Mbatia: Tumefungua ukurasa mpya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

SASA uwezekano wa vyama vya upinzani kuungana, kukabiliana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeanza kuonekana.

James Mbatia, mwenyekiti wa taifa wa chama cha NCCR-Mageuzi amefuta kesi ya uchaguzi aliyoifungua dhidi ya mbunge wa Kawe (CHADEMA), Halima Mdee.

Makubaliano ya kufuta shauri hilo la madai yalifikiwa baada ya mazungumzo ya kina, baina ya viongozi wa kada mbalimbali kutoka NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Katika makubaliano, pande hizo mbili zimeafikiana “kuanza ukurasa mpya wa ushirikiano.” Katika kuonyesha kuna dhamira ya dhati ya kutaka kujenga umoja, mshikamano na ushirikiano endelevu, Mbatia amekubali kufuta kesi yake bila masharti yeyote.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI juzi Jumatatu, Mbatia amesema, makubaliano yaliyofikiwa yamevuka ngazi ya watu wawili – yeye Mbatia na Mdee – sasa yapo kwenye ngazi ya vyama vyao.

Alisema, “Haya si makubaliano ya mtu na mtu. Si ya James na Halima peke yao;  ni makubaliano ya vyama vyetu vya NCCR-Mageuzi na CHADEMA.”

Alipoulizwa nini kimemsukuma kufuta shauri hilo mahakamani, Mbatia alisema, “…migogoro ni jambo la kawaida; ikitumika vizuri inaweza kuimarisha mageuzi.”

Alisema, “Suala la ubunge wa Kawe ni dogo, lakini limetumika kama changamoto za kukutanisha vyama vyetu na kuibua mambo mazito yanayoweza kutupeleka mbele zaidi.”

Akiongea kwa sauti ya upole na iliyoonyesha umakini, Mbatia alisema, “Kwa hakika, vyama vyetu kwa dhamira ya dhati na ukweli, vimekubaliana kushirikiana kwenye ulingo wa kisiasa.”

“Tunataka kuhakikisha kwamba kila mwanya ambao unapatikana katika kutimiza lengo letu la kuiondoa CCM madarakani, tunautumia kufanikisha hilo,” aliongeza.

Naye Mdee akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dodoma anakohudhuria mkutano wa Bunge, amelieleza MwanaHALISI kwamba uamuzi uliofanywa na Mbatia umelenga maslahi ya taifa.

“Mheshimiwa James Mbatia, akiwa  mwanasiasa mwenzangu wa upinzani, ameona mbali zaidi. Ameona tuliposhinda Jimbo la Kawe, CCM na serikali yake walikuwa wamepata kiwewe na sasa walikuwa wanatumia kila hila kutaka kurejesha jimbo hili,” alisema Mdee.

Lakini kwa uamuzi wake huu, aliongeza, “sasa nitakuwa huru kuwatumikia wananchi wangu. Kwani ukiwa mbunge na papohapo ukawa na kesi mahakamani, unakuwa hujui kesho yako,” ameeleza Mdee.

Amesema, “Kinachofurahisha zaidi, ni kwamba Mheshimiwa James Mbatia ameondoa shauri lake mahakamani bila masharti ya kulipwa gharama. Hii yote inaonyesha jinsi alivyotanguliza mbele maslahi ya vyama vyetu na ukomavu wake wa kisiasa.”

Mdee ameahidi kuwa mara atakaporejea Dar es Salaam kutoka Dodoma anakohudhuria mkutano wa Bunge, atakwenda moja kwa moja kumuona mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi.

“Leo usiku (juzi Jumatatu) nimepanga kumtafuta kwa njia ya simu mheshimiwa Mbatia. Lakini nikifika Dar es Salaam nitafanya miadi ya kukutana naye ili kuanza ukurasa mpya wa ushirikiano wa kisiasa,” amesema.

Katika sauti yake nene, lakini mara hii ikisikika bila mkwaruzo, Mdee amesema, “Binafsi nitumie nafasi hii kumshukuru mheshimiwa Mbatia kwa maono yake na kuwashukuru pia viongozi wangu waliosimamia jambo hili.”

Alipoulizwa katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alivyopokea uamuzi huo mkubwa wa kuondoa shauri hilo mahakamani, haraka alisema, “Tumepata mahali pa kuanzia. Tunatarajia kwenda hatua zaidi mbele.”

Mbatia akizungumzia hatua kwa hatua jinsi makubaliano hayo yalivyofikiwa, anasema, pamoja na kwamba alikuwa na maamuzi yake katika suala hili, ikiwamo kuweza kukataa ushauri wa wenzake wa kuondoa shauri hilo mahakamani, lakini yeye kama kiongozi sharti aonyeshe mfano kwa wengine.

Anasema, “Ukiwa kiongozi usiwe mbinafsi. Nimekubali kuumia kwa faida ya vyama vyetu na taifa. Naamini tumepata mahali pa kuanzia. Tumeanza kufungua ukurasa mpya.

“Mgogoro huu umekuwa wa manufaa kwa kuwa umezaa jambo jema lililokuwa limeshindikana. Ni lile la kuwaleta wapinzani katika meza moja ya mazungumzo,” ameeleza.

Anasema mara baada ya kupokea ombi la CHADEMA la kutaka wafute kesi aliyoifungua kwa maslahi ya vyama vyao na taifa kwa jumla, haraka alikubaliana na ombi hilo kwa kile alichoita, “huwezi kuhudumia jamii kwa kutumia ubabe kama wafanyavyo watawala na vyama vya dola.”

Kuhusu mengine yaliyofikiwa, Mbatia hakuwa tayari kueleza zaidi ya kusema, “Tumekubaliana kushirikiana, maana umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Tumekubali kusema, makosa yetu ya jana yamekuwa fundisho leo.”

Anasema hati ya makubaliano iliyopelekwa mahakamani ilizuia vyama hivyo kushambuliana majukwaani; yeye hana kinyongo juu ya mambo ya nyuma yaliyotokea wakati wa uchaguzi na hivyo ameamua “kwa nia safi, kufungua ukurasa mpya wa kisiasa.”

Kwa mujibu wa Mbatia, makubaliano hayo hayataishia ngazi ya viongozi wa juu kama ilivyofanyika, bali yatapelekwa kwenye vikao rasmi vya chama kubarikiwa na kuwekewa mwongozo wa utekelezaji.

Alipoulizwa kwa nini hayakuanzia kwenye vikao, Mbatia alisema, “Masuala makubwa kama haya hayawezi kuanzia kwenye vikao vya juu, lazima yaanzie kwa watu wachache ndipo vikao viingie ku-formalize.

“Ukianzia huko juu, huwezi kufanikiwa. Unajua kwamba kwenye vikao vya wengi kuna vitu vingi; baadhi ya watu ni wabinafsi, wengine ni wapambe na wengine wanaangalia maslahi fulani.”

Anasema, “Mfano, hata suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama lingeanzia kwenye vikao lisingefanikiwa, lakini Mwalimu Nyerere (Julius) na Karume (Abeid Aman) walikaa pamoja na baada ya kukubaliana ndio wakapelea makubaliano kwa wengi.”

Mfano mwingine, ambao Mbatia anauelezea kuhalalisha hatua ya vyama hivyo viwili kutopeleka suala hilo kwenye vikao vyake kwanza, ni mabadiliko ya katiba.

Mbatia alipoulizwa uhusiano wake na Marando alisema, “Marando ni rafiki yangu. Sote ni wanamageuzi. Mwaka jana alinialika kwenye harusi ya mtoto wake, nilikaa naye kwenye jukwaa kuu pamoja na Dk. Slaa. Kwa hiyo, sisi hatuna uadui, tunashirikiana kwenye masuala ya kijamii.”

Kuhusu vyama kuungana katika chaguzi, Mbatia anasema, “Hayo ya kuungana ndiyo yatazungumzwa katika hatua ya juu zaidi ya vikao vya vyama vyetu, maana ndiyo Watanzania wanayoyataka. Hii ni pamoja na ushirikiano katika chaguzi zinazokuja na mengineyo.”

Kufikia makubaliano hayo, kwa mujibu wa Mbatia halikuwa jambo rahisi. Kulikuwa na vikwazo vingi ambavyo kila upande ulilazimika kufunika maslahi binafsi na kuangalia maslahi mapana ya umma.

Anasema, “…nimeamua kuchukua hatua hii kwa maslahi ya mambo mazuri zaidi. Niliona si busara kuendeleza minyukano kati ya upinzani na upinzani, kwa sababu ina athari kubwa kwa jamii. Heri minyukano ingekuwa kati yetu na chama tawala,” anaeleza.

Mara baada ya kufuta kesi, viongozi wa pande zote mbili walikutana na waandishi wa habari katika ofisi za NCCR-Mageuzi, Ilala.

Mkutano huo ulihudhuriwa, pamoja na wengine, Katibu Mkuu wa NCCR, Sam Ruhuza, wakili wa Mbatia, Mohammed Tibanyendera, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala CHADEMA, Anthony Komu na mawakili wa Mdee, Edson Mbogoro na Mabere Marando.

Marando na Komu walijiunga na CHADEMA wakitokea NCCR. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Marando kufika kwenye ofisi za chama hicho tangu mwaka 2008.

0756 346175
0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: