Maximo, Phiri sasa wasingizia Ligi Kuu

MWISHONI mwa wiki iliyopita kocha mkuu wa timu ya soka ya Simba, Patrick Phiri alitoa kauli iliyoashiria kwamba Ligi Kuu ya Bara ni dhaifu.
Phiri kutoka Zambia alisema udhaifu huo umechangia kupata vipigo viwili katika michuano ya Kombe la Kagame. Alimaanisha Simba ilitwaa ubingwa wa soka Tanzania Bara katika ligi dhaifu.
Simba ilianza michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Atraco ya Rwanda mjini Kigali lakini ilikula kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Sofapaka ya Kenya na ikafunga kundi kwa kipigo cha 2-1 kutoka kwa URA ya Uganda.
“Simba ni bingwa, lakini ilicheza katika ligi mbovu ndiyo maana inapata shida kwenye michuano ya kuwania Kombe la Kagame,” alikaririwa Phiri akisema.
Siku iliyofuata kocha mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo alikaririwa na gazeti dada la hili, MSETO akiiponda pia Ligi Kuu ya Bara inayotoa wachezaji wa kucheza Taifa Stars.
“Sasa kama hatukuwa na ligi bora kuanzia kwenye klabu, hatuwezi kuwa na timu bora ya taifa au klabu inayoweza kushindana kimataifa kwa sababu, msingi utakuwa mbovu. Hivyo changamoto kwa timu zetu ni kuona jinsi ya kukuza soka kuanzia ngazi ya vijana,” alisema.
Hivi Phiri na Maximo anayekaribia kurejea kwao Brazil baada ya kumaliza mkataba wake Julai mwaka huu wanaona udhaifu huo leo? Hivi si makocha hawa waliosifu ligi na kudai Tanzania ina wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu?
Stars ilipopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Ivory Coast katika michuano ya CHAN mwaka jana, Maximo alisifu wachezaji na hata mfumo wa ligi ya nyumbani.
Rekodi zinaonyesha katika kipindi cha miaka minne, Taifa Stars imecheza mechi 61 za mashindano na kirafiki ambapo imeshinda 24, imetoka sare 18 na kufungwa 19. Maximo hakulalamikia mfumo wa ligi Stars iliposhinda.
Baadhi ya mechi ilizoshinda ni dhidi ya Burkina Faso, Zambia, Kenya, Uganda, Cape Verde, Sudan, DR Congo na imewahi kutoka sare na Senegal, Angola, Ghana kwa mechi zilizofanyika Dar es Salaam.
Naye Phiri aliyejipatia sifa baada ya kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa bila kupoteza mechi isipokuwa sare mbili, hakutoa malalamiko kama hayo Simba ilipoilaza Lengthens ya Zimbabwe na hata ushindi wa bao 2-1 jijini Dar es Salaam dhidi ya Haras el-Hadood ya Misri.
Je, inawezekana kuwa ligi yetu ni dhaifu ikilinganishwa na za DR Congo, Zambia, Rwanda, Burundi au Djibout?
Takwimu zinaonyesha Taifa Stars imewahi kupata ushindi japokuwa baadhi ya timu ziko juu kiubora katika chati ya FIFA.
Uganda iko nafasi ya 74, Rwanda iko nafasi ya 107, Tanzania ya 108 wakati DR Congo ni ya 111, Kenya 114, Ethiopia 123, Burundi 145, Eritrea 159, na Somalia 174.
Mwaka jana Kilimanjaro Stars ilifungwa na Somalia. Je, ni kutokana na udhaifu wa ligi? Je, baada ya Taifa Stars kuichapa Somalia kwa mabao 6-0 katika michuano ya CHAN Machi mwaka huu ligi imekuwa madhubuti?
Maximo atoe tathmini inayoeleweka si hii ya sasa.
Kwa uapnde wa Phiri, kipigo cha Simba hakitokani na udhaifu wa ligi bali ni kukosa wachezaji madhubuti wa kiungo. Katika kipindi chote cha ligi na hata mwanzo wa michuano ya kimataifa, Simba iliwategemea zaidi Mohammed Banka na Hilally Echessa.
Banka na Echessa ni kama muhimili katika timu ya Simba. Na kwa jinsi walivyocheza kwa uelewano katika msimu wote wa ligi, kukosekana kwao katika michuano ya Kombe la Kagame ni lazima timu itatetereka.
Banka alikuwa katika kiwango cha juu msimu ulioisha na kila mechi aliyocheza alikuwa msaada mkubwa kwa timu.
Kimsingi ndiye aliyekuwa mchezeshaji wa timu, huku akisaidiwa na Echessa ambaye alipangwa zaidi kucheza kiungo cha upande wa kulia.
Si kwamba Simba haina wachezaji wengine wanaoweza kucheza sehemu ya kiungo – wapo ila hawajafikia kiwango cha Banka. Juma Saidi Nyosso, Jerry Santo na Jabir Aziz wanaopangwa kucheza badala ya Banka hawajafikia kiwango chake.
Anapokuwa uwanjani Nyosso mashabiki wa Simba wanaamini wakati wowote atapewa kadi nyekundu au kutoa penalti. Si rahisi Nyosso kumaliza dakika 90 bila kuonyeshwa kadi kutokana na utumiaji wake wa nguvu zaidi kuliko akili.
Wakati anasajiliwa Jerry Santo katika dirisha dogo la usajili mashabiki wa Simba waliamini wamepata bonge la mchezaji. Lakini kila muda unavyo songa, mashabiki hao wanapoteza imani naye.
Mchezo wa Jerry ni taratibu. Akikutana na timu yenye viungo kama Banka lazima atashindwa kuhimili mchezo. Kwa kifupi ameshindwa kukonga nyoyo za mashabiki wa Simba waliokuwa na imani ya kupindukia kabla ya hata hawajamuona uwanjani.
Kwa mfumo unaotumiwa na kocha Phiri lazima timu iwe na mchezaji mwenye uwezo wa kuichezesha timu. Mwenye uwezo wa kuhangaika uwanja mzima na kufuta makosa ya wachezaji wengine.
Phiri asiogope kusema ukweli, wala asidhani kusema hivyo ni kuwapa kichwa Banka na Echessa. Ni haki yao na mwenye kustahili sifa apewe sifa zake.
Wajerumani leo wanalia kumkosa nahodha wao katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia, Michael Ballack, anayechezea Chelsea ya England.
Mwaka 2002 Ufaransa ililazimika kumtumia Zinedine Zidane katika fainali za Kombe la Dunia ilhali alikuwa majeruhi kwa sababu ndiye aliyekuwa na uwezo wa kuichezesha timu.
Hapa, haina maana Ufaransa haikuwa na wachezaji wengine wa kiwango cha Zizou, au si kwamba leo Ujerumani haina wachezaji wanaoweza kucheza nafasi ya kiungo anayocheza Ballack, hapana ila hawawezi kucheza kama anavyocheza yeye.
Kwa maneno mengine wanaona si rahisi kuziba pengo la Ballack.
Aidha, Liverpool ya England imeshindwa kushika hata nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi kuu ya England, sababu kubwa ikiwa ni majeraha ya wachezaji wake nyota, Fernando Torres na nahodha Steven Gerard.
Majeraha yaliwafanya muda mwingi kuwa nje ya kikosi hicho na kusababisha timu kukosa mwelekeo kwani wao ndio ni kama injini ya timu.
Hili ndilo tatizo la Simba. Hayo mengine mimi naona ni visingizio tu.