Mbivu, mbichi kuhusu Bodi ya Mikopo


Petro Eusebius Mselewa's picture

Na Petro Eusebius ... - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version

BODI ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) iliyoanzishwa kwa Sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuzinduliwa 30 Machi 2005, imethibitika kuwa imeshindwa kazi.

Aliyezindua Bodi hiyo Julai 2005, alikuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Pius Ng’wandu.

Wanafunzi waliotumia huduma za Bodi kwa mara ya kwanza ni wale wa mwaka wa masomo wa 2005/2006 ulioanza Septemba.

Msingi wa kwanza mkuu wa kuanzishwa kwa HESLB ilikuwa kusaidia wanafunzi wa elimu ya juu waliokuwa wamepata udahili kwenye vyuo vikuu, lakini hawakuwa na uwezo wa kugharimia masomo yao.

Kwa kifupi HESLB ipo kwa ajili ya wanafunzi kutoka familia ‘maskini’ waliodahiliwa vyuoni.

Labda tujiulize, kwa nini mara zote kila ukifanyika mgomo wa wanafunzi bodi hutupiwa lawama? Je, inatenda haki kufanikisha elimu ya wanafunzi? Wanaopata mikopo ndio waliotarajiwa? Kama sivyo, tatizo hasa liko wapi?

Ingawa mimi si mtaalamu wa Bajeti ya Serikali, naamini kuwa serikali zilizopita na iliyopo hazikuwa na wala haina uwezo wa kulipia gharama za masomo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa vyuo vikuu.

Kuna sababu nyingi. Moja kubwa ni kwamba si kila mwanafunzi hana uwezo. Wapo wanaohitaji mikopo kweli, lakini wapo tena wengi  hawastahili kukopeshwa.

Hawa ‘na sisi-tupate’ wana uwezo lakini husababisha tu vurugu vyuoni. Hawa ni watoto wa familia zenye kipato cha wastani na cha juu. Hawa ni tatizo.

Jambo jingine ambalo yafaa watu waelewe ni kwamba matatizo yaliyopo sasa kwenye mikopo yalianza punde tu Bodi ilipoanza kuchapa kazi.  Bodi ilianzishwa kisiasa zaidi.

Wakati HESLB inaanzishwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) klikuwa katika maandalizi ya kutetea kiti chake cha uongozi wa nchi hii katika uchaguzi mkuu mwaka 2005. Kilifanikiwa baada ya Jakaya Kikwete kuchaguliwa kuwa rais mwaka 2005.

Ili kusafisha njia na kuteka nyoyo za wananchi wapenda elimu, serikali ilitangaza kuzaliwa mfumo wa ukombozi kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Ikatangaza kuanzishwa na kuanza kazi kwa Bodi ya Mikopo.

Mwenye nacho na asiye nacho wote waende serikalini kupata mikopo. Mwanafunzi alitakiwa kufika na kitambulisho kimoja tu muhimu: udahili. Udahili umetoka wapi halikuwa swali la msingi kwa serikali ‘sikivu’.

Wale waliokuwa wakijisomesha kwa fedha zao pia hawakusahauliwa. Nao walialikwa kwenye tafrija hiyo nono ya mikopo.

Na zaidi, hata wanafunzi wa kidato cha sita waliomaliza Machi 2005, walihamasishwa na kukaribishwa kujiunga na vyuo vikuu bila hata ya kulaza mwaka mmoja na miezi minne mitaani kama ilivyokuwa mwanzo.

Wakaunganisha moja kwa moja vyuoni. Kipaza sauti cha serikali kikaita huku na kule na kutangaza neema ya kupatikana faraja kwa ‘maskini’ wengi: mikopo.

CCM, kwa sera yake hiyo ikakomba asilimia 82 ya kura katika uchaguzi mkuu wa 2005 huku ikiacha moto kati ya Bodi na wanafunzi wa elimu ya juu.

Walijitokeza wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani walioona matatizo mapema katika mfumo huo wa utoaji mikopo, wakalalamikia utendaji usioridhisha wa HESLB.

Malalamiko yakaendelea, migomo ikaendelea, serikali na Bodi zikajitetea, kila mmoja akisema na kufanya lake. Hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyewahi kukiri kitovu cha tatizo.

Ukweli ni kuwa siasa iliharibu kila kitu. Kura zikawala wanafunzi na Bodi. Kumbe wakati serikali inatangaza faraja ilikuwa haijaangalia mfukoni mwake. Haikuwa na fedha za kuwalisha na kuwanywesha waalikwa wote hao.

Baadaye, ikatangaza sasa ni daraja la kwanza na la pili tu ambao wanastahili mikopo. Halafu wanafunzi wa ualimu na sayansi wakaruhusiwa hata kwa daraja la tatu.

Pia madaraja mbalimbali ya mikopo yakawekwa. Vigezo vya kuwapata wa daraja husika vikaendelea kuwa tatizo. Waka wamechelewa sana, kwani vyuo vikuu vilikuwa vimeongezeka kama shule za sekondari.

Kwanini? Jibu ni rahisi. Serikali ilihitaji barua ya udahili tu wa wanafunzi bila ya kujali zinakotoka. Makosa makubwa!

Yaweza kusemwa kuwa HESLB imezidiwa nguvu na mikopo. Haina fungu la kutosheleza gharama za kila mwombaji.

Sasa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-Mlimani, Chuo Kikuu cha Ardhi na Chuo cha Ustawi wa Jamii wameanza mchakato kwa njia ya mgomo na maandamano (kuanzia Februari 3, 2011) wa kutaka waongezewe fedha za kujikimu kutoka Sh. 5000 hadi Sh. 10000 kwa siku.

Wanahoji kuwa ikiwa gharama za maisha zimepanda pamoja na mishahara, kwanini ‘boom’ (mgawo huu wa fedha) lisipande? Wana malalamiko mengine zaidi ya hayo ambayo si sehemu ya makala hii. Huu utakuwa msumari wa moto mwingine kwa Bodi.

Jamani huruma! Serikali isingelipelekeshwa na joto la uchaguzi wa 2005, labda isingelifanya ilivyofanya. Labda ingeanza na waliofaulu vyema kwanza kama ilivyokuwa kabla ya Bodi, halafu wa vyuo vya umma, halafu vya binafsi. Hatua kwa hatua.

Ikumbukwe kuwa kabla ya Bodi ya Mikopo,Serikali ilikuwa ikifanya jambo jema sana la kuwasomesha wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma waliofaulu kwa kiwango cha juu na waliokuwa hawana uwezo.

Iliamininika na kufanyika kuwa wale waliokuwa na ufaulu wa wastani na wa chini walijisomesha wenyewe. Hivi ndivyo ilivyokuwa kabla ya mwaka 2005 katika vyuo vya umma na binafsi. Lakini sasa wote wanapanga foleni ya mikopo.

Sina hakika kama wote wanastahili. Si wameitwa na Serikali kwanini wasiende?

Serikali iangalie vyema suala hili na kulifanyia kazi. Yaweza kurudi nyuma halafu kusonga mbele ikitokea nyuma. Wanaostahili wapate, wasiostahili waambiwe: hamstahili.

Au, bajeti ya Bodi iongezwe maradufu ili kila aliyealikwa kwenye tafrija ya mikopo ale na kunywa kwa raha zake. Hata kama Bodi itavunjwa kama ilivyopendekezwa na Umoja wa Vijana wa CCM, tatizo litabaki.

Kwani Bodi ikishavunjwa, haiyaundwa nyingine? Je, itakuwa imepata uwezo kifedha? Hapa serikali itimize ilichoahidi kwa kipaza sauti kikubwa mwaka 2005 au iwe tayari kupokea lawama badala ya HESLB.

Mwandishi wa makala haya, Petro Eusebius Mselewa, amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa simu: 0713 111171
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)