Marando: Upinzani tumeaibisha


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Tumekipa upenyo Chama Cha Mapinduzi
Mabere Marando

MABERE Marando, mmoja wa waasisi wa mageuzi ya vyama vingi nchini, amesema ni aibu kwa vyama vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea katika sehemu nyingi nchini katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita.

Amesema kutosimamisha wagombea kumekipa upenyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) hata mahali ambapo wananchi waliishakata tamaa na walihitaji mabadiliko.

Vyama vya upinzani, amesema havina haki ya “kulalamikia ushindi wa chee wa chama tawala katika maeneo ambayo wao wameshindwa kusimamisha wagombea.”

Marando ambaye aliasisi chama cha NCCR-Mageuzi na kuwa mbunge kwa kipindi kimoja (1995 – 2000) na kufuatia kuwa mbunge wa baraza la kutunga sheria la Afrika Mashariki, amesema kutoshiriki uchaguzi kunaua demokrasi waliyotolea jasho.

Katika mahojiano maalum na MwanaHALISI, Jumatatu, kufuatia CCM kuzoa viti vingi vya chee, Marando alisema ni wajibu wa vyama vya upinzani kuzama vilivyo kwa wananchi ili kujijengea nguvu.

Alisema yeye na wenzake walifanya kazi nzito ya kudai mageuzi na walifanikiwa na kwamba sharti mageuzi hayo yapelekwe chini (vijijini) waliko wananchi ili wayaunge mkono na kuyakomaza.

“Tulidai demokrasia kwa nguvu nyingi na tukaipata. Kazi haikuwa rahisi kama wengine wanavyofikiri. Tulikuwa wengi lakini tukabaki wachache tuliokuwa na msimamo wa mageuzi ya kweli. Sasa kuyalinda mageuzi kunahitaji umakini,” alisema.

Amesema sheria ya uchaguzi inasema wazi kwamba kwa pale ambapo mgombea hakupata mshindani, basi msimamizi wa uchaguzi wa eneo husika atamtangaza kuwa ndiye mshindi, bila ya kulazimika kupiga kura.

Kuhusu wajibu wa viongozi wa upinzani katika kukuza demokrasia ya vyama vingi, Marando amesema, “Lazima vyama vya upinzani vizame kwenye vitongoji na vijiji. Vikishindwa kufanya hivyo na hatimaye kushindwa kuweka wagombea, visilaumu yeyote.”

Amelaumu alichoita “siasa za magazetini na kwenye televisheni” kwamba haziwezi kuleta tija kwa ukuaji wa mfumo wa vyama vingi. “Viongozi wanapaswa kutembelea wananchi huko waliko – vijijini na siyo kubaki tu mjini na kuendesha siasa kupitia magazetini,” alisema.

Kuhusu madai ya upinzani kuwa wanakosa nguvu ya kujiimarisha kwa sababu ya ukata, Marando ambaye ni mwanasheria kitaaluma anayeendesha kampuni ya uwakili, alisema hakubali kisingizio hicho kwani ni kazi ya viongozi kupanga jinsi ya kupata fedha.

“Wewe ukiwa kiongozi jua kwamba ndio kazi yako kutafuta fedha; unahangaika. Kwani mbona sisi tulifanikiwa kupata fedha tukasonga mbele?” aliuliza.

Marando alizungumzia pia mfumo wa uchaguzi nchini na kulaumu kuwa unaua demokrasia kwa kuwa wasimamizi wote wa uchaguzi wamekuwa wakitoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alisema ni mfumo mbaya unaonyima fursa sawa katika uwanja wa mapambano miongoni mwa vyama vya siasa.

Amesema, “Hatuwezi kukuza demokrasia namna hii. Wasimamizi wote ni makada wa CCM hata wale wasiokuwa makada wanatishwa na kulazimishwa  kutumika kupendelea chama tawala.”

“Hapa lazima nikiri kuwa mazingira ya uchaguzi bado ni mabaya nchini petu. Hili ni jambo linalohitaji kutazamwa upya vinginevyo badala ya demokrasia kuimarika, itazidi kudhoofika,” alisema.

Marando amesema amesikitishwa na upinzani kupoteza hata mitaa ambayo umekuwa ukishikilia katika serikali za mitaa – vitongoji na vijiji, na kutoa mfano wa jimboni kwake, Rorya ambako upinzani umeshindwa kulinda ngome yake.

Mahojiano na Marando yalitokana na matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumapili ambapo katika maeneo mengi ya nchi CCM ilipata ushindi bila ya kupigiwa  kura kwa kuwa vyama vya upinzani vimeshindwa kusimamisha wagombea.

Wakati CCM imepata ushindi kwenye maeneo mengi ya nchi bila upinzani wowote, yapo maeneo ambako imepigwa kumbo kwa kupoteza hata walipokuwa wakishikilia.

Mfano hai ni wilayani Mafia, ambako CCM imepigwa mweleka katika vijiji vinane kati ya 20 vilivyopo ndani ya wilaya hiyo. Kati ya vijiji hivyo vinane, upinzani umefanikiwa kushinda kijiji muhimu cha Baleni ambako ni nyumbani kwa mwanasiasa mkongwe wilayani humo, Ayuob Kimbau.

Vilevile, upinzani umeshinda vijijiji vitano katika tarafa ya Kaskazini ambako kunatakwa kulikuwa ngome kuu ya CCM. Kote huko Chama cha Wananchi (CUF) ndiyo walioitesa CCM.

Lakini kituko kikubwa zaidi ni katika jimbo la Chilolo mkoani Iringa, ambako upinzani umeshinda nyumbani kwa mbunge wa sasa Profesa Peter Msola.

Kiti cha nyumbani kwa Profesa Msola ambaye pia ni mjumbe Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, imenyakuliwa na Chadema.

3
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: