Mbatia: Ubunge wangu si zawadi


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia

JAMES Mbatia anasema hajapata kuandika barua kwa Rais Jayaka Kikwete ya kuomba ubunge. Mwenyekiti huyo wa Chama cha NCCR-Mageuzi, amesema kwa sababu hiyo, kuteuliwa kwake kuwa mbunge, si zawadi.

Wala uteuzi huo, anasema, hauwezi kuchukuliwa kuwa amepewa nafasi hiyo ili awe kibaraka wa rais.

Katika mahojiano na MwanaHALISI yaliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, Mbatia amepuuza hisia walizonazo baadhi ya watu kwamba amezawadiwa ubunge.

“Wanaosema mimi kuteuliwa mbunge na rais nimezawadiwa wafahamu mimi si kibaraka wa rais wala wa chama chake CCM,” amesema.

Anasema kuthibitisha hilo, alipokula kiapo cha ubunge, aliapa kuilinda katiba ya nchi siyo rais.

Mbatia aliteuliwa Mei mwaka huu na rais kwa mamlaka ambayo rais amepewa kupitia ibara 66(1)(c) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

“Nimeteuliwa ili kusaidia wananchi kwa matarajio yao. Hata rais mwenyewe analijua hili.”

Marais waliopata kufanya hivyo ni wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na hata Rais Kikwete alifanya hivyo katika kipindi cha kwanza.

Mkapa alimteua Hamad Rashid Mohamed wa Chama cha Wananchi (CUF) mwaka 2002 kufuatia muafaka uliosainiwa na CCM na CUF baada ya vurugu zilizoleta mauaji ya raia waandamanaji visiwani Zanzibar.

Rais Kikwete katika awamu ya kwanza ya uongozi wake, alimteua Ismail Jussa Ladhu, pia kutoka CUF, kuwa mbunge, miezi michache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010.

Mbatia anasema imani yake ni kwamba rais amepima mchango wake kwa jamii ndipo akamteua.

“Mheshimiwa rais Kikwete anajua uwezo wangu. Anajua ninavyoongoza chama chetu. Sasa haya yanachangia kiongozi kumtambua mtu anayetaka kumteua,” anasema.

Mbatia anakumbukwa kwa msaada aliotoa wakati wa mafuriko ya Desemba 2011 ambayo pia yalikumba eneo la bonde la Kawe.

Alipodokezwa uvumi kwamba NCCR-Mageuzi ina unasaba na CCM, haraka alijibu, “Haiwezekani na haitawezekana hata siku moja.”

Mbatia anasema NCCR-Mageuzi sasa ni chama imara chenye uwezo wa kusimama baada ya kukutwa na misukosuko mingi.

Anataja msukosuko wa kwanza wa mwaka 1994 akisema baadhi ya waasisi kama vile Prince Bagenda na Oswald Mashaka waling’oka na kuunda NCCR-Asilia.

“Hapo tuliyumba,” anasema Mbatia na kuongeza kuwa chama kilirudi kwenye mstari na kuaminiwa baada ya kujiunga Augustine Mrema Machi 1995.

Mrema alipitishwa na mkutano mkuu wa chama kuwania urais ambapo alipata asilimia 28 ya kura. Walipata viti 16 vya ubunge.

Mbatia anatamba leo kuwa kama si uhuni uliofanyika kwa majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam kuuvuruga uchaguzi, “Mrema angekuwa rais wa awamu ya tatu.”

Anakumbuka, “Haiingii akilini… vifaa vya kupigia kura viwe vimefika kwa wakati mikoani, tena mikoa ya mbali kama Kigoma na Mtwara au Ruvuma, lakini visifike Kawe, Dar es Salaam.”

Wajumbe wengi wa kamati kuu ya NCCR-Mageuzi walishinda ubunge hali anayosema ilichangia kuibua mgogoro kwani “baadhi ya viongozi waandamizi waliokuwa si wabunge waliangalia kibinafsi mafanikio hayo.”

Mbatia ambaye yeye alikuwa mbunge wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro, anasema viongozi hao walileta hoja kuwa wabunge ambao walikuwa na nafasi za uongozi katika chama waachie nafasi zao kwa kuwa “siasa hazifanywi bungeni bali hufanywa nje ya bunge.”

Anasema Mrema ambaye hakuwa mbunge alishika kundi lililoleta hoja hiyo huku Marando aliyekuwa mbunge wa Rorya, mkoani Mara, akiwa kinara wa kundi la wabunge.

Mbatia ambaye wakati huo alikuwa mkurugenzi wa uchaguzi, anajivunia rekodi anayodai haijavunjwa ya mbunge wa upinzani ya kushinda kiti kwa asilimia 85.

Mgogoro huo ulimegua chama hicho. Mrema alihamia Tanzania Labour Party (TLP) akikaribishwa na Leo Lekamwa aliyekuwa mwenyekiti, huku viongozi wengine wakiongozwa na Marando wakibaki kukiimarisha.

Hali ilikuwa ngumu kiasi cha kutoaminika tena na hivyo kikashindwa kufanya vizuri kwenye uchaguzi wa pili wa 2000.

“Ni mgombea mmoja tu aliyerudi,” anasema Mbatia, akimtaja Kifu Ghulamhussein Kifu wa jimbo la Kigoma Kusini.

Kifu mwenyewe alipigwa kumbo mwaka mmoja na nusu baadaye, baada ya mahakama kuu kutengua ubunge wake kutokana na kesi iliyofunguliwa kupinga matokeo.

Alichaguliwa mwenyekiti mwaka 2000 akimrithi Haidary Maguto aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo tangu Mrema alipotoka.

Mbatia anasema alilazimika kuanza upya kujenga chama na ilipofika uchaguzi wa 2005 wakashiriki lakini hawakuambulia hata kiti kimoja cha bunge.

“Kasoro tuliona ni zilezile kwamba watu bado hawatuamini na hatukuwa na rasilimali fedha maana hatukuwa na ruzuku na wafanyabiashara walitukimbia.

“Hivyo tukajikusanya na kwa kile kidogo tulichopata, tukasema tuwekeze kwenye eneo dogo la nchi.

“Takwimu na tathmini ilitukusuma tuwekeze Kigoma. Tukafanyia kazi ili angalau tupate wabunge wawili. Ooh Mungu mkubwa, tukapata majimbo manne,” anasema.

Awali, anasema yeye aliamua kutogombea jimboni kusudi aweke nguvu katika majimbo ambayo waliona kulikuwa na dalili za wagombea wao kushinda.

Hata hivyo, chama kilimkatalia. “Wakasema lazima nigombee, ndipo nilipogombea Kawe. Matokeo ni kama Tume ilivyotangaza Halima Mdee wa CHADEMA kuwa ndiye mbunge wetu.”

Mbatia alimkatia Mdee rufaa lakini aliifuta kesi kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kile alichosema “Haina maana kuendeleza malumbano katika vyama vya siasa hasa vya upinzani.”

Kwa dhana hiyohiyo ya yeye kutopenda vyama vya upinzani kupingana, Mbatia anasikitika kuona viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakishambulia chama chake pamoja na CUF katika jitihada za kutafuta wanachama.

Akiwa ndiye mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), anasema lazima vyama hivyo viheshimiane na kutoa nafasi kwa utu.

“Hapa nina maana siasa za amani na utulivu zichukue nafasi yake badala ya malumbano na kushambuliana ambako hakuna tija,” anasema.

Anasema kazi kubwa iliyopo kwao ni kujenga vyama imara dhidi ya nguvu za CCM ili kuking’oa madarakani uchaguzi ujao.

Ana matumaini kuwa NCCR-Mageuzi kitashinda kesi ya kupinga matokeo ya ubunge jimbo la Babati Vijijini ambako walimsimamisha Laurent Tala.

Akigusia mgogoro mpya uliotaka kumegua tena chama, Mbatia anasema aliyekuwa Katibu Mwenezi, David Kafulila, alianza chokochoko   ndipo alipoadhibiwa na mkutano wa Halmashauri Kuu.

“Tulimfuta uanachama baada ya wajumbe kukataa kurudia kule walikokusahau,” anasema na kuongeza kuwa ingawa yeye alimsamehe, “wenye chama walikataa.”

Kafulila alifungua kesi mahakama kuu kupinga uamuzi huo na mahakama imeamua kuwa angali mbunge halali mpaka kesi aliyofungua itakapoamuliwa.

Kwa sasa, Mbatia anasema chama kinazidi kuimarika kutokana na kuongozwa vizuri.

Kuhusu ukusanyaji maoni ya katiba mpya ya nchi, anasema moja ya maeneo muhimu kuangaliwa ni kupunguza madaraka makubwa ya rais.

Anasema ukiritimba huo wa madaraka unatoa mwanya ya kukuza ufisadi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: