Masauni: Mbegu ya viongozi iliyooza


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 26 May 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Hamad Masauni Yussuf

HATIMAYE yametokea. Hamad Masauni Yussuf ameng’olewa uongozi ndani ya Umoja wa Vijana (UV-CCM). Hivyo ndivyo tuliripoti miezi miwili iliyopita.

Gazeti hili liliandika kuwa ndani ya UV-CCM kuna mgogoro wa uongozi unaohatarisha uhai wa uenyekiti wa Masauni. Tulitaja hata vinara wa mkakati wa kumng’oa Masauni katika kiti chake.

Makamu mwenyekiti Beno Malisa, Ridhiwani Kikwete na naibu katibu mkuu wa UV-CCM Zanzibar, Mohammed Moyo, ndio walitajwa kuwa vinara wakuu katika njama za kumwangamiza Masauni.

Mara baada ya gazeti kufichua njama hizo, viongozi wa juu wa umoja huo na chama chao, waliitisha mkutano na waandishi wa habari.

Humo walishambulia gazeti kwa kusema “limezoea kuandika uwongo.” Hata hivyo, hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyesema gazeti liliandika uwongo huo mara ngapi, lini na wapi?

Hawakusema, kwa mfano nani ambaye amefungulia gazeti kesi mahakamani na kulishinda kwa kukashifiwa uwongo. Kilichosimamia ni matusi na madai ya jumla.

Hata katibu mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba, hakubaki nyuma. Alinukuliwa akisema, “MwanaHALISI limekuwa na tabia ya kugombanisha viongozi wa chama na serikali; ndani ya UV-CCM hakuna mgogoro wowote unaohatarisha uenyekiti wa Masauni.”

Makamba na UV-CCM hawakuishia kushambulia tu, walitumia hadi fedha za umma kulipia matangazo kwenye magazeti kwa kile umoja ulichoita, “Taarifa ya Ufafanuzi.”

Lakini ni wiki iliyopita, hata kabla wino uliofichua njama za kumng’oa Masauni haujakauka, Baraza Kuu la UV-CCM, lililokutana mjini Iringa, limetekeleza kile kilichokuwa kikikanushwa.

Limemuondoa Masauni katika nafasi yake. Mkutano uliomuangamiza Masauni kisiasa ulihudhuriwa na wote waliokuwa wamejitokeza kukana wakati huo; akiwamo Makamba.

Hadi sasa, hakuna maelezo ya kutosha yaliotolewa kuhalalisha hatua ya Masauni kujiuzulu.

Hata Rais Jakaya Kikwete, aliyezungumza na wajumbe siku moja baada ya Masauni kujiuzulu na bila Masauni mwenyewe kuwepo, hajaweza kuzima kiu ya wengi ya kutaka kujua kilichotokea.

Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa gazeti kushambuliwa na watawala. Orodha ya mashambulizi ni ndefu.

Kwa mfano, mara baada ya gazeti hili kuripoti kwa ufasaha kashfa ya mkataba wa kinyonyaji wa kitega uchumi kati ya UV-CCM na mwekezaji, Edward Lowassa, mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa UV-CCM aliibuka, kukana na kukandia gazeti.

Lowassa alitishia hata kupeleka gazeti mahakamani kwa madai kuwa limemsingizia uwongo. Mpaka sasa, Lowassa hajapeleka shauri lake mahakamani kama alivyoahidi.

Lakini mwezi mmoja baada ya kufichuka kwa taarifa hizo, Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, ilikiri Lowassa kusaini mkataba huo bila kufuata taratibu. Hatimaye iliunda Kamati kuchunguza mkataba wa Lowassa.

Si hivyo tu. Ni MwanaHALISI lililoripoti kwa kina na ufasaha kuwapo kwa mkataba wa kinyonyaji wa kufua umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC).

Kila hatua ambayo gazeti lilikuwa likionyesha, watawala walijitokeza kukana. Lakini ukweli ulipodhihirika, Lowassa alibakia kujiandikia historia binafsi.

Vilevile, ni gazeti hili lililofichua uhusiano wa mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na kampuni ya Kagoda Agriculture Lilimted inayodaiwa kukwapua mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Gazeti lilichapisha hata maelezo ya hati ya kiapo yaliyotolewa na wakili wa mahakama kuu, Bhydinka Sanze, mbele ya Kamati ya Rais iliyoundwa kushawishi wezi kurejesha fedha walizoiba.

Hata pale tulipoandika kuwa mtoto wa Rais, Ridhiwan Kikwete, anaweza kutumika kudhoofisha baba yake kisiasa, hatukueleweka. Leo, wenye akili timamu wamethibitisha tulichokuwa tukisema.

Turejee kwa Masauni. Sasa si mwenyekiti tena wa UV-CCM. Hakujiuzulu kwa hiari kama ambavyo Makamba na wenzake wanavyotaka kuaminisha dunia. Amejiuzulu chini ya shinikizo kubwa la viongozi wa CCM na wale wa vyombo vya dola.

Kwanza, siku ambayo Kamati ya Utekelezaji ya UV-CCM ilikuwa inakutana mjini Iringa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Iwapo kweli itathibitika Masauni ameghushi nyaraka ili kudanganya umri, tutamuondoa.”

Hapa Chiligati alikuwa anaandaa mazingira ya Masauni kujiuzulu ili kuepuka rungu la dola. Lakini ni Masauni huyuhuyu anayeambiwa amejiuzulu kwa hiari na anayedaiwa “kuchukua baadhi ya vijana wenzake na kuwapeleka Iringa” ili wamtetee.

Huo ndio ulikuwa msingi wa kauli za “tutarudi na Masauni wetu yuleyule.” Walijiapiza kumtetea.

Hata kauli ya Rais Kikwete kwa wajumbe wa Baraza imedhihirisha kuwa Masauni ameng’olewa katika nafasi yake kwa shinikizo kutoka juu.

Hii ni kwa sababu, hata kama madai kwamba Masauni alitenda jinai, hakuna utamaduni wa kuwajibishana ndani ya chama hicho.

Hata ndani ya serikali ya Kikwete kuna baadhi ya mawaziri na wabunge wanaotuhumiwa kughushi vyeti vya elimu, lakini hakuna aliyechukuliwa hatua hadi sasa.

Lakini kubwa ni hili. Kusingekuwa na njama za kumwangamiza Masauni, asigeondolewa katika nafasi yake. Wala Kikwete hawezi kusema kuwa hakujua kama Masauni alighushi umri.

Vyombo vyote vya dola viko chini yake. Usalama wa Taifa, Polisi, Uhamiaji, Magereza na vingine vyote, vinaripoti kwake. Hivyo kama vitajitetea kuwa havikujua kuwa Masauni ameghushi umri, basi vitakuwa vimeshindwa kazi.

Kwanza, ni kwa sababu, Masauni ni mwajiriwa serikalini. Taarifa zake za lini amezaliwa na wapi, zinapatikana kwa urahisi.

Pili, Masauni ni mtoto wa Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Masauni Yussuf Masauni. Masauni huyu wa ZEC anajua kanuni za UV-CCM. Anajua kuwa mwanae amezaliwa miaka 37 iliyopita.

Masauni huyu anafahamu kanuni za utumishi na misingi ya maadili ya viongozi wa umma. Mbali ya kuwa mwenyekiti wa ZEC, alikuwa ofisa wa ngazi ya juu katika Idara ya Uhamiaji Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, isingekuwa rahisi kwake kukubali mwanae kugombea bila kuhakikishiwa usalama wake.

Ukiacha baba yake, vyombo vya dola vilikuwa wapi wakati Masauni anatenda jinai hiyo ambayo Kikwete anasema hakuifahamu?

Nani atasema kuwa Kikwete aliyesheheni vyombo vya uchunguzi hakujua hilo, na kwamba amegundua baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo?

Msaidizi Na. 2 wa Kikwete – Makamu Mwenyekiti wa CCM na rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alikuwa wapi wakati Masauni anagushi nyaraka zilizoingiza nchi katika kashfa?

Idara ya Usalama wa Taifa ndani ya chama chake ilikuwa wapi wakati haya yanatendeka?

Viongozi wakuu wa UV-CCM na hata chama chenyewe akiwamo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salehe Ramadhani Feruzi, walikuwa wapi?

Kama madai ya Kikwete kwamba hakujua kilichotendeka yana ukweli, basi kuna mambo mawili.

Kwanza, udhaifu wa serikali na vyombo vyake; lakini pili, imedhihirisha kuwa Kikwete anaweza kudanganywa na yeye anadanganyika hadi kufikia kupandikiza watu wasiokuwa na sifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: