Mauaji ya raia basi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KWANINI mauaji ya ovyo ya raia wema yanaendelea nchini huku wahusika wakifanikiwa kutoroka mkono wa sheria.

Tunalalamikia mauaji ya aina tatu. Kwanza, yanayofanywa na vyombo vya dola kwa maana ya askari wa serikali na yale yanayofanywa na wanaoitwa wawekezaji.

Mauaji mengine ni yale yenye sura ya kisiasa.

Mapema mwaka huu, polisi waliua raia wawili (wa tatu mgeni kutoka Kenya) mjini Arusha; wakaua dereva wa gari, eneo la Kimara Mwisho mkoani Dar es Salaam. Wiki iliyopita, waliua raia kadhaa wilayani Tarime, Mara.

Utaratibu wa kisheria baada ya mauaji haya unaendeshwa kwa taratibu mno, tena mara nyingi ni mpaka vyombo vya habari vishinikize.

Hata haya mauaji ya aina nyingine mbili, hushughulikiwa kwa uzito vilevile. Badala ya polisi kuchunguza kitaalamu, hujiingiza katika malumbano.

Watalumbana na ndugu wa marehemu kama vile kupuuza wajibu wao kikatiba. Pale mauaji yanapokuwa yametekelezwa na askari, utasikia kauli zinazopishana zikitolewa na viongozi wa taasisi.

Mfano ni mauaji yaliyotekelezwa wiki iliyopita wilayani Tarime, kwenye mgodi wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG).

Wakuu wa Polisi Mkoa walisema waliouliwa ni wavamizi. Lakini alipofika Kamishna Paul Chagonja ambaye ni mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, akakana.

Ukweli unabaki: Polisi wa serikali wameua raia.

Mauaji mengine yalitokea mapema mwezi huu hoteli ya South Beach, Kigamboni, Dar es Salaam. Mkurugenzi mmojawapo wa hoteli, alishirikiana na watumishi kuangamiza raia mmoja kikatili.

Walimkamata, wakamtesa na kumvika tairi la gari. Wakamwagia petroli na kumlipua. Athari za mateso hayo, zilichochea kifo chake siku nne baadaye hospitalini.

Polisi walijivuta. Walipokamata watuhumiwa, wakafungua mashitaka yasiyokuwa ya mauaji hadi walipobanwa na watetezi wa haki za binadamu kufuata sheria.

Kuna mauaji ya kisiasa. Aliuawa Profesa wa Sheria, Juan Mwaikusya mapema mwaka huu. Juzi tu akauawa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Halmashauri ya Rungwe, John Mwankenja. Miaka michache nyuma aliuawa mwenyekiti wa CCM Uyui, mkoani Tabora, Mohamed Mgeleka.

Wakati umma unasubiri kuona hatua katika tukio la karibuni la wilayani Rungwe, hadi leo, hakuna aliyeshitakiwa kuhusiana na mauaji ya Prof. Mwaikusya. Ni uzito uleule kwa waliomuua mzee Mgeleka.

Tunaamini Polisi ya Tanzania ina wapelelezi makini hivyo ni muhimu wakaachiwa kufanya kazi kitaalamu na siyo kwa shinikizo.

Tungependa kuona raia wanalindwa kweli siyo kimaneno. Ni haki yao ya kikatiba.

0
No votes yet