanza yeye alikuwa katibu mkuu wa klabu hiyo katika miaka ya mwanzoni mwa 1990, akisimamia pendekezo la kuiongoza klabu kuendeshwa kwa mfumo wa kampuni.

Lakini pili, ana uzoefu na viashiria vya migogoro katika klabu nyingi nchini, ikiwepo ya Yanga. Mpondela alikumbana na wakati mgumu mwaka 1994 wakati wafadhili walipojitoa kuisaidia klabu hiyo, wakishinikiza aondolewe.

Matukio mengi yalifanyika na hata kuidhoofisha timu ifungwe ionekane uongozi wake mbaya. Alipojiuzulu mwaka 1995, ili aanze maisha mapya ya siasa, Mpondela hajaweza kuaminiwa kupewa madaraka kwenye klabu hiyo.

Mpondela huyo, ndiye akishirikiana na mwanachama mwingine Ibrahim Akilimali, kwa niaba ya walichodai wanachama wa klabu hiyo, wameandika barua kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulalamikia serikali kuingilia uendeshaji wa klabu za mpira.

Lakini, maudhui ya barua ya Mpondela na Akilimali si kulalamikia uendeshaji bali kupinga utaratibu mzima wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa klabu hiyo uliofanyika Julai 18, 2010.

Wakati kichwa cha habari kinasema; “Yah: Serikali kuingilia uendeshaji wa vilabu vya mpira wa miguu” ndani anaanza malalamiko yake kwa kusema; “Sisi ni wanachama hai wenye kadi namba 000020 na 000073 tulikuwa washauri wa mmoja wa wagombea ambaye tuliambatana naye katika kampeni zote zilizofanyika.”

Anaendelea kusema, “…Tunadiriki kusema wazi uchaguzi huu uligubikwa na mizengwe ambayo ilifanya uchaguzi uonekane haukuwa huru na haki.” Barua ina udhaifu mwingi.

Kwanza, hakuna mahali ambapo Mpondela na wenzake wanathibitisha kwamba serikali imeingilia uendeshaji wa vilabu vya mpira wa miguu.

Angalau angesema ‘labda kwa kuwepo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, serikali imeingilia uchaguzi’ maana uendeshaji anaozungumzia ni wa shughuli za kila siku.

Pili, hata kama lingekuwa suala la serikali kuingilia chaguzi za klabu, katika barua nzima hakuna mahali anapotaja klabu nyingine mbali ya Yanga.

Tatu, Mpondela na wenzake wanazungumzia utata wa mtu aliyechukua fomu ya mgombea Lloyd Nchunga kwamba ni Ridhiwani Kikwete mtoto wa Rais Jakaya Kikwete. Hoja hii ilishajibiwa wakati wa mchakato na usaili na haikuwa na nguvu.

Nne, bila uthibitisho wowote, Mpondela na wenzake wanawatuhumu baadhi ya wagombea kuwa ni wezi hivyo hawakustahili kuandikiwa barua ya kupongezwa. Hivi, hilo ni jukumu la TFF?

Tano, inasikitisha kuona Mpondela na wafuasi wake wameshindwa kujua kwa nini Ridhiwani na Bendera walifika kwenye uchaguzi wa Yanga. Wanachama hawa wanalazimisha ieleweke kuwa Ridhiwani alifika kwa kuwa ni mtoto wa Rais na Bendera kwa vile ni waziri—huu ni upotoshaji kwani Ridhiwani si kiongozi wa serikali.

Ikiwa wanachama hao hawajui kuwa Ridhiwani alikuwa mwenyekiti wa muda wa kamati ya uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga, na ikiwa hawajui kuwa Bendera alikuwa mgeni rasmi, barua hii itakuwa na lengo la kuanzisha mgogoro usio na maana katika klabu hiyo.

Mwisho, wanasema, “Tunaomba TFF itoe ufumbuzi wa jambo hili la sivyo uamuzi wetu wa kwenda kortini utaendelea ili haki yetu ipatikane, mahakamani.”

Mpondela, ambaye ni mmoja wa wazee wa klabu hiyo, anapaswa kubeba dhamana kubwa ya kuwahamasiha wanachama kuunga mkono uongozi mpya ili kurejesha amani klabuni vinginevyo anaweza kuwa anapigania kitu ambacho hawezi kukipata.

Kiongozi mstaafu hapaswi kuwa mwanzilishi wa tafrani na migogoro bali kuonyesha njia inayopaswa kufuatwa ili kuweka mshikamano na umoja.

Isitoshe, mwenyekiti mpya Nchunga ameunda safu ya uongozi akiwashirikisha waliokuwa wapinzani wake, Mbaraka Igangula katika nafasi ya kamati ya utendaji na Francis Kifukwe katika Bodi ya Wadhamini.

Nchunga akitambua umuhimu wa umoja, amefanya hivyo ili watoe mawazo yao kwenye vikao halali. Hii ina maana wanachama ambao walikuwa wanawaunga mkono wamewakilishwa vilivyo, sasa Mpondela na Akilimali wanataka nini zaidi?

Kiongozi mstaafu anapaswa kuwa kisima cha kuchota busara badala ya kuandika barua za uchochezi na tishio la kwenda mahakamani.

Jambo zuri ni kwamba Mpondela, Akilimali pamoja na wafuasi wao wanasema wamesoma Katiba ya FIFA. Kama wamesoma ibara zote na wamezielewa, waende kortini waone cha moto. Mpondela, Akilimali waepushe uchuro.

0
No votes yet