Mapunda kampiga 'red card' Nchimbi


Clement Ulisa's picture

Na Clement Ulisa - Imechapwa 24 February 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Michezo

UCHAGUZI mdogo wa kujaza nafasi ya makamu wa pili wa rais wa TFF utakaofanyika Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam, unatarajiwa kukutanisha wagombea wawili wenye sifa tofauti.

Mtaji wa Ramadhani Nassib aliyepoteza nafasi hiyo baada ya Villa Squad iliyomdhamini kushuka hadi daraja la kwanza anawania tena nafasi hiyo akijinadi kwa matunda ya kazi yake alipokuwa makamu wa rais wakati mpinzani wake, John Nchimbi anategemea kampeni kali aliyoifanya katika siku za hivi karibuni.

Mtaji wake hauko katika soka bali umaarufu wa familia yake katika nyanja za siasa. Kazi kubwa anayoifanya mgombea huyo ni kujitambulisha; yeye ni nani na lini alianza kujiweka karibu na soka na anakusudia kufanya nini akichaguliwa.

Ingawa si lazima kila mdau wa soka awe anafahamika kwa wote, lakini walau kwa wazee wa mpira wa miguu hapa nchini ambao ni TFF, vyama vya soka vya mikoa, wilaya, vyama vya waamuzi na makocha. Asiyewajua hao atalazimika kujenga ushawishi wa hali ya juu ili wamjue na kumfikiria kumpa kura.

Watu walio karibu na kijana huyo wanadai kwamba ana uwezo mkubwa kujenga hoja na kufanya ushawishi huku akisaidiwa nyuma yake na wanasiasa kadhaa. Yeye binafsi hana mafungamano na soka au wadau wa soka na inaelezwa anaweza kuwa ameanza kujihusisha na Majimaji baada ya kupata wazo la kugombea.

Japokuwa kila mmoja ana bahati yake, kijana huyo atakuwa na wakati mgumu katika kinyang’anyiro hicho kutokana na ukweli kwamba anafahamika zaidi katika nyanja za siasa na si soka. Huu ndio mtaji wa watoto wa wanasiasa.

Kwa mfano, baada ya viongozi kadhaa kushinda viti vya ubunge na ndani ya chama mwaka 2005 na 2007 ndipo ndugu, jamaa na watoto wao wakajitokeza kuwania nafasi za uongozi kwenye michezo, halaiki na skauti wakashinda. Mtaji wao ni umaarufu wa wazazi wao siyo uwezo wao.

Kama ilivyo kwa watoto wengine wa wanasiasa, kijana huyo anayetoka pia katika familia ya wanasiasa hana mashiko yake mwenyewe ndiyo maana hata wapigadebe wake ni wanasiasa ambao wana malengo ya miaka kadhaa ijayo. Labda kwa sasa kwa vile anawania nafasi hiyo, atadai anaisaidia Majimaji iliyoko kwenye sita bora.

Pigo lingine kubwa anaokabiliana nao ni kukosa kwake baraka kutoka kwa wazee wa soka mkoa wa Ruvuma inakotoka klabu ya Majimaji iliyomdhamini. Msimamo wa Chama cha Soka Mkoa wa Ruvuma (FARU) ambao umetangazwa na mwenyekiti wake Joseph Mapunda ni kwamba anayefaa kwa nafasi hiyo ni Ramadhani Nassib.

FARU hawataki unafiki, udugu usio na maslahi katika soka. FARU wanadai wanampigia debe mtu ambaye atakuwa wa msaada kwa soka ya nchi nzima si Majimaji tu.

FARU hawataki kuugua ugonjwa walionao baadhi ya wadau wa michezo hasa wa mikoani wa kudhani vijana kutoka Dar es Salaam wanajua zaidi soka kuliko wao. Bila hata sababu za msingi, utaona wanawachagua wenyeji wa mikoa hiyo waishio Dar es Salaam kuwa wawakilishi kwenye mkutano mkuu wa TFF au wenyeviti.

Singida waliwahi kumchagua Kassim Dewji kuwa mjumbe wa mkutano mkuu, Tabora wakaona anayefaa ni Aden Rage, Pwani wakamchagua Imani Madega kuwa mwenyekiti wao na sasa Hassan Othman ‘Hassanol’. Je, wamesaidiaje maendeleo ya soka ya mikoa waliyoombea kura? Soka la mikoa hiyo likoje?

Mikoa inatumika kama ngazi tu ya umaarufu wa baadhi ya watu kuelekea katika safu za kisiasa. FARU kwa kauli moja wamekataa kutumiwa kama kipazasauti cha Nchimbi ambaye hajulikani katika medani ya soka. Je, kwa msimamo huo, ajihesabu kuwa ameonyeshwa kadi nyekundu ‘red card’ katika uchaguzi huo utakaofanyika Februari 28, mwaka huu?

Kiubishi ubishi anaweza kukataa kuwa huo ndio mwisho wake na sababu kubwa si nguvu yake bali watu wanaombeba. Akifanikiwa atakuwa amejisogeza karibu na watu ambao hakuwa karibu nao awali.

Mbaya zaidi FARU ni kati ya vyama vya mikoa mitano; Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Lindi vilivyoamua kumchukulia fomu Nassib na vikaungwa mkono na mikoa mingine 12 iliyotangaza kumuunga mkono kijana huyo anayewania tena nafasi hiyo baada ya kupoteza nafasi kutokana na klabu iliyomdhamini awali Villa Squad ya Dar es Salaam kupoteza sifa.

Uzito mwingine kwa Nassib ni msimamo wa klabu kubwa na zenye mashabiki wengi nchini Simba na Yanga kuonyesha kumuunga mkono badala ya Nchimbi.

Wadau wa soka wanajua kwamba soka ya Tanzania imekuwa katika mtafaruku mkubwa miaka ya kuanzia 1993 ulipoingia uongozi wa FAT (sasa TFF) chini ya Muhidin Ndolanga na Katibu Mkuu, Ali Hassan Mwanakatwe.

Uongozi wa Ndolanga ambao baadaye ulikuwa na makatibu kama Ismail Rage na Michael Wambura ulikuwa na misukosuko mikubwa na mingi ilichangiwa na wanasiasa waliotafuta umaarufu kupitia soka.

Kampeni kali iliyofanywa na wadau wa soka mwaka 2004 ilifanikisha mwanasoka wa zamani wa kimataifa, kocha na msomi Leodegar Tenga kuchaguliwa kuwa rais. Aliingia na safu mpya iliyorejesha amani hadi leo.

Tenga ameifanya taasisi hiyo kuwa ya wadau wote na yenye jukumu la kuendeleza soka nchi nzima badala ya sifa binafsi na migogoro. Serikali imepewa nafasi kubwa kama mdau mkuu, lakini haijaachwa kuingilia maamuzi ya taasisi hiyo.

Jaribio lolote linalofanywa na wanasiasa kutaka kupigia debe wagombea wasio na chembe ya mpira kichwani itakuwa sawa na kuingiza virusi vya migogoro katika shirikisho hilo lenye utulivu mkubwa sasa. Vilevile wagombea wanaotumwa na watu walioko nje ya mduara wa soka hawawezi kuwakilisha mawazo yao bali ya waliowatuma.

Nafasi nyingine inayotarajiwa kujazwa katika uchaguzi huo itakuwa ya mjumbe wa kamati ya utendaji wa TFF kutoka kanda ya tano yenye mikoa ya Mbeya na Rukwa. Nafasi hiyo iliachwa na Theophil Sikazwe aliyefariki dunia Juni, mwaka jana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: