Masalia ya Zitto yapukutishwa CHADEMA


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ililazimika kujigeuza mahakama ili kusikiliza malalamiko dhidi ya wagombea nafasi ya uenyekiti wa baraza la vijana la chama hicho (BAVICHA).

Katika kusikiliza malalamiko hayo, Kamati Kuu iliwateua wanasheria wake mashuhuri, Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari kuwa majaji wa kuendesha kesi ya Habibu Mchange aliyekuwa anawania nafasi ya mwenyekiti.

Mchange ambaye anajitambulisha kuwa ni mfuasi wa naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe lilalamikiwa na mwenyekiti wa BAVICHA mkoani Mwanza, Liberatus Mlebele kukiuka maadili ya uchaguzi, ikiwamo kusafirisha wajumbe wa mkutano wa uchaguzi kutoka mikoani hadi Dar es Salaam.

Ndani ya CC, Mchange alilazimika kujibu tuhuma moja baada ya nyingine ikiwamo malalamiko ya kushindwa kuwajibika yaliyofunguliwa na katibu wa BAVICHA jimbo la Kigamboni.

Katibu huyo alimtuhumu Mchange kushindwa kutimiza wajibu wake kwa kile alichoeleza, “Tangu achaguliwe kushika nafasi ya mwenyekiti wa BAVICHA wilayani humo hajahudhuria vikao.”

Mjumbe mmoja wa CC amedokeza gazeti hili kuwa Mchange ambaye alionekana kuwa na wafuasi wengi, alikatwa kwa kuwa alishindwa kujitetea mbele ya mahakama ya CHADEMA.

Kwa mfano, kati ya 20 Mei na 25 mwaka huu, Mchange alituma zaidi ya Sh. 2, 561,000 kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa vijana kutoka katika mikoa mbalimbali nchini. Fedha hizo zilitumwa na Mchange mwenyewe kupitia mtandao wa M-Pesa na Tigo Pesa.

Namba ya Mchange iliyotumika kusambaza fedha hizo, ni 0658 178678. Alianza kutapakanya fedha kwa wajumbe 11 Mei 2011 saa 10:44.58 ambapo kiasi cha Sh. 28,500 zilitumwa kwa mmoja wa wajumbe wenye simu Na. 0659 374206.

Baadaye saa 11:04.24 alituma Sh. 15,500 kwenda Na. 0659 374206 na kisha 20 Mei 2011 saa 14:03.04 alituma Sh. 19,000 kwa mwenye Na. 0713 866650.

Tarehe 23 Mei 2011 saa 10:56.06, nyaraka zinaonyesa Mchange alituma Sh. 50,000 kwenda kwa mwenye Na. 0713 867745; tarehe 21Mei 2011 saa 11:54.47 alituma Sh. 40,000  kwenda kwa mwenye Na. 0717 268576 na saa 12:41.48 alituma Sh. 81,000  kwa mwenue Na. 0714 038536.

Wengine waliotumiwa fedha na Mchange; ni wenye Na. 0712 511508 aliyetumiwa Sh. 26,000 na mwenye Na. 0713 606169 aliyetumiwa Sh. 10,000 ambaye alitumiwa fedha hizo, saa  22:24.31.

Nyaraka za M-PESA zinamuonyesha Mchange akimtumia Peter Shiyo, mwenyekiti wa BAVICHA wilayani Maswa Sh. 50,000. Fedha hizo zilitumwa 23 Mei 2011 saa 16:39.

Tarehe hiyo 23 Mei 2011 saa 18:48, Mchange alituma kiasi cha Sh. 30,000 mwenyekiti wa vijana wilaya ya Singida Mjini, Wilfred Kitundu.

Aidha, siku hihiyo Mchange akitenda kama karani wa benki alituma Sh. 150,000  kwa mwenyekiti wa baraza hilo mkoani Mwanza, Liberatus Mlebele.

Mara baada ya kupokea fedha hizo, Mlebele aliwasilisha malalamiko kwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa akimtuhumu Mchange kumshawishi kwa njia ya rushwa ili amchague kuwa mwenyekiti.

Katika barua yake hiyo, Mlebele pamoja na mambo mengine alisema, “Ninakuandikia kwa nia njema kabisa ya kulinda hadhi ya chama chetu nikiomba maelekezo yako kama mtendaji mkuu wa chama.”

Anasema, “Tarehe 28 Mei 2011 Baraza la Vijana wa chama chetu litafanya uchaguzi wa viongozi wake wa kitaifa. Je, sisi wajumbe tumegharamiwa na chama ama wagombea kufika Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi huu?

Alisema, “Ninauliza hivi kwa sababu tayari mmoja wa wagombea ameshaniagiza kufika Dar es Salaam kwa gharama zake ili kukagua hoteli ambayo wajumbe wa mkoa wangu na kwingineko watafikia hali ambayo ninaihesabu kama rushwa.”

Mlebele alisema katika barua yake, “Niko tayari kutoa vielelezo sahihi juu ya kitendo hiki kama itabidi, ili kulinda hadhi ya chama chetu dhidi ya watu hatari kama hawa.”

Alisema, “Kwa kuwa mimi binafsi sipendi rushwa na siwezi kuvumilia vitendo vya rushwa na kwa kuwa natambua chama chetu kimekuwa kinara wa kupambana na rushwa nchini, ninaomba kamati kuu ichukue hatua stahiki dhidi ya mtu huyu ili kulinda hadhi ya baraza na chama chetu mbele ya wananchi.”

Ni maelezo hayo ya Mlebele yaliyozika ndoto za Mchange kuwa mwenyekiti wa BAVICHA. Taarifa zinasema Dk. Slaa aliwasilisha malalamiko yote mbele ya wajumbe wa CC. Barua ya Mabele iliwasilishwa kwa Dk. Slaa, 26 Mei 2011.

Taarifa zinasema kabla ya CC kujigeuza mahakama ya kusikiliza shauri hilo, mjumbe mmoja alinukuliwa akimtetea Mchange. Hata hivyo, alizimwa na Dk. Slaa aliyesimama kidete kutaka chama chake kichunguze suala hilo na kichukue hatua.

Katika barua yake, Mlebele anasema alifikia katika hoteli ya Bondeni One iliyoko Magomeni. Anamtaja Mchange kuwa ndiye aliyelipa fedha hizo. Alitoa nakala ya kitabu cha wageni kuthibitisha kuwa fedha hizo zililipwa na aliyemteja.

Mchange alikiri mbele ya wajumbe wa CC kuwa ni kweli kwamba simu iliyotajwa kupeleka fedha ni yake; alimhonga Mlebele kiasi kilichotajwa, alilipia sehemu ya gharama za hoteli na alikiri kumuagiza akusanye wajumbe wa mkutano wa uchaguzi.

Kamati kuu ya CHADEMA ilipitisha majina ya wagombea tisa katika nafasi ya mwenyekiti na kisha kukasimu madaraka yake kwa kamati ya wazee kwa hatua nyingine inazoona zinafaa.

Ni kupitia kamati hiyo, ndiko wagombea wengine watatu walifyekwa. Waliopatwa na panga la kamati hiyo iliyokuwa chini ya Edwin Mtei, Bob Makani na mwanasheria wa chama hicho, Mabere Marando, ni Mtela Mwampamba, Bernard Saanane na Grayson Nyakarugu, huku John Heche akionywa na na kuelezwa ikibainika alifanya vitendo kinyume cha maandili, atavuliwa madaraka.

Wote waliokatwa walipatikana na makosa ya rushwa, kutoaminika, kupanga matokeo, makundi na kutumiwa na watu wa kutoka nje ya baraza la vijana.

Akifanya marejeo ya kilichofanyika Jumamosi katika uchaguzi huo uliofanyika ukumbi wa PTA Sabasaba, Temeke, jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema chama chake kimeweza kunasua mitego yote ya rushwa iliyopandikizwa na CCM.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: