Maswahiba wa kisiasa wageukana Australia


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Julia Gillard

HATUA ya chama cha Labour nchini Australia kumtoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu, Kevin Rudd, na kumpa nafasi hiyo swahiba wake mkubwa, Julia Gillard, imewashtua wengi ndani na nje ya nchi hiyo.

Wanasiasa hao wawili ndiyo waliofanya kazi kubwa ya kumbomoa kisiasa na hatimaye kumbwaga mtangulizi wa Rudd, Michael Howard, kutoka chama hasimu cha Conservative miaka minne iliyopita.

Lakini sasa, wakati dunia nzima ikifahamu kwamba pengine Rudd ndiye mwanasiasa anayekubalika zaidi nchini humo, wanamikakati wa chama hicho wameamua kumng’oa kabisa madarakani.

Nyota ya Rudd iling’ara zaidi kimataifa mwaka jana wakati alipokuwa miongoni mwa wazungumzaji wakubwa wakati wa mkutano wa dunia wa masuala ya tabia nchi (Climate Change) uliofanyika jijini Coppenhagen, Denmark.

Australia, miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi, ilikuwa miongoni mwa nchi zilizopigania sana kuwapo kwa mabadiliko katika mkataba wa Kyoto na Rudd ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu.

Ilifikia wakati hata Rais Barack Obama wa Marekani alipata kutamka kwamba kati ya viongozi wote duniani, ni Rudd pekee ambaye yeye anaweza kuzungumza naye na wakaelewana vizuri kuhusu mambo mbalimbali yakiwamo yale ya tabia nchi.

Hata hivyo, ndani ya Australia, hali ya kisiasa ya Rudd ilikuwa ikienda mrama kila kukicha. Alikuwa akishutumiwa kwa mambo mengi ambayo chama chake kilihofu yanaweza kukisababishia matatizo katika siku za mbele.

Rudd alikuwa akishutumiwa kwa mambo makubwa mawili. La kwanza lilikuwa ni hatua yake ya kuahirisha mpango wa ulipaji fidia kwa makampuni makubwa yaliyokuwa yakitajwa kuhusishwa sana na mabadiliko ya tabia nchi nchini humo.

Wakati alipokuwa akikampeni ili achaguliwe kuongoza nchi hiyo, Rudd alikuwa ameahidi kwamba mara atakapoingia madarakani ataamuru makampuni makubwa yanayoongoza kwa uchafuzi wa mazingira yalipe fidia ya uharibifu huo.

Lakini hadi sasa, takribani miaka mitatu tangu alipoingia madarakani, Rudd hajatekeleza ahadi yake hiyo na kauli zake za hivi karibuni zilikuwa zikionyesha kana kwamba alikuwa ameutekeleza kabisa mpango wake huo.

Wengi wa wananchi wa Australia waliokuwa wamemchagua walifanya hivyo kwa matarajio kwamba yeye ni mtetezi mkubwa wa mambo ya mazingira na hatua yake ya kutotekeleza ahadi yake hiyo kuu ilikuwa ni sawa na matusi kwa wapiga kura wake.

Jambo la pili linalotajwa kummaliza zaidi kisiasa Rudd inadaiwa ni tabia yake ya kupenda kujisikia na kutozungumza vizuri, akidaiwa kuzungumza kwa dharau kubwa.

Ilifikia hatua vyombo vya habari vya Australia vilimpachika mwanasiasa huyo jina la “Fidel Castro wa Australia” kutokana na tabia yake ya kupenda kuzungumza kwa muda mrefu kana kwamba anatoa mhadhara kwa wanafunzi.

Ilifikia wakati, wanadai wapinzani wake wa kisiasa, mwanasiasa huyo alifikia hatua ya kujiona ana ufahamu na upeo mkubwa mno kulinganisha na raia wote wa nchi hiyo.

Mambo hayo mawili ndiyo yaliyofanya umaarufu wa Rudd ndani ya Australia uporomoke kwa kiwango ambacho wengi nje ya nchi hiyo walishindwa kukifahamu.

Kushuka kwa umaarufu wa Rudd kulichukuliwa kama jambo la hatari kwa chama cha Labour ambacho ndiyo kwanza kimeshika madaraka baada ya kuwekwa kando kwa muda wa mrefu na mahasimu wao wa Conservative.

Na alikuwa ni mwanamama Julia ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumza hadharani kwamba umefika wakati kwa Rudd kuachia ngazi kwa vile anaweza kukigharimu chama chake.

Julia alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa Australia, wadhifa alioupata kutokana na kazi ngumu alioufanya kushirikiana na Rudd kumng’oa madarakani Howard aliyekuwa swahiba mkubwa wa utawala wa George W. Bush wa Marekani.

Mwanamama huyo alikuwa amempa Rudd fursa ya kujiuzuli kimyakimya katika mazungumzo yao binafsi nyumbani kwa aliyekuwa waziri mkuu huyo lakini hoja yake ikakataliwa.

Rudd alikuwa na mawazo kwamba hakukuwapo na sababu ya maana kwake kuachia ngazi kwa vile hakuna kiongozi ambaye amewahi kutimiza ahadi zake zote alizowapa wananchi na pia anayependwa na wananchi wote.

Kutokana na msimamo huo wa mtu aliyekuwa swahiba wake mkubwa, Julia aliongea na wabunge wa chama chake na kuomba wapige kura kuamua iwapo Rudd aendelee na cheo chake au yeye aokoe jahazi.

Awali, Rudd alikubaliana na ombi hilo la Julia lakini baada ya kuzungumza na wabunge waandamizi wa chama chake, alibaini kwamba hakuwa na uwezekano wa kumshinda mwanasiasa huyo mwanamke.

Julia ni mwanasheria kitaaluma na kuna imani miongoni mwa wengi wa wananchi wa Australia kwamba ana kipaji cha aina ya pekee cha kuzungumza kati ya wanasiasa wote waliopo nchini humo kwa sasa.

Ndani ya Bunge la Australia, Julia amekuwa ni kivutio kikubwa wakati wowote anapozungumza; akijenga hoja nzito katika suala linaloonekana kuwa jepesi na akiweka utani katika jambo linaloonekana kuwa gumu.

Mama huyo alikuwa amepania kuwa mwalimu wa shule ya msingi kutokana na kuvutiwa kwake sana na mwalimu wake aliyemfundisha katika hatua hiyo wakati alipokuwa mdogo.

Jambo la ajabu ni kwamba ni mwalimu wake huyo aliyemvutia kuutaka ualimu ndiye huyohuyo aliyemshauri kwenda kusomea sheria wakati atakapokuwa mkubwa.

“Ni jambo la kushangaza kidogo. Wakati nilipomwambia mwalimu wangu kwamba nataka kuwa mwalimu yeye akaniambia nitafaa kuwa mwanasheria. Akaniambia kama angekuwa na uwezo wa kujieleza na kujenga hoja kama niliokuwa nao mimi, angekuwa mwanasheria,” alisema Julia katika mazungumzo yake na vyombo vya habari mwaka juzi.

Kwa kuwa kwake Waziri Mkuu, Julia ameweka rekodi mbili. Kwanza ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini humo na pili kwa vile hana mume hadi sasa, kuwa mseja (bachela) wa kwanza kushika wadhifa huo pia.

0
No votes yet