Marando, Slaa wamvaa Kikwete


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Mabere Marando

MWANASHERIA mashuhuri nchini na mwasisi wa mageuzi, Mabere Marando amesema, Rais Jakaya Kikwete hana nia njema ya kuleta katiba mpya, bali amejitumbukiza kuteka hoja ya katiba.

Akizungumza na MwanaHALISI juzi Jumatatu, Marando alisema, “Msimamo wa Kikwete hauna tofauti na ule wa mwanasheria wake mkuu, Jaji Frederick Werema. Ndiyo maana amekuja na hoja ya kuunda tume ya kurekebisha katiba, badala ya kuandika katiba mpya.”

Anasema kwa anavyokifahamu Chama Cha Mapinduzi (CCM), katu hakiwezi kusimamia mchakato wa kuanzishwa kwa katiba mpya kwa kuwa katiba iliyopo sasa inakinufaisha zaidi chama hicho.

“Yule Werema hana tofauti na bosi wake. Ukimsikiliza Kikwete vizuri, haraka utagundua kuwa anachokizungumza ndicho hicho anachokieleza Werema; kwamba anaunda tume ya kurekebisha katiba,” anaeleza.

Anasema kuunda tume ya kurekebisha katiba hakuna maana ya kuandika katiba mpya, na kwamba anachokifanya Kikwete ni  kuteka nyara hoja ya katiba ambayo imekuwa ikidaiwa na upinzani.

“Kikwete hawezi kukubali kuandika katiba mpya kwa kuwa katiba hii inambeba yeye na chama chake,” anasema Marando.

Kwa mfano, Marando anaeleza, Rais Kikwete hawezi kukubali wakuu wa mikoa na wilaya “kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi, kwa kuwa hao ndiyo wanaomsaidia kuiba kura.”

Anasema wala Kikwete hawezi kukubali mwenyekiti wa chama hicho kuachana na utaratibu wa kuchagua wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na watendaji katika mikoa.

Akizungumza na wananchi kupitia hotuba yake ya mwisho wa mwezi mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Kikwete aliahidi wananchi kuunda tume ya kusimamia marekebisho ya katiba.

Kauli ya Kikwete ilikuja siku chache baada ya mmoja wa waasisi wa CCM, Peter Kisumo kunukuliwa akitaka chama chake kuchukua uongozi wa kusimamia upatikanaji wa katiba mpya, vingevyo kitapitwa na wakati.

Akieleza kwa sauti ya upole kile alichoita, “janja ya Kikwete,” Marando alisema, anaamini kiongozi huyo wa nchi hawezi kuruhusu  wajumbe wa tume ya uchaguzi wakachaguliwa na Bunge.

Anasema, “Wala rais hawezi kukubali mawaziri kutoka nje ya Bunge. Kwa sababu, kuteua mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge kunamsaidia kuwa na serikali ya watu woga, wanaojipendekeza kwake, badala ya kuwatumikia wananchi.”

Anasema, “Kenya tayari wamefika huko. Wajumbe wa tume ya uchaguzi wanachaguliwa na bunge. Kule Malawi wamefika hatua kubwa zaidi. Mawaziri wanatoka nje ya Bunge na sasa wabunge wanasimama kama watu binafsi, kutetea wananchi wao.”

Naye Dk. Willibrod Slaa, katibu mkuu wa CHADEMA ameuponda uamuzi wa rais Kikwete kuunda tume kurekebisha katiba.

Amesema, “Mapendekezo ya Rais Kikwete ya kuunda alichoita Constitutional Review Commission siyo kilio cha waliowengi na wanaodai katiba mpya. Wanachotaka wananchi ni katiba mpya ambayo haiwezi kamwe kupatikana kwa njia ya Constitutional Review Commission,” anaeleza.

“Tusipoangalia kwa makini, Watanzania tutaingia kichwa-kichwa. Rais Kikwete amependekeza kuundwa kwa tume na siyo katiba mpya,” anaeleza.

Anasema katika historia ya taifa, hasa katika siku za karibuni, tume za aina hiyo ziliwahi kuudwa na viongozi waliotangulia, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

“Uzoefu wa tume za Mwinyi na Mkapa ni kuwa maoni yalikusanywa kwa upendeleo, hojaji zilipelekwa kwenye matawi ya CCM, halmashauri za wilaya… hatimaye serikali ikatoa mapendekezo ya vifungu vya kurekebishwa na vingine kuachwa. Ndivyo hivyo viraka tunavyoviona katika katiba ya leo,” anaeleza Dk. Slaa.

Anasema, “Katika nchi zote zilizoandika upya katiba au kutengeneza katiba yenye hadhi ya kuitwa Katiba ya wananchi, zilipitia njia ya National Constitutional Congress/Convention, ambako) inakubaliwa kati ya Serikali, Bunge, wadau mbalimbali na wananchi kupitia Baraza la Katiba.”

Anasema, “Baada ya chombo husika kuundwa, maoni ya wadau yanakusanywa kwa njia itakayokubalika. Baraza la katiba linakaa tena na kupitia maoni yote kipengele kwa kipengele na kukubaliana.”

“Tulichotaka sisi siyo Constitutional Review Commission chini ya Rais. Tume hiyo haikubaliki kabisa. Tunachotaka ni chombo cha
wananchi, kinachoweza kuwekewa utaratibu na Bunge, siyo mtu au wanatume wanaochaguliwa na rais, na watakaotoa ripoti yao kwa rais,” ameeleza.

Dk. Slaa amesema itakuwa hatari kubwa iwapo wananchi hawataelewa tofauti kati ya Tume ya Kikwete na Mkutano wa Katiba (National Constitutional Congress) ambao unadaiwa na watu wote wenye nia njema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: