Mamilioni yafukuliwa shambani kwa waziri wa zamani


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version

WAZIRI wa Kazi wa zamani katika serikali ya Rupia Bandah, Austin Liato amejikuta matatani baada ya vyombo vya upelelezi vya Zambia kufukua fedha taslimu kiasi cha Kwacha 2.1 bilion, (dola 412,000 au TSh 700 milioni) zilizokuwa zimezikwa katika shamba lake la Mwembeshi, karibu na Lusaka.

Haikuweza kuelezwa mara moja kwa nini waziri huyo wa zamani ambaye alikuwa swahiba mkubwa sana wa rais wa zamani, Rupia Banda, afukie fedha hizi nyingi shambani mwake badala ya kuziweka benki.

Hata hivyo, wapelelezi wanahisi kwamba fedha hizo zilipatikana kwa njia ya kifisadi na kwamba zilifukiwa ili baadaye kutafuta namna ya ‘kuzisafisha’ (money laundering).

Inspekta Jenerali wa Polisi, Martin Malama aliwaambia waandishi wa habari mapema wiki hii kwamba fedha zilikutwa zimefukiwa ndani ya jengo moja ambalo ujenzi wake ulikuwa ukiendelea katika shamaba la Liato.

IJP Malama alisema fedha hizo taslimu katika noti za viwango vya Kwacha 20,000 na 50,000 na katika mabunda ya kwacha milioni 25 kila moja zilikuwa zimezikwa katika jengo hilo ambalo liliwekewa vyombo vya kutahadharisha wezi na zilikuwa katika makasha mawili ya chuma ya kuhifadhia fedha (safes) na juu yake ikajengewa zege ya unene wa kiasi cha sentimita 30.

Aidha, wapelelezi walikuta hati za kuingizia fedha benki (bank slips) kutoka benki kadhaa zikiwemo Bank of Zambia, Finance Bank na benki ya ZANACO za tarehe kuanzia Machi 2010 na Machi 2011. Iliwachukua polisi zaidi ya saa mbili kuvunja hiyo zege na kuzifikia fedha hizo.

IJP Malama amebainisha kwamba kukamatwa kwa fedha hizo haukuwa mkakakati wa kuwalenga mawaziri na maafisa wengine wa serikali ya zamani, bali ilikuwa  kutokana na zoezi tu la kawaida linaloendelea katika kupambana na ufisadi.

Pia alitoa wito kwa viongozi wa umma kuacha mara moja vitendo vya uporaji wa mali za umma bila kujali hali ya umasikini inayowaandama Wazambia walio wengi.

Alisema polisi itachunguza chanzo cha fedha hizo kwani namna zilivyohifadhiwa yaonyesha hazikupatikana kwa njia ya halali na kwamba mhusika atahojiwa mara moja.

Wakati huo huo, Rais wa nchi hiyo, Michael Sata, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema amepata habari hiyo kwa mshtuko mkubwa – kwamba kiasi kikubwa hicho cha fedha kilikutwa kimefichwa kwa namna ya ajabu na isiyo ya kawaida katika shamba la waziri wa zamani.

Alisema kufichwa kwa fedha hizo kunaleta maswali mengi ya namna zilivyopatikana.

Alisema: “Inanivunja moyo kuona kwamba mtu anaweza kwenda mbali na kufanya hivyo iwapo fedha zilipatikana kwa njia ya halali.”

Hata hivyo, habari nyingine zimebainisha kwamba mawaziri kadhaa wa serikali ya zamani ya chama cha MMD wanachunguzwa na vyombo vya upelelezi kutokana na utajiri waliojilimbikizia wakiwa madarakani.

zakmalang@yahoo.com
0
No votes yet