MAUAJI TARIME: Mkuu wa wilaya ashitakiwa kwa Kikwete


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version

MKUU wa Wilaya (DC) wa Tarime, John Henjewele ametuhimiwa kubeba mwekezaji katika mgogoro kati ya wananchi wa Nyamongo na wamiliki wa mgodi wa dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Africa Gold ya Canada.

Katika barua rasmi kwa serikali, wenyeviti wa serikali za vijiji vitatu vya Kewanja, Nyangoto na Matongo vinavyouzunguka mgodi huo, Henjewele ametajwa kuwa ndiye kikwazo kikubwa kwa amani ya eneo la Nyamongo.

Wenyekiti Elisha Marwa Nyamhanga wa Kijiji cha Nyamongo, Itembe Nyamhanga Itembe wa Matongo na Tanzania Mtima wa Kewanja, wameeleza katika barua yao serikalini kuwa pamoja na Henjewele, polisi nao ni tatizo kubwa la amani mgodini hapo.

Tarehe 16 Mei 2011, polisi wilayani Tarime waliua watu saba kwa kuwapiga risasi kwa madai kuwa walikuwa wamevamia mgodi wa North Mara.

Mtu wa sita kufariki ni Wambura Kebacho wa kijjiji cha Mrito aliyefia hospitali ya Sungusungu. Mtu wa saba jina lake halijafahamika kwani, kwa maelezo ya wananchi, alifia kichakani.

“Polisi kama chombo cha usalama wa wananchi na mali zao wao ni tatizo kubwa kwenye migogoro hii,” imesema sehemu ya barua hiyo ambayo imekabidhiwa kwa viongozi kadhaa wa serikali akiwamo Waziri wan chi ofisi ya Rais, mahusiano ya jamii, Stephen Wasira.

Katika barua hiyo ambayo ilikabidhiwa pia kwa msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa mjini Mwanza mwishoni mwa wiki, viongozi hao wa vijiji wametoa masharti manne wanayotaka yatekelezwe.

Wanasema bila kutekelezwa kwa masharti hayo amani haitapatikana.

Masharti hayo ambayo ambayo yamo katika mkataba kati ya mgodi na wanavijiji, ni pamoja na mgodi kulipa asilimia moja ya mapato yake kwa vijiji, ujenzi wa hospitali yenye hadhi ya wilaya na ajira kwa wenyeji wa vijiji hivyo.

Mengine ni ujenzi wa chuo cha ufundi, malipo ya ada ya ardhi, kuunda mfuko wa dhamana (trust fund) kugharimia mradi wa maji kwa kila mwanakijiji na kujenga miundombinu ya barabara.

Masharti hayo yamo katika mkataba waliokubaliana kati ya muwekezaji na wananchi wa vijiji hivyo. Ulifungwa kabla ya kampuni hiyo kupewa leseni ya kuchimba dhahabu kwenye vitalu vilivyokuwa vikimilikiwa na vijiji hivyo.

Mgogoro wa sasa unatokana na hatua ya Henjewele kudaiwa kutumiwa na mgodi huo kulazimisha vijiji vipokee dola 100,000 ili wasaini mkataba mpya na mgodi na kuachana na mkataba wa zamani.

Wenyeviti hao walipokataa mkataba huo mpya kwa niaba ya wananchi, ndipo mkuu huyo wa wilaya akaagiza viongozi hao kunyang’anywa bunduki walizokuwa wakimiliki kihalali huku akidai wenyeviti hao wangezitumia.

DC anadaiwa kusema pia kuwa wenyeviti hao wanatumia vibaya bunduki hizo kuku akiwatuhumu kukwamisha mazungumzo na mgodi na kufanya kazi yake kuwa ngumu.

Katika barua hiyo ya tarehe 26 Mei mwaka huu, wenyeviti hao wawili wa vijiji kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja wa CHADEMA, kwa pamoja wamewaasa viongozi wa wilaya, mkoa na taifa kuacha kukumbatia wenye mgodi na badala yake wawe wanakutana na viongozi wa vijiji na serikali zao ili kutatua kero zao.

Haya yanatokea wakati kuna habari kuwa polisi kwa kushirikiana na maofisa usalama kutoka makao makuu wameanzisha mradi mpya wa kutafuta fedha kwa kuendesha kile wanachoita, “operesheni kubwa ya kuwatafuta watu wanaohusika na uvamizi katika mgodi wa North Mara.”

Tayari wakazi wa Nyamongo wanalalamika kwamba msako huo umelenga kuwakamata wakazi wa eneo hilo wenye fedha tu jambo ambalo linawabagua kwa sababu wavamizi wa mgodi kama wapo ni watu wa kawaida kutoka maeneo yote mkoani Mara.

“Waliopigwa risasi na kufa katika vurugu zile ni walikuwa wanatoka Bukenye, Sirari, Nyakunguru na Mugumu. Mtu kutoka Nyamongo alikuwa ni mmoja tu. Sasa kwa nini Wanyamongo tu ndio wakamatwe tena wale wenye fedha wanaoweza kuhonga polisi,” wanahoji.

Wanasema, “Lengo la operesheni hii ni kutafuta fedha na kuwabambikizia kesi watu wasiohusika.”

Mtoa habari huyo wa gazeti hili amewataja wafanyabiashara waliokamatwa kuwa ni Mhere Wangi wa kijiji cha Nyangoto, Mwita Nyamhanga Waigama wa Kijiji cha Kewanja na Maisa Ryoba Gituni maarufu kama ‘Wakwao’ wa kijiji cha Nyangoto.

Mkazi mwingine alisema ni kawaida ya polisi kukamata watu wengi kila kunapotokea vurugu kwenye eneo la Nyamongo na kwamba kila anayekamatwa hatoki kwa dhamana bila milioni mbili au tatu.

“Eeh muraa! Bolisi panyore omoryo (polisi wamepata mlo),” alisema mwananchi mwingine naye akidai hadi sasa watu watatu wote Wanyamongo wamekamatwa na kuhusihwa na vurugu zilizotokea hivi karibuni Nyamongo na kusababisha vifo vya watu saba.

Mara kadhaa, viongozi wote, ukiacha wale wa CHADEMA, wakifika Nyamongo huingia mgodini kwanza na baadaye kukutana na viongozi wa Nyamongo na wakati mwingine bila kuonana na viongozi wala wananchi kujua kero zao.

Taarifa zinasema baadhi ya polisi waliowahi kufanyakazi Nyamongo sasa wanahaha kufanya mawasiliano na washirika wao wa huko ili kuhakikisha hawatajwi kuwa walikuwa wakihusika katika uvamizi wa mgodi huo.

Imeelezwa kwamba polisi wanahonga kwa wakubwa wao ili kuhamishiwa Nyamongo ambako hupata isivyo halali zaidi ya Sh. 80,000 kila siku wanapokuwa zamu.

Taratibu hizi za kujipatia mafao ya nyongeza kutoka mgodini sasa zinafahamika kwa jina la “mchongo.”

“Polisi wote wa Nyamongo kutoka kanda maalumu ya polisi wanaoitwa tasiki fosi (task force) wanalipwa na kampuni ili kutupiga risasi na kutuua,” anaeleza raia mmoja wa Nyamongo kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Alipotakiwa kuthibitisha madai hayo, haraka aliuliza, “Kama sivyo, sasa wanalipwa pesa za nini huku wanauza mawe kama mainturuda (intruders) wanaovamia mgodi?”

Katika “mchongo” huo, polisi huruhusu magenge maalum yanayofahamika kwa askari wa jeshi hilo ili kuingia mgodini kuchimba dhahabu. Kila polisi mmoja hulipiwa kati ya shilingi 10,000 na 20,000 kulingana na hali ya upatikanaji (mawe) dhahabu kwa siku hiyo, amesimulia mtoa taarifa.

Ukisikia polisi amepiga mtu risasi, basi ujue mtu aliyepigwa risasi hakutoa pesa, amesema mtoa taarifa wetu na kuongeza, “Polisi ndio wanauza mawe na mchanga wa dhahabu kwa wachuuzi.”

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamongo anasema bila kutafuna maneno kuwa “polisi wakiacha michongo na mgodi ukatekeleza masharti ya mkataba ulioingia na vijiji, basi uvamizi mgodini utaisha.”

0
No votes yet