Matatizo mengine CHADEMA mnajitakia


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Willibrod Slaa

UCHAGUZI mkuu wa kuchagua viongozi wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) umekuja na mambo yake. Mengine yalitarajiwa na mengine hayakutarajiwa.

Kwa mfano, miongoni mwa yaliotarajiwa ni maneno, tetesi na minong’ono na malalamiko ya kila aina katika mtandao, kwamba baadhi ya wagombea walikuwa wanabebwa na viongozi wakuu wa chama.

Jingine ambalo lilitarajiwa, ni kampeni zisizo sahihi - nje ya wakati – na ushawishi wa aina fulani hasa kwa kutumia mitandao ya intaneti, simu na vikao vya vilivyoendeshwa na baadhi ya wabunge na viongozi wengine ndani ya chama. Wanafahamika hata kwa majina na mahali ambako vikao hivyo vilifanyika.

Yale ambayo hayakutarajiwa ni ushupavu mkubwa ulionyeshwa na Kamati ya Wazee ambayo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi. Kamati hii imesimamia uchaguzi huu kwa kufuata kanuni na taratibu zote zilizotakiwa ikiwa ni pamoja na kuengua wagombea waliopatikana na makosa ya ukiukaji wa maadili.

Katika kutekeleza jukumu hili, CHADEMA hakikuangalia sura ya mgombea, dini yake, kabila lake wala nani anayemuunga mkono.

Hata hivyo, kilichosumbua mchakato mzima wa uchaguzi huu ambao unaweza kutengeneza matatizo huko mbele, ni jinsi CHADEMA kinavyocheleewa kufanya mabadiliko, badala yake inatumia au inafuata mfumo unaotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kupata viongozi wake.

Tofauti kubwa iliyopo kati ya vyama hivyo viwili – CCM na CHADEMA – CHADEMA wanaweza kusimamia kile wanachokiamini. CCM hawawezi.

Mfumo wa kutumia kamati kuu (CC) ya chama kuchuja na kupitia majina ya wagombea. Hoja kubwa inayotumika kuhalalisha mfumo huu, ni ukubwa wa chama na hasa wingi wa wanachama kukutana na kupitisha majina ya wagombea.

Ukisoma katiba ya CCM na katiba ya CHADEMA zote zinaweka mkazo sana mtindo huu wa mnyororo kutoka chini kwenda juu. Ni mtindo wa vyama vya kisoshalisti ambavyo havina kawaida ya kuamini wananchi wao kuwa wanaweza kusimamiana na kutekeleza majukumu yao sawasawa.

Katika katiba ya CHADEMA, kamati kuu imepewa jukumu la “kusimamia utendaji kazi wa mabaraza ya vijana, wanawake na wazee.” Kwa maneno mengine, mabaraza haya yote yako chini na yanawajibika kwa kamati kuu.

Mfumo huu wa kamati kuu kusimamia mabaraza haya unaweza kuwa mzuri, hasa ikizingatiwa kuwa mabaraza haya si chama cha siasa, bali ni matawi ya ndani ya chama.

Lakini binafsi ninaupinga mfumo huu kwa kuwa mtindo huu unafaa kwenye nchi yenye chama kimoja ambako kwenye nchi kama hiyo utii na utulivu ni jambo kubwa zaidi na hivyo mnyororo wa utii unafuata kama mnyororo wa utii ulivyo katika jeshi.

Bali katika nchi yenye vyama vingi mtindo huu ni mtindo wa matatizo kwa sababu ushawishi wa kisiasa na matamanio ya madaraka na nafasi huzaa matatizo mara zote.

Haya tunayoyaona kwenye Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) na migongano ambayo imetokea sasa hivi huko Arusha na hata malumbano ambayo tumeyasikia mara kwa mara ni matokeo ya mfumo huu. Ni migongano ya maslahi ya kuweza kuwa katika nafasi ya madaraka. Mfumo ulivyo hutengeneza migongano hii.

Hivyo, linapokuja suala la kupata uongozi wa jumuiya wenye mtandao wa kitaifa watu wengi wenye malengo tofauti hujitokeza. Chama kama CHADEMA ambacho kimejaribu sana kujipambanua kwa kumulika utawala uliyopo ni lazima kiwe kinalengwa na watu wabaya na hata watu ambao wanafikiria labda ni kupitia chama hicho matamanio yao ya kushika madaraka yanaweza kutimia.

Binafsi sielewi kwanini CHADEMA hawakutengeneza mfumo uliopo ambao ungeruhusu wagombea wa nafasi mbalimbali wanajulikana mapema zaidi, wanachujwa na kufanya kampeni katika mazingira ya uwazi, kuliko utaratibu huu ambao umepelekea mikutano ya uchaguzi kumalizika usiku wa manane.

Ungeweza kutengenezwa mfumo mzuri ambao ungeifanya CHADEMA iwe tofauti sana na CCM katika kusimamia chama, kukiendesha na katika utafutaji wa viongozi.

Bila ya kuwa na mfumo mzuri wa kupata wagombea kuanzia ngazi za chini, kuwachuja, kuwapima na hata kuwapendekeza kwa nafasi mbalimbali basi matatizo makubwa yanaweza kutokea huko mbele.

Bila kutengeneza mfumo ambao utahahakisha ni wale tu ambao wamekuwa na mapenzi ya kweli kwa chama na wako tayari kukitumikia ndiyo wanaopewa nafasi ya kuongoza, badala ya kubeba hata wale wanaosukumwa na watu wa nje, chama hiki kinaweza kutumbukia katika mikono ya vibaraka huko tuendako.

CHADEMA hakiwezi kwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao kikiwa na mfumo huu; kinatakiwa kubuni mkakati mkuu wa mabadiliko ambayo yatakifanya chama kiwe cha wananchi kweli, chenye kujitegemea kiuongozi na ambacho kitazuia mizengwe ya watu wenye madaraka au ushawishi.

Lengo ni kuhakikisha kuwa CHADEMA siyo tu kinakuwa tofauti na CCM kwa kuangalia ujumbe wake kwa jamii au ilani yake, lakini kimfumo na kimtindo.

Hivi sasa haiingii akilini kwanini viongozi wajuu wa chama ndio hao hao, viongozi wa juu bungeni, na ndio hao hao wenye kusimamia ushawishi mkubwa katika mabaraza ya vyama na hata kusimamia utendaji mzima wa chama.

CHADEMA ni chama cha “Demokrasia na Maendeleo.” Mfumo wake lazima uoneshe demokrasia - yaani utawala wa watu; kanuni zake ni lazima zioneshe kuwa wanachama wana sauti ya mwisho na kuweka imani kwa watu wengi zaidi kufanya maamuzi kuliko kikundi cha watu wachache.

Nisieleweke kuwa nasema kusiwe na “kamati kuu” ninachokataa ni nguvu ambazo nimezikataa zamani sana katika kile nilichokiita wakati ule “jinamizi la CCM” kwani matatizo mengi ya CCM yanatokana hilo hilo dubwasha liitwalo “kamati kuu” na ambalo kwa kweli limetusababishia matatizo mengi sana ya kisiasa.

Ninachoogopa ni kuwa bila kuondoa hili jinamizi na kuweka madaraka katika vyombo vya kiutendaji (siyo vya wanasiasa) na tusipoangalia matatizo tunayoyaona ndani ya kamati kuu ya CCM, tunaweza kujikuta tunayarudia kwenye kamati kuu ya CHADEMA endapo itashika madaraka kama wengi wetu tunavyotarajia hilo kutokea miaka si mingi ijayo.

Tatizo ni kuwa ukishakosea msingi wa hesabu, matokeo yake ni kuwa wote mtapata jawabu lile lile - lenye makosa. Ukishakosea kanuni, unakosea na matokeo yake. CCM walipoingia kwenye vyama vingi hawakubadili mfumo wao wa kamati kuu; vyama vyote nchini navyo vimekopi mtindo huu huu. Matokeo yake wanarudia makosa yale yale. Kama ilivyo kwa CCM wasivyoona tatizo la mfumo waliouzoea, wapinzani nao wanaweza kujikuta wanashindwa kuachana na mfumo huu.

CHADEMA kama chama ambacho kina fikra mpya kama tunavyoona katika ilani yake yenye mvuto wa ajabu, inaitwa na historia kujiangalia na kuhakikisha inafanya marekebisho ya haraka na ya lazima ili yaendane na wito wake kizazi hiki.

Vinginevyo, tulioshika tamaa kwa huzuni kwa yale ambayo tunayoyaona, tutaanza kudondosha machozi kwa nafasi inayopotezwa.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: