Mambo yamwendea kombo Putin


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly versionSend to friend

BAADA ya mfululizo wa maandamano ya maelfu ya watu ya kupinga ushindi wa chama Vladimir Putin, sasa anakabiliwa na changamoto mpya katika uchaguzi mkuu ujao.

Tajiri na mtu mashuhuri, bilionea na mmiliki wa New Jersey Nets, Mikhail Prokhorov ametangaza kuchuana na Putin katika uchaguzi mkuu wa Machi 2012.

Prokhorov alitangaza uamuzi huo saa chache baada ya waziri wa zamani wa fedha chini ya utawala wa Putin, Alexei Kudrin, kusema yuko tayari kuanzisha chama kipya.

Kujitokeza kwa Kudrin na Prokhorov ni uthibitisho wa kiasi cha kutoridhishwa na mwanasiasa huyo aliyetawala siasa za Russia kwa miaka zaidi ya 12 sasa.  Uthibitisho mwingine ni kuibuka kwa mfululizo wa maandamano nchi nzima.

Maelfu ya watu wamekuwa wakijimwaga barabarani kulalamikia uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi wa wabunge Desemba 4, 2011 yaliyokipendelea chama cha United Russia kinachoongozwa na Putin.

Pia waandamanaji walimshangilia Mikhail Gorbachev, rais wa mwisho wa iliyokuwa Soviet hadi ilipovunjika 25 Desemba, 1991.

Udanganyifu na ukweli kwamba chama chake kilifanya vibaya katika uchaguzi huo – kupoteza asilimia 20 ya viti japo bado kiliongoza kwa wingi wa kura chache – vilichochea upande wa upinzani kuanzisha mfululizo wa mandamano, likiwemo kusanyiko kubwa la watu wapatao 30,000 katikati ya jiji la Moscow hivi karibuni.

Katika mkutano na waandishi wa habari kutangaza nia yake ya kuwania urais hivi karibuni, Prokhorov alijizuia kumshutumu Waziri Mkuu, Putin wala Rais Dmitry Medvedev, lakini alisisitiza "jamii inaamka."

"Mamlaka zitakazoshindwa kufanya majadiliano na jamii zitaondoshwa,” alisema.

Baada ya kuwepo kwa shutuma nyingi kuhusu uchaguzi huo wa wabunge, Rais Medvedev aliahidi kupitia ukurasa wa Facebook kwamba visa vya wizi wa kura katika uchaguzi huo vitachunguzwa.

Lakini msemaji wa Putin, Dmitry Peskov, alitabiri kuwa hata ukifanyika uchunguzi itabainika hitilafu kidogo tu ambazo haziwezi kuathiri matokeo.

Matamshi hayo  ya Peskov yanathibitisha kuwa Putin – aliyeshika wadhifa wa urais kuanzia 2000-2008 na akashuka kuwa Waziri Mkuu kutokana na ukomo wa mihula – anashikilia msimamo licha ya maandamano makubwa kuwahi kutokea nchini Russia baada ya iliyokuwa Soviet.

Ili kuonyesha kwamba Putin anapendwa na watu wengi yaliandaliwa maandamano wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kumuunga mkono. Taarifa zinasema yalihudhuriwa na watu 25,000.

Taarifa rasmi na hata kwa maoni ya watu waliojitokeza kuunga mkono walilazimishwa. “Wala sijui kwa nini hasa nipo hapa,” alisema “mfuasi” mmoja wa Putin na mwingine alisema alilazimishwa.

"Tumeambiwa tuongeze idadi ya watu,” alisema mwanamke mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mhasibu katika chama cha United Russia.

Magazeti na mashirika mengine ya habari yanasema watu walioandamana kumuunga mkono Putin walifikia 5,000 hivi na wala si 25,000 kama inavyotangazwa.

Bado haieleweki, mpinzani huyo mwenye umri wa miaka 46 Prokhorov anaweza kuhimili kiasi gani ushindani. Utajiri wake, kwa mujibu wa jarida la Forbes unafikia dola 18 bilionni.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Muonja asali huyo,
Sokoro